Jumatano Agosti 16, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 23 Dhulqaada 1438 Hijria sawa na Agosti 16, 2017
Siku kama leo miaka 129 iliyopita, alizaliwa Thomas Edward Lawrence, jasusi mkubwa wa Uingereza aliyekuwa na mchango mkubwa katika kuzidhoofisha nchi za Kiarabu. Kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia Lawrence, alikuwa amefanya safari katika nchi kadhaa za Kiarabu ambapo alijifunza lugha ya Kiarabu na kutambua tamaduni na maisha ya Waarabu. Katika vita hivyo vya Kwanza vya Dunia vilivyojiri kati ya mwaka 1914 hadi 1918, na kwa msingi wa siasa za kikoloni za Uingereza, Lawrence alifanya njama kubwa kuyachochea makabila ya Kiarabu kwa kisingizio cha kutaka kujitawala ili yajitenga na utawala wa Othmania ambao katika vita hivyo ulikuwa ukikabiliana na Uingereza. Thomas Edward Lawrence pia alikuwa na mchango mkubwa katika kuufikisha madarakani ukoo wa Aal-Saud nchini Saudi Arabia. Jasusi huyo wa Uingereza ambaye amekuwa mashuhuri kwa jina la Lawrence of Arabia, ameandika baadhi ya hatua zake katika nchi za Kiarabu katika vitabu vya Revolt in the Desert na Seven Pillars of Wisdom.

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita mfalme wa mwisho wa Iran, Shah Muhammad Reza Pahlavi na mkewe walikimbilia Italia. Kabla ya hatua hiyo, Reza Pahlavi alitia saini dikrii ya kumuuzulu Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iran, Muhammad Musaddeq. Kwa kuwa alielewa kwamba kutafanyika mapinduzi dhidi ya Musaddeq Shah aliamua kukimbilia kwa muda nchini Italia. Baada ya Musaddeq kutaifisha sekta ya mafuta ya Iran, suala hilo lilihatarisha maslahi ya wakoloni wa Kiingereza nchini na kuamua kufanya vitimbi na njama nyingi dhidi ya mwanasiasa huyo, na njama ya mwisho ya wakoloni hao ilikuwa mapinduzi yaliyofanywa kwa ushirikiano wa Marekani na Uingereza dhidi ya serikali ya Musaddeq tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria Shamsia. Siku tatu baada ya mapinduzi hayo yaliyoindoa madarakani serikali ya Musaddeq, Shah kibaraka Muhammad Reza Pahlavi alirejea nchini. Hata hivyo mtawala huyo kibaraka tarehe 26 Dei mwaka 1356 Hijria Shamsia aliikimbia daima Iran baada ya Mapinduzi ya Kiislamu yalioongozwa na hayati Imam Ruhullah Kohomeini.

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, kisiwa cha Cyprus kilipata uhuru baada ya machafuko ya miaka kadhaa. Kisiwa hicho ambacho hii leo kinaendeshwa chini ya mfumo wa jamhuri, kiko katika bahari ya Mediterraneanna kusini mwa Uturuki kikiwa na ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 9000. Kwa miaka kadhaa kisiwa cha Cyprus chenye historia kongwe na muhimu katika eneo kilikuwa chini ya falme za Iran, Ugiriki, Misri na utawala wa Othmania. Lakini mwaka 1878, utawala wa Othmania ulikabidhi usimamizi wa kisiwa hicho kwa Uingereza katika mkutano uliofanyika mjini Berlin Ujerumani na mwaka 1925 kisiwa cha Cyprus kikawa rasmi koloni la Uingereza.

Tarehe 25 Mordad 1372 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 16 Agosti mwaka 1993 alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzavari mwanachuoni mashuhuri wa nchini Iran. Ayatullah Sabzavari alizaliwa mnamo mwaka 1290 Hijiria Shamsia, sawa na mwaka 1911 katika mji wa Sabzavar ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanachuoni huyo alipatia elimu ya msingi katika mji wa Sabzawar na baadaye elimu ya dini katika mjini Mash’had. Baadaye Alielekea Najaf nchin Iraq na kupatia elimu ya juu ya maarifa ya Kiislamu. Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzavari ameandika vitabu vingi, maarufu zaidi ikiwa ni tafsiri ya Qur'ani ya ‘Mawaahibur-Rahman fii Tafsiril-Qur’an’ chenye juzuu 20, ‘Muhadh-Dhibul-Ahkaam fii Bayaanil-Halali wal-Haraam’ chenye juzuu 30 na ‘Tahdhibul-Usul’ chenye juzuu mbili.
