Mar 18, 2018 10:17 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (24)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 24.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki bila ya shaka mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tuliendelea kuzungumzia fikra na mitazamo ya Imam Khomeini kuhusu suala la umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu. Tulieleza kuwa kwa mtazamo wa mrekebishaji huyo wa umma katika zama hizi, bila ya kuwa na ratiba na mipango maalumu ya kifikra yenye msingi wenye chimbuko na mashiko, haitowezekana kuleta mageuzi na mabadiliko ya kimsingi katika jamii za Kiislamu na kuweza kuwakomboa Waislamu na hali ya utengano na mifarakano. Sababu ni kwamba, hali mbaya na isiyoridhisha ya Ulimwengu wa Kiislamu ni matokeo ya hali, mazingira na visababishi vingi ikiwemo upotokaji wa kifikra, kiutamaduni na kiitikadi walionao Waislamu wenyewe na ubeberu wa madola ya kikoloni dhidi yao; wakoloni ambao daima wamekuwa wakichukua hatua zenye lengo la kuufuta utambulisho wa kifikra na kiutamaduni wa jamii za mataifa ya Kiislamu na kupora maliasili zao.

Kwa hivyo ili kuondokana na hali hiyo na kufikia kwenye hali inayotakiwa na inayotamaniwa, njia pekee ni kung’oa na kutokomeza misingi ya upotokaji wa kifikra, kiutamaduni na kiitikadi iliyokita ndani ya jamii za Waislamu. Na ili kuweza kufanya hivyo, kuna ulazima na udharura mkubwa zaidi hivi sasa wa kutumiwa nyenzo na suhula zote zilizopo kwenye nchi na mataifa ya Kiislamu kwa kufuata stratijia maalumu na jumuishi. Kwa hivyo Ulimwengu wa Kiislamu ambao ni majimui moja yenye mfungamano wa pamoja wa kihistoria, kiutamaduni na kisiasa unapaswa kulifanya suala la kurejea kwenye historia na utamaduni wake wa asili kuwa ndiyo dira ya kufuata katika harakati yake sambamba na kuyaelewa vizuri na kuyatumia mambo yanayojenga utambulisho wake wa kidini na kitaifa.

Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, wenye vipawa wa jamii ya Kiislamu, yaani maulamaa wa dini na wanafikra wataalamishaji wa kidini ndio wanaopaswa kuwa manahodha wa kuongoza jahazi la harakati ya kifikra na kiutamaduni ambayo hatimaye itawezesha jamii ya Waislamu kuwa na imani na itikadi za pamoja.

Kongamano la Wiki ya Umoja Tehran

 

Imam Khomeini alikuwa anaitakidi kuwa utengano na mfarakano unaoshuhudiwa katika Ulimwengu wa Kiislamu unatokana na serikali na wananchi wa mataifa ya Waislamu kujitenga na kujiweka mbali na mafundisho ya wahyi na yenye kuhuisha nyoyo ya Uislamu na badala yake Waislamu kuyategemea madola ya Kiistikbari ya Mashariki na Magharibi; na kwa mtazamo wa mrekebishaji huyo wa umma, njia pekee ya kujivua na kuondokana na matatizo ni kuzielewa tena kisawasawa nukta tatu kuu za msingi ambazo ni “Uislamu”, “Uhuru” na “Kujitawala”, kwa sababu anavyoamini yeye, kuielewa barabara misamiati hiyo mitatu mikuu ndiko kunakowezesha kuujenga tena upya utambulisho wao uliosahauliwa wa Kiislamu. Kwa sababu hiyo Imam Khomeini alitoa wito kwa vyuo vya kidini hususan maulamaa na wenye vipawa wa kidini wa kuwataka wafanya juhudi na idili ya kufufua mafundisho wa kidini hususan misamiati hiyo mitatu tuliyoiashiria. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, kuufuata na kuutekeleza Uislamu kumefungamana na uundaji utawala wa Kiislamu; na njia pekee ya kutibu machungu na masaibu yaliyozitanza jamii za Kiislamu ni kuufufua “Uislamu halisi wa Kimuhammad”. Uislamu halisi na wa asili ni chachu ya kuleta umoja baina ya Waislamu bila kujali madhehebu, asili, lugha na kaumu zao. Katika fikra za Imam Khomeini (MA), Uislamu halisi ni mjumuiko wa kifikra na kivitendo uliokamilika wenye ukwasi na utoshelezi mutlaki ambao una mipango na ratiba makini na za pande zote kuhusiana na maisha ya mwanadamu. Katika tafsiri ya Imam Khomeini ya Uislamu halisi wa asili, kutokana na ukamilifu wake, mvuto ulionao, sura yake ya umajimui kwa ajili ya ulimwengu mzima, na kukita kwake kwa kina kwenye imani na itikadi za watu wa mataifa ya Kiislamu, Uislamu huo una uwezo, vipawa na nguvu za kutosha za kuuhuisha umoja wa Kiislamu; na endapo Uislamu huo utatangazwa vizuri, unao uwezo wa kuirejesha tena heshima na adhama ya Ulimwengu wa Kiislamu kwa Waislamu wenyewe.

