Mar 15, 2016 10:35 UTC
  • Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (12)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 12 ya mfululizo huu.

Kama mnavyokumbuka wapenzi wasikilizaji, katika vipindi vilivyopita tulisema kuwa Uislamu, tangu mwanzo wake, ulikuwa ukiwashajiisha watu kuifunza na kujifunza elimu. Katika baadhi ya hali na mazingira, Uislamu umewajibisha kwa wafuasi wake kujifunza elimu za kimaada na za jarabati. Kwa hivyo hakujawahi kuwepo mgongano na makabiliano baina ya elimu za sayansi za jarabati na mafundisho ya dini ya Uislamu. Nukta nyengine muhimu ni kwamba Uislamu haujawahi katu kukana mfumo wa sababu za vitu, bali kinyume na mitazamo ya kale iliyozoeleka miongoni mwa wafuasi wa dini zilizopita, dini hiyo tukufu inauangalia mfumo wa dunia kuwa umejengeka juu ya mfumo wa sababu na visababishi. Lakini hiyo haina maana ya kupunguza au kukana utawala wa Mwenyezi Mungu; bali mfumo wa sababu katika ulimwengu wa kimaada uko chini ya majimui (au unafuatana na) ya utendaji wa Mwenyezi Mungu.

Ukweli ni kwamba kile ambacho katika istilahi za falsafa kinajulikana kama mfumo wa ulimwengu na "kanuni ya sababu", katika lugha na misamiati ya dini kinajulikana kama "Sunnat-Allah". Kulingana na mafundisho ya Uislamu, kama ambavyo kuwepo kwao viumbe hakujivui na utegemezi kwa Mwenyezi Mungu, ni vivyo hivyo haujivui na utegemezi katika kuathiri kwao juu ya mambo. Kwa msingi huo, Uislamu haupingi, bali unakubaliana hasa na nadharia-tete ya elimu za jarabati juu ya kuwepo mfumo wa usababishaji katika ulimwengu wa maumbile. Lakini kwa mujibu wa Uislamu suala hili haliishii hapa.

Nukta kuu na ya msingi zaidi katika kuzungumzia Usayansi ni kwamba maudhui inayojadiliwa katika elimu za jarabati ni hali mahususi za ujudi na athari zake. Amma kuuzungumzia ujudi wenyewe na aina zake, huo ni mjadala wa kiakili na kimantiki tu na inapasa waachiwe wanafalsafa. Vilevile kwa upande wa masuala yanayohusu akhlaqi, elimu juu ya ulimwengu pamoja na elimu nyengine za mantiki na akili, yote hayo ni mambo yaliyo nje ya jarabati. Wanafalsafa na wanafikra wengi, hata bila ya kutegemea mafundisho ya dini; bali kwa kutumia akili zao tu wamethibitisha kuwepo ulimwengu nje ya huu wa kimaada, ulimwengu ambao una kanuni na nidhamu zake maalumu. Na si kwamba hakuna mahusiano yoyote baina ya ulimwengu huo usio wa kimaada na huu wa kimaada; bali kuna hali ya athari na kiathiriwa inayotokana na sababu na kisababishwa. Kwa maana kwamba ulimwengu usio wa kimaada unaweza kuwa na athari kwa ule wa kimaada; na aina hiyo ya "taathira" nayo pia ni sehemu ya mfumo wa sababu halisi japokuwa haufahamiki katika njia za jarabati na majaribio. Kuna njia nyengine pia ikiwemo ya akili na wahyi ya kumbainishia mwanadamu jinsi taathira hiyo ilivyo na inavyofanya kazi. Kwa hivyo "ujudi" au uwepo wa kitu si wa kimaada tu; na mfumo wa sababu na visababishi haukomei kwenye ulimwengu wa kimaada tu. Suala hili ni miongoni mwa mafundisho ya msingi ya Uislamu.

