Mar 18, 2018 10:11 UTC
  •  Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (23)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 23.

Kwa wafuatiliaji wa kawaida wa kipindi hiki bila shaka mtakuwa mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulianza kuzungumzia fikra na mitazamo ya Imam Khomeini (MA), akiwa ni mrekebishaji umma mkubwa wa Kishia katika Ulimwengu wa Kiislamu na ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tukasema kuwa Imam Khomeini (MA), kama alivyokuwa Sayyid Jamaluddin Asad Aabad amelishughulikia suala la umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa uzito mkubwa kwa upande wa fikra na nadharia na vilevile katika uga wa hatua za kivitendo. Isitoshe, Imam Khomeini (MA) alikuwa mmoja wa wanafikra wachache, ambao walilipa umuhimu maalumu suala la kuunda utawala kwa ajili ya kufanikisha dhana ya umoja wa Kiislamu; na kwa mafanikio aliyopata katika kuunda utawala, alianzisha wimbi kubwa la vuguvugu katika Ulimwengu wa Kiislamu. Tuliashiria pia kwamba imani ya dhati aliyokuwa nayo Imam Khomeini kwa kadhia ya “umoja” sio tu ilimbadilisha kuwa shakhsia mtajika zaidi wa kimapinduzi wa Ulimwengu wa Kiislamu, lakini pia ilimfanya awe na nafasi maalumu na ya juu mbele ya harakati na madhehebu tofauti za Kiislamu.

 

Katika fikra na mitazamo yake, Imam Khomeini aliitakidi kuwa Marekani na utawala haramu wa Israel zina nafasi kubwa sana katika kuzusha mifarakano na migawanyiko baina ya Waislamu na akawataka Waislamu wote waungane pamoja kukabiliana na maadui hao hasahasa Israel. Mrekebishaji umma huyo alikuwa akiitakidi kwamba kuwepo adui wa pamoja wa Waislamu wote yaani Israel ni chachu ya kuleta umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu; na kutokana na ukweli kwamba kuwepo adui kama huyo hakutoruhusu kupatikana umoja kati ya nchi za Kiislamu, aliielezea hali hiyo kama kitendawili au fumbo kwa kusema: “Kuna jambo ni kitendawili kwangu mimi; nalo ni kwamba nchi zote za Kiislamu na mataifa yote ya Waislamu yanajua ni nini kinachotutaabisha. Wanajua kama kuna mikono ya maajinabi hapa inayowafarakanisha; wanajiona wenyewe jinsi mifarakano hii inavyowadhoofisha na kuwahilikisha; wanajionea wenyewe jinsi utawala mmoja bandia wa Israel ulivyosimama kukabiliana na Waislamu; lakini pamoja na yote hayo wako duni na dhaifu katika kukabiliana nao. Kitendawili kilichopo ni kwamba kama wanayajua hayo, kwa nini basi hawaielekei tiba iliyo mjarabu kwao ya umoja na maafikiano” (Loho ya Nuru, Juzuu ya 9, Ukurasa wa 274-275).

Kwa kuzingatia upembuzi na uchambuzi huo, Imam Khomeini anatoa wito wa umoja kwa viongozi wa nchi za Kiislamu na kuwataka wawe na maelewano kwa ajili ya umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu, licha ya kila mmoja kuchunga mipaka yake: Analizungumzia suala hilo kwa kusema:

“Wajibu wa viongozi wa Uislamu, wafalme wa mataifa ya Waislamu na marais wa nchi za Kiislamu hivi sasa ni kuweka kando hitilafu na tofauti zao ndogondogo na za kupita; waweke pembeni tofauti hizo… wao wanapaswa kufuata Uislamu…wajibu wa viongozi ni kukaa pamoja wakafahamiana, wakachunga na kulinda mipaka yao. Kila mmoja na alinde mipaka yake, lakini kutokana na kuwepo adui yule wa nje anayekusababishieni madhara kiasi hiki, tumieni kalima ya umoja kukabiliana naye.” (Loho ya Nuru, Juzuu ya 2, Ukurasa wa 32-35).

