Mar 18, 2018 10:25 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (26)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 26.

Bila shaka wapenzi wasikilizaji mngali mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tuliahidi kwamba baada ya kuzungumzia fikra na mitazamo ya Imam Khomeini, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu suala la umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu, katika sehemu hii ya 26 tutaanza kuzungumzia fikra na mitazamo ya Kiongozi Mkuu wa sasa wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, juu ya suala hilo muhimu kwa Ulimwengu wa Kiislamu.

Ayatullah Khamenei analielezea suala la umoja wa Kiislamu kuwa ni hitajio la dharura zaidi kwa Waislamu katika dunia ya leo. Katika kubainisha maana ya umoja, Ayatullah Khamenei anaukataa mtazamo wa kimakanika unaoelezea umoja kwa maana ya kuweka kando tofauti zote za kifikra na za kihistoria zilizopo baina ya Waislamu na badala yake anatiliza mkazo umoja kwa maana ya Waislamu kuwa na muelekeo mmoja katika kukabiliana na maadui wa nje. Katika kuvunja hoja za watu wanaotaka kuzima mijadala ya kimadhehebu kwa kisingizio cha kulinda umoja, Ayatullah Khamenei anasema: Umoja baina ya Waislamu maana yake si wao kuweka pembeni itikadi zao juu ya masuala wanayohitilafiana; bali inavyotakiwa hasa ni kuwepo majadiliano ya kielimu baina ya maulamaa wa madhehebu za Kiislamu; lakini jambo ambalo halifai ni majadiliano hayo kuwa na sura ya uhasama na ugomvi; bali yawe muda wote yanafanyika na kubainishwa kwa sura ya ujengaji hoja; na mhimili mkuu wa mijadala ya aina hiyo unapasa uwe ni Quráni, Mtume wa Allah na akili ya burhani. Sababu yake ni kwamba Quráni tukufu imewalingania watu kutumia akili pia. Kwa hivyo haiwezekani kuyafuta majadiliano ya kimadhehebu kwa kisingizio cha umoja, wala kutumia kisingizio cha majadiliano hayo ili kuuvuruga umoja. Kwani kama kuwepo hitilafu tu ni sababu ya kufarakana, haingepasa pia kufunga ndoa na kuanzisha familia, seuze kuwa na jamii na jamii ya kidini. Kwa sababu hata watu wa nyumba moja na familia moja, nao pia wanatofautiana kifikra na kimawazo. Kwa hivyo umoja uliokusudiwa na viongozi wetu wakubwa wa dini ni umoja wa kukabiliana na makafiri na maadui wa Uislamu; si umoja katika itikadi na masuala ya ndani ya kimadhehebu.

 

Kwa mtazamo wa Ayatullah Khamenei, mfarakano ni sumu yenye kuhilikisha kwa Ulimwengu wa Kiislamu na anaamini kuwa mikono ya wakoloni wenye nia ya kupora maliasili na utajiri wa nchi za Kiislamu ndiyo inayosababisha mifarakano hiyo. Ayatullah Khamenei anaamini kuwa uadui wa maajinabi kwa Mashia na Masuni unafanyika kwa ajili ya kufikia lengo moja ambalo ni la kukabiliana na Uislamu wenyewe. Katika hotuba aliyotoa tarehe 8 Agosti 2006, Ayatullah Khamenei amesema: "Suala la Shia na Suni ni moja ya nyenzo muhimu zinazotumiwa na maadui kuusambaratisha umma wa Kiislamu. Masuni walijue hilo na Mashia pia walijue; Waislamu wote, ndani ya Iran na katika Ulimwengu wa Kiislamu, wajue kwamba hitilafu baina ya Shia na Suni ni moja ya nyenzo na fimbo inayotumiwa na adui dhidi ya umma wa Kiislamu. Wanautumia wenzo huu kwa kila namna wanayoweza. Siku Masuni wa Palestina wanapokuwa kwenye mbinyo, baadhi ya watu wanatumia shaár na propaganda kwamba: Hawa ni Suni, nyinyi ni Shia, ili kujaribu kuhakikisha hawasaidiwi. Leo hii ambapo Mashia wa Lebanon wako kwenye mashinikizo, wanawaambia baadhi ya watu: Nyinyi ni Suni, hawa ni Shia; msiwasaidie. Wao hawaheshimu Shia wala Suni; wao wanakabiliana na Uislamu wenyewe. Mfarakano ni sumu yenye kuuhilikisha Ulimwengu wa Kiislamu. Hii mifarakano inayatenganisha mataifa; inazitenganisha nyoyo".

