Mar 18, 2018 10:22 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (25)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 25.

Kwa wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki bila ya shaka mtakuwa mngali mnakumbuka kwamba kuanzia sehemu ya 22 ya mfulululizo huu tumekuwa tukizungumzia fikra na mitazamo ya Imam Khomeini (MA) kuhusu suala la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Tumeeleza kwamba akiwa mrekebishaji umma mkubwa wa Kishia katika Ulimwengu wa Kiislamu na vilevile Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (MA), kama alivyokuwa Sayyid Jamaluddin Asad Abadi alilishughulikia suala la umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa uzito mkubwa kwa upande wa fikra na nadharia na vilevile katika uga wa hatua za kivitendo. Isitoshe, Imam Khomeini (MA) alikuwa mmoja wa wanafikra wachache, ambao walilipa umuhimu maalumu suala la kuunda utawala kwa ajili ya kufanikisha dhana ya umoja wa Kiislamu; na kwa mafanikio aliyopata katika kuunda utawala, alianzisha wimbi kubwa la vuguvugu katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika kubainisha chanzo cha kutokuwepo msimamo na muelekeo mmoja katika Ulimwengu wa Kiislamu, Imam Khomeini ametaja sababu mbili muhimu na za msingi; mojawapo ikiwa ni: Kuwepo mpasuko baina ya watu na utawala na hitilafu kati ya watawala wa nchi za Kiislamu. Nukta nyengine ya msingi katika fikra na mitazamo ya mrekebishaji huyo wa umma na mlinganiaji wa umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu ni kwamba, Marekani na utawala haramu wa Israel zina nafasi kubwa sana katika kuzusha mifarakano na migawanyiko baina ya Waislamu na akawataka Waislamu wote waungane pamoja kukabiliana na maadui hao hasahasa Israel. Lakini mbali na maadui hao wa nje, Imam Khomeini alikuwa akiitakidi kuwa utengano na mfarakano unaoshuhudiwa katika Ulimwengu wa Kiislamu unatokana na serikali na wananchi wa mataifa ya Waislamu kujitenga na kujiweka mbali na mafundisho ya wahyi na yenye kuhuisha nyoyo ya Uislamu na badala yake Waislamu kuyategemea madola ya Kiistikbari ya Mashariki na Magharibi; na kwa mtazamo wa mrekebishaji huyo wa umma, njia pekee ya kujivua na kuondokana na matatizo ni kuzielewa tena kisawasawa nukta tatu kuu za msingi ambazo ni “Uislamu”, “Uhuru” na “Kujitawala”, kwa sababu anavyoamini yeye, kuielewa barabara misamiati hiyo mitatu mikuu ndiko kunakowawezesha Waislamu kuujenga tena upya utambulisho wao wa Kiislamu uliosahauliwa.

Imam Khomeini MA alikuwa mstari wa mbele kupigania umoja kati ya Waislamu

 

Imam Khomeini anaitakidi kuwa utegemezi mkubwa zaidi wa mataifa manyonge kwa madola yenye nguvu na ya kiistikbari ni utegemezi wa kifikra na wa ndani ya nafsi za watu ambao ndio chimbuko la aina nyengine za utegemezi. Na maadamu taifa halijawa huru na lenye kujitegemea kifikra, halitoweza kujitegemea katika nyuga nyinginezo.

