Oct 10, 2017 18:47 UTC
  • Jumanne 10 Oktoba, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 19 Mfunguo Nne Muharram 1439 Hijria sawa na Oktoba 10, 2017.

Tarehe 19 Muharram mwaka 61 Hijria msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na familia ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein (as) na mashahidi wengine waliouawa na utawala wa Yazid bin Muawiya katika medani ya Karbala uliondoka Kufa nchini Iraq ukielekea Damascus, makao makuu ya serikali ya bani Umayyah. Msafara huo hususan Imam Zainul Abidin na Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib (as) ulifichua na kuanika maovu ya Yazid bin Muawiyyah na kuwafanya watu wa Kufa wajute sana kwa kumuacha peke yake mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein katika mapambano ya Karbala. Watu wa mji wa Kufa walisikitika sana kutokana na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume na wasiwasi ulizuka juu ya uwezekano wa kuanza harakati ya wananchi dhidi ya utawala wa Yazid mjini humo. Kwa msingi huo mtawala wa Kufa, Ubaidullah bin Ziyad, alikhitari kutuma wajukuu hao wa Mtume wetu Muhammad (saw) huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyyah wakitanguliwa na kichwa kilichotenganishwa na mwili cha Bwana wa Vijana wa Peponi, Imam Hussein (as).

Miaka 286 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa huko katika mji wa Nice Ufaransa,  Henry Cavendish mwanafalsafa na tabibu wa Kiingereza. Cavendish alikuwa mwalimu wa masomo ya fikizikia na kemia. Henry Cavendish alikuwa mtu wa kwanza aliyethibitisha kuwa gesi ya hyadrogen ni nyepesi zaidi kuliko hewa ya kawaida. Cavendish aliaga dunia mwaka 1810. 

Henry Cavendish

Tarehe 10 Oktoba miaka 136 iliyopita, kuliundwa muungano wa mihimili mitatu kati ya Austria, Ujerumani na Italia. Kabla ya Italia kujiunga na muungano huo, awali kulikuwa na muungano wa mihimili miwili kati ya Austria na Ujerumani. Moja ya vipengee vya muungano huo kilikuwa na kusaidiana nchi wanachama pindi mmoja wao atakaposhambuliwa. Muungano huo ulikuwa ukiongezewa muda kila baada ya miaka mitano.

Miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo, mfumo wa Jamhuri nchini China ulichukua hatamu baada ya kuangushwa mfumo wa Kifalme. Katika kipindi cha kati ya mwaka 1907 na 1911 kulitokea uasi mara tano nchini China dhidi ya familia ya Kifalme ya Manchu. Uasi wote huo chimbuko lake kwa namna moja au nyingine lilikuwa ni fikra za kimapinduzi za Sun Yat-Sen mwanamapambano mashuhuri wa China. Hata hivyo uasi wa tano ambao ulianza tarehe 9 Oktoba mwaka 1911 ulipelekea kutokea ukandamizaji mkubwa, kutiwa mbaroni watu na mamia ya wengine kunyongwa hali ambayo ililipua ghadhabu na hasira za watu.

Kongresi ya Taifa ya Watu wa China

Na miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Fiji ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na siku kama hii husherehekewa nchini humo ikijulikana kama siku ya taifa. Fiji ilikuwa koloni rasmi la Uingereza tangu mwaka 1874 na Uingereza iliendelea kuukoloni muungano wa visiwa vya Fiji na ukoloni huo uliendelea kwa zaidi ya miaka 90. Mwaka 1965 katiba mpya ilianza kutekelezwa huko Fiji ambapo sheria zilibuniwa kwa ajili ya kupigania mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.

Bendera ya Fiji

 

Tags