Mar 18, 2018 10:35 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (28)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 28.

Katika sehemu hii ya 28 ya mfululizo tunaendelea kuzungumzia fikra na mitazamo ya Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Mkuu wa sasa wa Mapinduzi ya Kiislamu juu ya suala la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Ayatullah Khamenei anaitakidi kuwa kutawasali na kushikamana na Ahlul-Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW ni moja ya hazina zenye thamani za dini ya Uislamu kwa ajili ya kupatikana umoja; na anaamini kwamba kuwapenda Ahlul Bayt na kujifunza mafundisho ya dini, ambayo ni mambo yanayokubaliwa na yanayoziunganisha madhehebu zote za Kiislamu yanaweza kuwa nukta za kutegemea na kuleta mshikamano baina ya Waislamu duniani. Analitolea ufafanuzi zaidi suala hilo kwa kusema: "Ulimwengu wa Kiislamu unaweza kuwa na mwafaka na umoja katika nukta mbili zinazowahusu Ahlul Bayt Alayhimu-Salam: moja ni katika kuwapenda, ambalo ni suala la kihisia na kiitikadi; na Waislamu wameamrishwa kuwapenda Ahlul Bayt (alayhimu-salam) na wote wamelikubali hilo. Hii inaweza kuwa nukta ya kuunganisha hisia na mapenzi ya Waislamu. Nukta ya pili ni mafunzo ya dini na kujifunza mafundisho na hukumu za dini kulingana na uadilifu wa Qur'ani na kwa mujibu wa Hadithi ya Thaqalaini. Hadithi hii yenyewe imepokelewa na Shia na Suni na madhehebu nyengine tofauti za Kiislamu. Hiki ni kitu muhimu. Kupeperusha bendera ya Ahlul Bayt (alayhimu-salam) katika Ulimwengu wa Kiislamu, kwa hakika kunaweza kuukusanya na kuuleta pamoja Ulimwengu wa Kiislamu na Waislamu kupitia nukta hizi mbili. Leo hii Waislamu wote wanayo fursa hii adhimu. (Hadithi ya Wilayat, juzuu ya 4, ukurasa wa 216).

Moja ya mapendekezo muhimu na ya kivitendo ya Ayatullah Khamenei kwa ajili ya kufanikisha lengo la umoja wa Kiislamu ni kuasisi Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu. Jumuiya hii ni mahala pa kukutanisha na kuunganisha fikra za viongozi wa madhehebu za Kiislamu kwa ajili ya kupunguza hitilafu na kuandaa mazingira ya kuwa na muelekeo zaidi wa pamoja. Kuhusiana na falsafa na hekima ya kuasisiwa jumuiya hiyo pamoja na malengo yake, Ayatullah Khamenei anasema: "Kuna watu bilioni moja duniani ambao wana itikadi moja kuhusu Mwenyezi Mungu, Mtume, Sala, Hija, Al Kaaba, Qur'ani na hukumu nyingi za dini na pia wanahitilafiana katika baadhi ya mambo. Hawa waamue kushikilia na kupigana vita kwa sababu ya hayo mambo machache wanayotafautiana ili yule mtu ambaye anampinga hata Mungu, Mtume SAW, dini na mambo yote aweze kufanya anayotaka? Je hilo linakubalika kiakili?! Sisi tumesema baadhi ya maulamaa na wanafikra wakutane pamoja na katika upeo wa kielimu na kiutamaduni, waanzishe "Jumuiya ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu" kwa ajili ya kukaribiana. Kuna madhehebu nne za kifiqhi katika Ahlu Sunnah, kuna madhehebu ya Imamiyyah, kuna madhehebu ya Zaydiyyah na kuna madhehebu nyengine za Kiislamu. Hao wote wakae waangalie wanaweza kufanya kazi na kushirikiana pamoja kwa kiwango gani katika masuala ya kielimu na kidini."

 

Ayatullah Khamenei anauelezea uundwaji wa jumuiya kama hiyo kuwa ni jambo la dharura kwa Ulimwengu wa Kiislamu na anaitaja diplomasia ya umoja wa Kiislamu kuwa ndio stratijia kuu inayotakiwa kutawala katika utendaji wake. Kuhusiana na matunda na mafanikio ya kuundwa taasisi kama hiyo, anasema: "Leo Ulimwengu wa Kiislamu unahitaji ukurubiano huu. Katika ukurubiano huu, madhehebu za Kiislamu zinapaswa kukaribiana kifikra na kiitikadi. Kwani si hasha mazungumzo na majadiliano yakawezesha kupatikana matokeo mazuri kuhusiana na baadhi ya dhana ambazo madhehebu zilikuwa zikidhaniana. Huenda baadhi ya suitafahamu zikaondoka, baadhi ya itikadi zikanyooshwa na baadhi ya fikra zikakaribiana kwa maana yake halisi. Bila shaka kama hili litakuwa, ni bora zaidi kuliko vingine vyovyote vile. Kwa akali ni kwamba mkazo utiliwe kwenye mambo ya pamoja. Hii itakuwa ndio faida ndogo kabisa ya mazungumzo na majadiliano haya. Kwa hivyo inapasa kujiepusha kuzungumzia masuala yanayoleta mfarakano. (Hadithi ya Wilayat, Juzuu ya 8, Ukurasa wa 79)