Kwa mtazamo wa mrekebishaji huyo wa umma kupanuliwa na kuimarishwa misingi ya tablighi na maulamaa, wanafikra wataalamishaji na waongozaji watu kifikra wa kidini na kitaifa ni moja ya njia za kivitendo za kuwezesha kufikiwa umoja baina ya Waislamu. Imam Khomeini alikuwa akiamini kwamba wenye vipawa wanapaswa kutumia suhula na rasilimali zote zilizopo kwa ajili ya kuinua upeo wa kifikra wa watu na kupanua na kuimarisha mahusiano ya kijamii ndani ya umma wa Kiislamu. Kwa kutoa mfano, kuzitumia ipasavyo ibada za kiimanawi na kisiasa za Sala ya Ijumaa katika upeo wa kitaifa, na Hija katika upeo wa kimataifa, ni mambo aliyokuwa akiyatilia mkazo sana Imam Khomeini (MA). Mrekebishaji huyo wa umma na mlingania umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu alikuwa na uelewa kamili wa taathira kubwa ya nafasi ya kijamii ya dini katika ujengaji wa fikra na ujengaji wa jamii. Imam Khomeini hakuwa akiipa uzito mijumuiko na hadhara za kidini kwa sababu tu ya kutumiwa kwake kimafunzo katika maudhui za kifikra, lakini muhimu zaidi ya hilo ni nafasi na mchango wa mikusanyiko hiyo katika kujenga jamii za Kiislamu na kuasisi mahusiano mapya ya kijamii kupitia mikusanyiko mbalimbali sambamba na Waislamu kupata uelewa wa nguvu na uwezo wao wa kiirada na wa rasilimaliwatu walionao. Kwa mintarafu hiyo, kuanzishwa Wiki ya Umoja na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds kama nembo mbili za umoja kwa Ulimwengu wa Kiislamu na ambazo zinabeba pia ujumbe wa kimapinduzi na wa kupinga ukoloni, ni hatua zilizopendekezwa na Imam Khoemini au kuungwa mkono na mrekebishaji huyo wa umma.

 

Kuanzisha harakati moja na katika upeo wa ulimwengu mzima itakayojumuisha mataifa ya Waislamu duniani na nchi za Kiislamu ni miongoni mwa stratijia zilizokuwa zikitumiwa na Imam Khomeini kwa ajili ya kuleta umoja baina ya Waislamu. Hizbullah na Hizbul-Mustadh'afiin zilikuwa istilahi mbili kuu katika misamiati ya kisiasa ya fikra za Imam Khomeini kwa ajili ya kufikia kwenye umoja wa Kiislamu. Mrekebishaji huyo wa umma alikuwa akiamini kuwa kuundwa harakati moja ya Uislamu ni dhihirisho la nguvu na uwezo ulioratibiwa wa umma wa ulimwengu wa leo wa Waislamu uliokumbwa na dhoruba za migogoro. Ni kwa sababu hiyo, Imam Khomeini aliitaja "Hizbul-Mustadh'afin” kuwa ni harakati na muundo wa kisiasa ambao si Waislamu peke yao, lakini wanaonyongeshwa wote duniani wataweza kuunganisha harakati zao za kisiasa zenye malengo maalumu pamoja na harakati hiyo kuu na kuimarisha zaidi mshikamano na muelekeo wa pamoja ulioko baina yao. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, lengo la kuunda chama na harakati kama hiyo ni kuziimarisha imani za pamoja katika upeo wa umma wa Kiislamu na baadaye kuchunguza na kupata njia ya ufumbuzi ya kuhitimisha matataizo na masaibu yaliyoutanza Ulimwengu wa Kiislamu. Kuhusiana na nukta hiyo, Imam Khomeini anasema: “Mimi ninatumai kwamba kitapatikana chama kimoja cha ulimwengu mzima kitakachoitwa Chama cha Wanyonge, ambapo wale wote walionyongeshwa watajiunga na chama hicho na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wanyonge, kusimama na kukabiliana na waistikbari na waporaji wa Mashariki na Magharibi na kutoruhusu waistikbari wawadhulumu wanyonge wa ulimwengu”. (Loho ya Nuru, Juzuu ya 8, Ukurasa 250).

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 25 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Ni matumaini yangu kuwa mumenufaika na kuelimika na yale mliyoyasikia katika kipindi hiki. Katika kipindi chetu cha juma lijalo, tutaanza kuzungumzia fikra na mitazamo ya Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na suala la umoja wa Kiislamu. Basi hadi wakati huo inshaallah, nakuageni na kukutakieni kila la heri maishani.

Tags