Sep 07, 2017 04:19 UTC
  • Alkhamisi tarehe 7 Septemba, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 16 Dhulhija 1438 Hijria sawa na 7 Septemba, 2017

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita alifariki dunia dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji.

Jenerali Mobutu Sese Seko

Tarehe 16 Shahrivar miaka 33 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani, mmoja wa maulamaa wakubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 1284 Hijria Shamsiya mjini Tehran. Ayatullah Ashtiyani alielekea katika chuo cha kidini cha Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali. Ayatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani alirudi Tehran na kuanza kutoa elimu kwa wanafunzi wa masuala ya dini baada ya kupata daraja ya ijtihadi. Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi vya thamani kama "Uongozi kwa Mtazamo wa Uislamu" na kile cha "Umiliki katika Uislamu". 

Ayatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani

Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita harakati ya kihistoria ya Wanamasumbwi nchini Uchina ilikandamizwa na kuzimwa. Wanamasumbwi lilikuwa jina walilopewa wanajeshi wa China waliosimama kupambana na ubeberu wa nchi za kigeni hususan za Magharibi ulioambatana na harakati za wamishonari wa Kikristo ndani ya China. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na wanamasumbwi hao ni kuteka balozi za nchi za Magharibi katika mji wa Beijing na kupambana vikali na shughuli za wahubiri wa Kikristo kutoka Ulaya. Harakati ya Wanamasumbwi wa Kichina ilikandamizwa na majeshi ya Ulaya, Marekani na Japan na serikali ya China ikalazimika kulipa gharama kubwa kwa nchi hizo.

Askari wa nchi 8 walishiriki kukandamiza harakati ya Wanamasumbwi nchini Uchina

Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita, nchi ya Brazil ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Ureno ilianza kuikoloni Brazil mwaka 1494, na mbali na kuwatumikisha watu wa jamii ya Wahindi Wekundu wa nchi hiyo, ilichukua mamilioni ya Waafrika kwa ajili ya kuwatumikisha kama watumwa katika shughuli za kilimo.

Bendera ya Brazil

Na miaka 967 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abu Abdullah Muhammad bin Jiyani, mnajimu na mwanahisabati wa Kiislamu huko Andalusia. Alizaliwa mwaka 379 Hijiria huko Cordoba moja ya miji ya kale ya Uhispania na alisoma hadi kuhitimu katika mji huo huo. Baada ya hapo alikwenda katika mji mkuu wa Misri, Cairo na kuishi huko kwa miaka minne. Jiyani alikuwa mahiri mkubwa katika elimu ya nujumu na miongoni mwa athari za mwanahisabati huyo ni kitabu chake cha nujumu ambacho kimetajwa katika makala ya 5 ya kitabu cha elementi cha baba wa jiometri, Euclid wa Ugiriki ya kale.