Huenda wasikilizaji wapenzi mkapitikiwa na suali hili, kwamba nini madhumuni ya Ayatullah Khamenei kuhusu kufuatiliwa diplomasia ya umoja wa Kiislamu katika Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu. Kuhusiana na hilo inapasa tueleze kwamba diplomasia ya umoja inazingatia manufaa na maslahi mapana zaidi kuliko maslahi ya kitaifa tu kwa kujumuisha pia manufaa na maslahi ya Uislamu na Ulimwengu wa Kiislamu. Umoja wa Kiislamu unazingatia yenye manufaa na maslaha kwa Ulimwengu mzima wa Kiislamu, si nchi moja pekee; japokuwa wakati zinapochukuliwa hatua za kudhamini maslahi ya Ulimwengu wa Kiislamu yanakidhiwa pia maslahi ya taifa ya nchi za Waislamu. Nukta muhimu ni kwamba maana ya manufaa na maslahi iliyomo kwenye tafsiri ya diplomasia ni manufaa na maslahi ya Kiislamu yanayodhamini pia manufaa ya taifa. Zinapozungumziwa nguvu pia, Umoja wa Kiislamu unajitokeza kama moja ya vitu vinavyounda mhimili wa nguvu za Ulimwengu wa Kiislamu. Kwa msingi huo diplomasia ya umoja inaweza kuelezewa maana yake kama: "fani na uhodari wa kutumia umoja wa Kiislamu kwa ajili ya kudhamini maslaha ya Uislamu na manufaa ya Ulimwengu wa Kiislamu na nchi za Kiislamu".

 

Moja ya mambo ya msingi ya kufanikisha diplomasia hii ni kuandaa mazingira ya kuunganisha pamoja maslahi na manufaa katika nchi zote za Kiislamu. Hii ikiwa na maana kwamba ikiwa sehemu moja ya jamii ya Kiislamu itakuwa na nguvu kielimu na kiuchumi na hata kijeshi, nguvu na uwezo huo unaweza kuenea kwenye sehemu nyengine za Ulimwengu wa Kiislamu. Kwa kutoa mfano, ikiwa nchi moja ya Kiislamu kama Iran, Pakistan, Indonesia au Misri itaweza kuwa na ustawi wa kisayansi au kiteknolojia katika uga fulani, ustawi huo uweze kufika kirahisi kwenye nchi nyengine za Kiislamu. Nukta nyengine ya umoja ni nchi za Kiislamu kumjua adui wao wa pamoja. Kwa mfano inapasa zijue kwamba uadui wa utawala wa Kizayuni wa Israel haukomei Palestina na nchi jirani na Palestina pekee bali utawala huo una uadui na ulimwengu mzima wa Kiislamu; na kuelewa maudhui hiyo kunaweza kuwa na taathira chanya kwa kuwafanya Waislamu wawe na muelekeo na mtazamo mmoja.

Nukta nyengine inayopasa kuzingatiwa katika kufahamu diplomasia ya Umoja wa Kiislamu ni nafasi na mchango wa wenye vipawa katika mchakato huo. Ili kufanikisha diplomasia hii inatakiwa kabla ya jambo lolote yafanyike kwanza "mazungumzo ya wenye vipawa" katika Ulimwengu wa Kiislamu. Ili yaweze kupatikana matilaba kuna ulazima kwa wenye vipawa wa Ulimwengu wa Kiislamu kujumuika pamoja na kuandaa hati ya mkakati wa umoja sambamba na kuifanyia uchambuzi na upembuzi hali iliyopo katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kwa utaratibu huo nafasi ya wenye vipawa katika vyuo vya kidini na vyuo vikuu katika kuratibu na kupitisha diplomasia ya umoja ndicho kitovu na mhimili mkuu; kwa sababu diplomasia inapata maana yake halisi kupitia mazungumzo. Kwa hivyo kama tunakubaliana kuwa moja ya nguzo muhimu za diplomasia ni mawasiliano, kuwepo mawasiliano baina ya wenye vipawa wa Ulimwengu wa Kiislamu ni moja ya masharti muhimu na ya lazima ya diplomasia ya umoja; kiasi cha kutufanya tuthubutu kusema kuwa bila ya mazungumzo ya wenye vipawa wa Ulimwengu wa Kiislamu, umoja wa Kiislamu utakuwa tasa na wenye kasoro.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umemalizika; hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo hadi tutakapokutana tena inshaaAllah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki.

Tags