Shahidi Murtadha Mutahari, mwanafikra mkubwa wa Kiirani anasema: "Wayakinifu, kwa kimombo Materialists, wamekosea kwa kuchukulia kwamba sehemu tu ya kanuni za maumbile za ulimwengu ambazo zimegunduliwa na sayansi ndizo kanuni halisi; kisha wakaichukulia miujiza kuwa ni kitu kinachokinzana na kanuni. Sisi tunasema yale yaliyoelezwa na sayansi ni ya kweli na sahihi katika mpaka na mazingira maalumu, na pale linapofanyika jambo lisilokuwa la kawaida kwa irada ya Mtume au walii wa Mwenyezi Mungu huwa kinaingia kisababishi maalumu kinachotokana na sababu zisizokuwa za kimaada. Kwa hivyo muujiza maana yake si kutokea jambo lisilo na sababu hata tuseme kuwa ni kitu kisicho na maana na kisichokubalika. Hoja hii sio tu inatumika katika kubainisha miujiza bali pia ina itibari katika kubainisha jinsi dua, kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kuamini irada ya Mola vilivyo na taathira katika maisha ya mtu." Shahidi Mutahari vilevile anasema: "Wengi wao hivi sasa wamebaini kuwa Usayansi (kuamini sayansi tupu) na malezi ya kisayansi matupu hayawezi kutengeneza mwanadamu aliyekamilika. Malezi ya kisayansi matupu yanatengeneza nusu ya mwanadamu, si mwanadamu kamili."

Kwa hivyo tunachoweza kusema ni kwamba Usayansi, kwa maana ya kubana njia za utambuzi wa mambo za mwanadamu kwenye utumiaji jarabati na majaribio tu na kutupilia mbali njia nyengine zote za utambuzi, haukataliwi na Uislamu pekee bali na hata wanafikra wenyewe wa Magharibi. Kwa hivyo moja ya misingi muhimu ya kifikra ya Usekulari, ambao nadharia hiyo ilikuwa ikiutegemea kwa karne kadhaa umeonekana ni kitu kisicho na itibari.

Tukiendelea na mazungumzo yetu sasa tunautupia jicho msingi mwengine wa Usekulari ambao ni Urazini kwa kimombo Rationalism kwa maana ya kutegemea misingi ya akili katika fikra, mwenendo na matendo. Waasisi wa fikra na nadharia hii iliyoibuka katika karne ya 17 walikuwa ni René Descartes, Baruch Spinoza na Gottfried Leibniz. Makusudio yao kuhusu Urazini yalikuwa ni kwamba akili ya mwanadamu ndio chanzo pekee cha kuaminika kwa ajili ya utambuzi wa mambo. Kwa matazamo wa Spinoza, utambuzi una anuai kadhaa ambazo zote zinatokana na akili. Warazini walikuwa wakiitakidi kuwa jarabati na ushuhudiaji ni masuala tete mno kuweza kuaminika kwa utambuzi wa mambo. Wanafikra hao walitaka kuthibitisha hakika za ulimwengu wa maumbile kwa kutegemea njia moja tu ya hoja na burhani za kiakili.

Warazini wanaamini kuwa ni kwa kutumia njia maalumu za kiakili ndipo itawezekana kuwa na ujuzi wa yakini wa mambo. Ujuzi wa aina hiyo hauwezekani kuwa wa makosa na usio sahihi katika hali na mazingira yoyote yale. Kauli maarufu ya Descartes kwamba: “Ninafikiri, kwa hiyo basi nipo” ni mfano wa hiyo shaka juu ya jarabati na masuala ya hisi. Kwa mtazamo wake yeye kile alichokuwa akikiona na kukihisi hakukikubali kuwa ni kitu cha kumfikisha kwenye yakini ya jambo, hivyo akawa hata na shaka kama yeye mwenyewe pia yuko kweli au la. Na kwa sababu hiyo akawa anatafuta sababu ya kimantiki na kiakili tu kwa ajili ya kuthibitisha kuwepo kwake yeye mwenyewe. Alikuwa akisema, mimi nina shaka juu ya kuwepo kwa vitu vyote; lakini sina shaka juu ya “kuwa na shaka kwangu”; na “kuwa na shaka” ni hoja ya kiakili juu ya kuwepo “mwenye shaka”. Ni kwa sababu hiyo alikuwa akijenga hoja ya kusema:”Ninafikiri, basi kwa hiyo nipo”.

Wanaurazini wengi kama Spinoza na Descartes walikuwa wakitumia hoja ya kiakili kuthibitisha kuwepo kwa Mungu na ulimwengu wa akhera; na katika hilo walikabiliana na wanafikra wenye mielekeo ya kijarabati, ambao walikuwa wakisema, kwa kuwa Mwenyezi Mungu hawezi kufahamika kwa njia ya hisi, kwa hivyo haiwezekani kumtambua.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mtajiunga nami tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kheri na fanaka maishani…/

Tags