Jumatano, 19 Aprili, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 21 Rajab 1438 Hijria sawa na Aprili 19, 2017.
Miaka 2050 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nadharia za wanahistoria, yaani tarehe 19 Aprili mwaka 33 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (as), kulianzishwa mjini Roma maktaba ya umma 'Public-Library' ya kwanza kabisa duniani ambayo kila mwenye uwezo wa kusoma na kuandika alikuwa na haki ya kuingia humo na kusoma vitabu alivyotaka. Kabla ya Waroma, Wasumeri, Waashuri, Wababeli na Wairani walikuwa na maktaba zao ingawa maktaba hizo hazikuwa zikitumika na watu wote, na maktaba ya Waashuri ikiwa ndio maarufu zaidi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, nchi ya kwanza ambayo ilianzisha asasi za uandishi na tarjama za vitabu duniani, ilikuwa Iran, ambapo katika karne ya 15 zilikuwa zikifanya kazi katika utawala wa Khosrow Anushirvan wa wakati huo.
Siku kama ya leo miaka 1190 iliyopita mwezi wa Rajab mwaka 284 Hijiria, alifariki dunia Abu Hatam, Sahal bin Muhammad Sajestani. Abu Hatam alikuwa ametabahari katika elimu ya Qur'ani, hadithi, fasihi na mashairi. Mbali na kuwa alikuwa akiisoma Qur'ani Tukufu na kuifundisha kwa mapenzi makubwa, Abu Hatam pia alijishughulisha na masuala ya kijamii. Msomi huyo ameacha vitabu vingi miongoni mwavyo ni I'irabul Qur'an', na Akhlaqul Insan.
Siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, sawa na tarehe 19 Aprili 1807, majeshi ya Uingereza yalilazimika kuondoka katika mji wa bandari ya Alexandria nchini Misri, baada ya kushindwa kukabiliana na jeshi la Misri. Ikiwa ni katika njama za kutanua wigo wake wa utawala wa kikoloni, Uingereza ilichukua uamuzi wa kuishambulia na kuiteka Misri ambayo ilikuwa sehemu ya ardhi ya utawala wa Othmaniya. Baada ya kuanza mashambulizi hayo na mji wa Alexandria kutekwa na Uingereza, maulamaa na wanazuoni wa nchi hiyo walitoa fatwa ya kuanzishwa vita vitakatifu dhidi ya wavamizi, kwa shabaha ya kuikomboa Misri kutoka kwa wavamizi wa Kiingereza.
Tarehe 19 Aprili miaka 24 iliyopita, polisi ya Marekani FBI ilishambulia makao ya wafuasi wa kundi la David na kuua watu 80 miongoni mwao. Wafuasi wa kundi hilo ambao wanapinga vikali siasa za serikali ya Marekani walishambuliwa na kuuawa na askari wa FBI baada ya kuzingirwa katika makao yao kwa siku kadhaa. Mauaji ya wapinzani wa serikali katika nchi kama Marekani inayodai kutetea uhuru wa kusema na kuabudu na haki za binadamu yaliwashangaza watu wengi duniani na kuifedhehesha serikali ya Washington.

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, Kadinali Joseph Ratzinger alikabidhiwa uongozi wa Kanisa Katoliki Duniani baada ya kufariki dunia Papa John Paul wa Pili na kuchagua jina la Papa Benedict wa 16. Ratzinger alizaliwa mwaka 1927 nchini Ujerumani na alipanda daraja na kuwa askofu mwaka 1977 na hatimaye kufikia daraja ya ukadinali. Papa Benedict wa 16 alikabiliwa na matatizo mbalimbali akiwa kiongozi wa kanisa hilo ikiwa ni pamoja na mgogoro wa masuala ya kiroho katika nchi za Magharibi, ufisadi na utovu wa na Saadili pamoja na vitendo vya ubakaji vinavyofanywa na maaskofu na makasisi dhidi ya watoto wadogo. Papa Benedict wa 16 alilazimika kuachia uongozi wa Kanisa Katoliki Februari mwaka 2013 baada ya kuzongwa na kashfa nyingi za viongozi wa ngazi za juu ndani ya kanisa hilo.