May 23, 2017 03:20 UTC
  • Jumanne, Mei 23, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 26 Shaaban 1438 Hijria sawa na tarehe 23 Mei mwaka 2017 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 1333 iliyopita inayosadifiana na mwezi 26 Shaaban mwaka 105 Hijria, Yazid bin Abdul Malik bin Marwan, khalifa mkandamizaji wa Bani Umayyah, alifariki dunia. Yazid bin Abdul Malik bin Marwan alichukua ukhalifa wa Bani Ummayah baada ya Omar bin Abdul Aziz, mwaka 101 Hijria. Abdul Malik bin Marwan alikuwa mtu mwenye maadili maovu na mbadhirifu wa mali na hakuwa akijishughulisha kabisa na masuala ya dola ya Kiislamu. Alikuwa ni jamaa wa Hajjaj Thaqafi, hivyo watu wengi wa ukoo huo waliingia katika utawala wake. Mwishoni mwa umri wake, Abdul Malik bin Marwan alitaka kuthibitisha kuwa starehe na anasa za dunia zinaweza kuwa bila ya machungu. Lakini baada ya siku chache, mpenzi wake wa kike alifariki dunia, hivyo maisha yake ya kupenda anasa za dunia yakabadilika kuwa machungu na haikupita siku nyingi ila na yeye alifariki dunia.

 

Siku kama ya leo miaka 399 iliyopita, yaani tarehe 23 Mei 1618 Milaadia, vilianza vita vya miaka 30 vya kidini barani Ulaya. Madhehebu ya Kikristo ya Kiprotestanti yaliundwa mwanzoni mwa karne ya 16 Milaadia na hivyo kuzusha mpasuko mkubwa katika safu za Wakristo. Baada ya hapo, Wakristo wa madhehebu mawili ya Kikatoliki na Kiprotestanti waliingia vitani kwa karne nyingi. Moja ya vita maarufu baina ya Wakristo wa madhehebu hayo mawili, ni vile vilivyotokea kwenye muongo wa pili wa karne ya 17 Milaadia. Vita hivyo viliendelea kwa muda wa miaka 30 mfululizo. Sehemu kubwa ya vita hivyo ilitokea nchini Ujerumani. Vita hivyo vilikuwa na pandashuka nyingi. Katika kipindi chote cha vita hivyo, nchi za Ufaransa, Sweden na Denmark ziliwaunga mkono Wakristo wa Kiprotestanti na serikali ya Uhispatia na Ufalme wa Roma waliwaunga mkono Wakatoliki. Vita vya miaka 30 baina ya madhehebu mawili ya Wakristo huko barani Ulaya, vilimalizika kwa kutiwa saini makubaliano ya Westphalia mwaka 1648 Milaadia. Ijapokuwa uhasama mkubwa baina ya Wakristo wa Kiprotestanti na Kikatoliki ulitokana na ugomvi wa muda mrefu baina ya madhehebu hayo mawili, lakini sababu kubwa za vita hivyo ilikuwa ni kugombania ardhi na masuala ya kisiasa ya tawala za wakati huo barani Ulaya. Moja ya matokeo muhimu ya vita hivyo ni kumalizika kwa namna vita vya kimadhehebu baina ya madhehebu hayo mawili ya Kikristo na kuanza kupata nguvu mirengo ya utaifa na ya ubaguzi wa rangi na kizazi barani Ulaya.

Vita vya miaka 30 mfululizo baina ya Wakristo wa Kiprotestanti na Kikatoliki

 

Na siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, yaani tarehe 23 Mei 1915 Milaadia, Italia ilijiingiza katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Kuingia Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia kulianza wakati nchi hiyo ilipoivamia Austria bila ya sababu yoyote isipokuwa tu kwa tamaa ya kujinufaisha kisiasa na kupanua utawala wake. Muda mchache baadaye, serikali ya Italia ilitangaza vita dhidi ya ufalme wa Uthmania na hivyo kuufanya moto wa vita uwake kwa ukali zaidi. Hata hivyo, licha ya kupata ushindi kundi la nchi Waitifaki, Italia ikiwa moja yao, lakini nchi hiyo haikufaidika kivyovyote na vita hivyo. Matunda pekee iliyopata ni kuwaulisha raia wa Italia baada ya kuwaingia Waitaliano milioni tano na nusu katika vita hivyo. Kwa maneno mengine ni kuwa maamuzi na siasa za Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia zilifeli, kwani haikupata matunda yoyote ya maana kwa kujiingiza kwake kwenye vita hivyo.

Vita vya Kwanza vya Dunia