 

Ili kuing’oa na kuitokomeza mizizi ya hitilafu na mifarakano baina ya Waislamu na kuweza kulifikia lengo la umoja wa kisiasa wa Ulimwengu wa Kiislamu, Imam Khomeini ametoa ramani iliyokamilika ambayo ndani yake mna dira na miongozo mwafaka kwa ajili ya kufikia umoja, ikiwemo kutoa changamoto ya harakati kwa wenye vipawa vya kisiasa na kidini ambao ndio watekelezaji wa mchakato wa umoja, kutumia nyenzo zinazohitajika ili kuweza kupiga hatua kuelekea kwenye umoja wa kisiasa wa Waislamu na hatimaye kuweza kuunda dola kubwa la Kiislamu. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, umoja ni jambo la stratijia na mkakati; na kwa mintarafu hiyo anabainisha mikakati ya kivitendo ya marhala na awamu mbili kwa ajili ya kufikia umoja. Wa kwanza ni “mkakati wa kiutamaduni na kiitikadi”; na mkakati wa pili ni wa “kisiasa na kiutekelezaji”. Kutokana na kuwa na uelewa wa uhalisia wa mambo na wa pande zote wa matatizo ya kifikra na kiakhlaqi ya jamii za Kiislamu na serikali za mataifa ya Waislamu, ili kuweza kufikia umoja wa umma wa Kiislamu na kuwa na umma mmoja mkubwa wa Waislamu, Imam Khomeini anapendekeza kabla ya jambo lolote, ifanyike kwanza kazi ya kurekebisha imani na itikadi za kidini na kisiasa za Waislamu na jamii zao, kwa kushikamana na kamba na mhimili wa Uislamu halisi. Kuhusiana na suala hilo, Imam Khomeini anabainisha aina mbili za Uislamu, ambazo ni Uislamu halisi wa Kimuhammad, na Uislamu wa Kimarekani; na kwa mtazamo wake, aina na tafsiri ya pili ya Uislamu ni Uislamu usiokubalika na ni kikwazo cha kufikiwa umoja wa Kiislamu. Huo ni Uislamu ambao Imam Khomeini alipambana nao na kukabiliana nao vikali.

Mlinganiaji huyo wa umoja na mrekebishaji wa umma alikuwa akitahadhrisha kuwa mtazamo wa viongozi wa jamii za Kiislamu si wa Kiislamu; na kimsingi fikra za Uislamu wa Kimarekani ni kizuizi kikuu kwa umoja wa umma wa Kiislamu. Imam Khomeini alikuwa akisisitiza kwamba ili kuandaa mazingira mwafaka na kufikia kwenye umoja halisi kuna haja ya kutekeleza mkakati sahihi wa kuondoa kizuizi hicho. Katika fikra na nadharia yake ya umoja, Imam Khomeini anavitaja vizuizi hivyo kimoja kimoja na kubainisha njia mwafaka ya kuviondoa. Kutangaza “Wiki ya Umoja” na “Siku ya Kimataifa ya Quds”ni miongoni mwa njia zilizopendekezwa na mrekebishaji huyo wa umma wa zama hizi.

 

Kwa mujibu wa fikra za Imam Khomeini, bila ya kuwa na ratiba na mipango maalumu ya kifikra yenye msingi wenye chimbuko na mashiko, haitowezekana kuleta mageuzi na mabadiliko ya kimsingi katika jamii za Kiislamu na kuweza kuwakomboa Waislamu na hali ya utengano na mifarakano. Sababu ni kwamba, hali mbaya na isiyoridhisha ya Ulimwengu wa Kiislamu ni matokeo ya hali, mazingira na visababishi vingi ikiwemo upotokaji wa kifikra, kiutamaduni na kiitikadi walionao Waislamu wenyewe na ubeberu wa madola ya kikoloni dhidi yao; wakoloni ambao daima wamekuwa wakichukua hatua zenye lengo la kuufuta utambulisho wa kifikra na kiutamaduni wa jamii za mataifa ya Kiislamu na kupora maliasili zao.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya sehemu ya 23 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu umefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumia kuwa mumefaidika na kunufaika na yale mliyoysikia katika kipindi chetu cha leo. Basi hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 24 ya mfululizo huu nakuageni huku kukutakieni heri na fanaka maishani.

Tags