Rais Rouhani akihutubia wajumbe wa kongamano la Umoja wa Kiislamu

 

Uhuru ni maudhui nyingine ya msingi katika majimui ya mfumo wa kifikra wa Imam Khomeini katika kigezo cha kifikra na kiutekelezaji cha kufanikisha kuthibiti kwa umoja wa Kiislamu, kwa sababu nchi za Kiislamu ndizo zinazounda nguzo kuu za Ulimwengu wa Kiislamu au "Dola Kubwa la Kiislamu" na ndizo zenye nafasi kuu katika kupanga na kufanikisha malengo na mipango ya harakati hiyo. Katika kuzijenga tena nguzo hizo za "Dola Kubwa la Kiislamu" na kuhuisha umoja na adhama waliyokuwa nayo huko nyuma Waislamu katika historia yao, kuundwa na kuwepo serikali zinazotokana na wananchi wa mataifa yenyewe ya Waislamu, zisizo za kitaghuti, kiimla na kidikteta ambazo ni dhihirisho la kubeba ujumbe wa uhuru kuna nafasi muhimu sana. Na kinyume chake kuwepo serikali na tawala za kiimla na kidikteta katika nchi za Kiislamu, ni kizuizi kikuu cha kuwepo harakati ya pamoja yenye muelekeo wa umoja kwa ajili ya maslaha ya Ulimwengu wa Kiislamu. Kutokana na hayo kujikomboa na tawala zisizojali maslahi ya watu ni moja ya misingi mikuu ya fikra za kisiasa za Imam Khomeini katika nadharia yake ya umoja. Kuhusiana na ulazima wa kuzing’oa tawala za kitaghuti kwa madhumuni ya kuandaa mazingira ya kuasisiwa utawala wa Kiislamu, Imam Khomeini anasema: “Ni jukumu letu sote kumtokomeza taghuti, yaani tawala zisizofaa zilizoko katika ardhi zote za mataifa ya Kiislamu. Vyombo vya tawala za kijabari na zisizojali wananchi inapasa viondolewe, kisha nafasi yake ichukuliwe na asasi za umma zitakazoendeshwa kulingana na sheria za Kiislamu; kisha kuasisiwa hatua kwa hatua utawala wa Kiislamu. (Katika kuitafuta njia kwenye maneno ya Imam, Daftari la kwanza, Uk. 186).

“Kujitawala” ni maudhui kuu ya tatu katika mfumo wa kifikra wa Imam Khomeini kwa ajili ya kufikia kwenye umoja wa Kiislamu. Kujitawala ni kuwa na hali ya uelewa, mwamko, kujitambua na kujikomboa mataifa ya Kiislamu na ubeberu wa madola ya Magharibi na Mashariki. Imam Khomeini anasisitiza kuwa Mwenyezi Mungu hajamkweza kafiri yeyote na kumfanya awanyongeshe Waislamu na kuwatawalia mambo yao; na haifai Waislamu kukubali unyongeshwaji huo. Kwa mujibu wa mwanafikra, mrekebishaji wa umma na mtetezi huyo wa umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu, kuna ulazima wa kuwa na hali ya kujitawala na kujitegemea katika uga wa ndani na pia uga wa nje. Imam Khomeini alikuwa akiamini kuwa kujitawala na kujitegemea ndani ya nchi ndilo sharti la kuweza kuwa na misimamo huru ya kujitawala na kujiamulia mambo katika uga wa nje; kwa sababu bila kujitawala na kuwa huru ndani haiwezekani kuwa huru na kujitegemea katika uga wa kimataifa. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, katika hatua ya kwanza kuelekea kwenye hali halisi ya kujitawala, mataifa ya Waislamu yanapaswa kupiga hatua ya kurejea kwenye asili yao kwa kushikamana na thamani zao za Kiislamu na za kitaifa; kisha hatua ya pili ni kuutokomeza ukoloni katika ardhi za Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 24 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 25 ya mfululizo huu. Nakuageni na kukutakieni kila la heri maishani.

Tags