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anaitakidi kuwa kuwepo hitilafu za mtazamo baina ya wafuasi wa fikra na itikadi mbili tofauti ni jambo la kawaida; na kuipeleka mijadala ya kihistoria na kimadhehebu kwenye ngazi za watu wa kawaida na kuzivaa maudhui hizo kihamasa na kijazba na kwa mtazamo usio wa kielimu ni moja ya nyenzo zinazotumiwa na maajinabi kwa lengo la kushadidisha hitilafu zilizopo baina ya Waislamu. Akiifafanua zaidi nukta hiyo, Ayatullah Khamenei anasema: "Kutokana na kuathiriwa na taasubi, hitilafu baina ya wafuasi wa itikadi mbili ni jambo ambalo lipo, na tena ni la kawaida; na wala halihusiani na Shia na Suni. Hitilafu zimekuwepo baina ya madhehebu zenyewe za Shia; na baina ya madhehebu zenyewe za Suni; hitilafu hizi zimekuwepo katika zama zote za historia. Mkiiangalia historia, mtaona kuwa kumekuwapo na hitilafu baina ya matapo ya kifiqhi na Usuli ya Ahlu Sunnah – kama Ash'ari na Mu'tazilah na pia baina ya Hanbali, Hanafi na Shafi'i – na vilevile baina ya matapo tofauti ya Shia. Hitilafu hizi zinapofikia kwenye ngazi ya chini – ya watu wa kawaida – zinafikia hata kwenye uchukuaji misimamo mikali na hatari ya watu kukabana koo.

 

Maulamaa huwa wanakaa kitako wakazungumza na kujadiliana; lakini inapofika zamu ya watu wasio na silaha ya elimu, wao hutumia silaha ya hamasa, ngumi na silaha za kimaada; na hili ni jambo hatari. Haya yamekuwepo duniani siku zote; na kila mara waumini na wenye kuutakia mema umma wamekuwa wakijitahidi kuzuia hali hiyo; maulamaa na shakhsia wateule, juhudi zao zote zimekuwa ni kuhakikisha katika ngazi za wasioyaangalia mambo hayo kielimu, haifikii hadi ya kuzuka ugomvi na utesi; lakini kuanzia kipindi fulani nyuma na kujia huku, kuna kitu kingine pia kimejiingiza kwenye kadhia hii nacho ni "Ukoloni". Hatutaki kusema kuwa hitilafu kati ya Shia na Suni kila mara zimesababishwa na Ukoloni; la hasha. Jazba zao wenyewe pia zimechangia; baadhi ya jazba hizo zimetokana na ujinga, baadhi yao zimetokana na taasubi, baadhi yao zimetokana na hamasa na baadhi yao zimetokana na ufahamu pogo; lakini wakati Ukoloni nao ulipojiingiza ukaitumia silaha hii kadiri ilivyowezekana kuitumia." (Hotuba ya tarehe 15 Januari, 2007).

Ayatullah Khamenei anaitakidi kuwa hatua za kutusiana na kuvunjiana heshima za baadhi ya makundi ya Kishia na Kisuni zinafanyika kufanikisha malengo ya maadui wa Uislamu; na anayakanya vikali makundi yote mawili kwa kuyataka yajiepushe na mambo hayo. Ayatullah Khamenei anasema: "Suni na Shia kila moja wana hafla zao za kimadhehebu, desturi zao, ada zao na majukumu yao ya kidini wanayotekeleza na inapasa wayatekeleze; lakini mstari mwekundu ni kwamba haifai abadani kusemwa kitu cha kusababisha wao kutengana kwa sababu ya hatua za kuyatusi matukufu ya upande mmojawapo, iwe inayochukuliwa na baadhi ya Mashia kwa sababu ya kujisahau, au inayochukuliwa pia na baadhi ya Masuni kama Masalafi na mfano wao kutokana na kujisahau. Hili ndilo jambo analotaka adui. Hapa pia inapasa kuwepo na umakini". (Hotuba aliyotoa mbele ya hadhara ya wananchi tarehe 19 Mei, 2009.

*********

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mtajiunga nami tena inshaaAllah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki. Basi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.

Tags