Mar 18, 2018 10:39 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (29)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 29.

Katika vipindi vitatu vilivyopita tumezungumzia nafasi ya umoja wa Kiislamu katika fikra na mitazamo ya Ayatullah Khamenei pamoja na pendekezo lake la kivitendo la kufanikisha kufikiwa lengo la umoja wa Kiislamu, yaani kuundwa Jumuiya ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu. Katika kipindi chetu cha leo tumekusudia kuzungumzia chimbuko la kujengeka fikra ya kuasisi jumuiya ya kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu baina ya maulamaa wa Kishia na Kisuni na hasahasa fikra na mitazamo ya waasisi wake wawili yaani Sheikh Mahmoud Shalt'ut, Mufti Mkuu wa Misri na Sheikh wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar na Ayatullah Al-Udhma Burujerdi, mmoja wa Marjaa Taqlidi wakubwa zaidi katika Ulimwengu wa Kishia.

Kwa kuanzia inapasa tuseme kuwa istilahi ya kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu ilizungumziwa kwa mara ya kwanza karibu miaka sabini iliyopita na taasisi ya "Daru-Taqrib Bainal-Madhahibil-Islamiyyah" mjini Cairo Misri. Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1327 hijria shamsia na jopo la maulamaa wakubwa wa Kisuni na Kishia na kwa juhudi kubwa za marehemu Allamah Sheikh Muhammad Taqi Qummi, ambaye aliishi kwa miaka kadhaa katika nchi za Lebanon na Misri na ambaye ndiye aliyekuwa Katibu Mkuu wake wa kwanza. Katika zama hizo, taasisi ya "Daru-Taqrib Bainal-Madhahibil-Islamiyyah" ilikuwa na umuhimu mkubwa katika Ulimwengu wa Kiislamu. Wajumbe wa taasisi hiyo walijumuisha wahadhiri wakubwa wa Al-Azhar kama Sheikh Abdulmajid Salim, Sheikh Mahmoud Shalt'ut, Sheikh Abu Zuhra, Hassan Al-Banna na wengineo.

 

Alikuwemo pia alimu mmoja wa madhehebu ya Zaydiyyah kutoka Yemen. Na kwa upande wa maulamaa wa Kishia alikuwemo Sheikh Muhammad Hussein Kashif-Al Ghit'aa aliyekuweko mjini Najaf pamoja na Sayyid Sharafuddin na Sheikh Muhammad Jawaad Mughniya waliokuweko nchini Lebanon. Madhehebu zilizokusudiwa katika fikra ya ukurubishaji ni madhehebu za fiqhi ya Uislamu ambazo zinajumuisha madhehebu kuu nne za Ahlu-Sunnah; yaani Hanafi inayonasibishwa na Ima Abu Hanifa, madhehebu ya Maliki inayonasibishwa na Imam Malik Ibn Anas, madhehebu ya Shafi'i, inayonasibishwa na Imam Muhammad bin Idris Shafi na madhehebu ya Hanbali inayonasibishwa na Imam Ahmad bin Hanbal pamoja na madhehebu mbili za Shia Imamiyyah na Zaydiyyah. Madhehebu ya Ismailiyyah ilihesabiwa kama tawi la madhehebu ya Imamiyyah na madhehebu ya Ibadhi ilihesabiwa kama tawi la madhehebu za Ahlu Sunnah. Madhehebu hizo zote kila moja ina fiqhi inayojumuisha hukumu za kimatendo za Uislamu za milango ya fiqhi kuanzia masuala ya tohara mpaka kwenye hukumu za diya; na katika baadhi ya masuala zinahitilafiana kutokana na ijtihadi za mafuqahaa wao.

Baada ya Daru-taqrib kufanya uhakiki mpana ilifikia hitimisho kwamba hauwezi kupatikana mwafaka na kuzikurubisha pamoja madhehebu katika mijadala ya ilmul-kalam na ya kiitikadi likiwemo suala la Ukhalifa na Uimamu na huenda hata mijadala juu ya masuala hayo ikasababisha kuibuka upya hitilafu; kwa sababu hiyo iliamua kuelekeza juhudi zake katika kutatua hitilafu za kifiqhi, ambazo hatimaye zilizaa matunda kwa fatua iliyotolewa na Sheikh Mkuu wa Al-Azhar Mahmoud Shalt’ut. Katika fatua yake hiyo, Sheikh Shalt’ut alisema wafuasi wa madhehebu nne za Ahlu-Sunnah wanaweza kurejea katika masuala ya fiqhi kwenye madhehebu nyenginezo ikiwemo ya Imamiyyah Ithnaasharia; yaani kwa kufuata hukumu zilizotolewa na mafuqahaa wa madhehebu hizo. Na sababu ni kwamba mafuqahaa wote hao wametoa fatua zao kwa kutegemea Qur’ani na Sunnah. Miongoni mwa hatua muhimu zaidi zilizochukuliwa na Sheikh Shalt’ut wakati alipokuwa Mkuu wa Al-Azhar ni kutoa idhini ya kusomeshwa fiqhi ya madhehebu ya Shia sambamba na masomo ya fiqhi ya madhehebu za Ahlu Sunnah, hatua ambayo ilitoa mwanga mpya kwa wahadhiri na watafiti wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar. Kwa mujibu wa fiqhi ya utabikishaji, mtafiti na mhakiki hutalii na kusoma rai na mitazamo yote ya kifiqhi ya madhehebu za Kiislamu na kuamua kufuata na kutekeleza rai ya madhehebu ambayo hoja zake ni madhubuti zaidi. Sheikh Shalt’ut alikuwa akiukubali usuli na msingi mmoja mkuu katika kulinganisha hoja za maulamaa wa madhehebu tofauti; nao ni kwamba hoja yoyote ile iliyo madhubuti zaidi ndiyo inayokubalika; iwe ni katika madhehebu yake mwenyewe au madhehebu nyengine; na alikuwa akisisitiza kwamba mafuqahaa wa Kiislamu wanapaswa waweke kando taasubi na hawaa za nafsi na kuwa tayari kila mmoja kukubali rai na fikra ya mwenzake atakayoona ni athirifu zaidi katika kuifanya misingi ya Uislamu iwe imara zaidi na itakayoihakikishia familia na jamii ya Kiislamu kuwa na hali bora zaidi.

 

Ayatullah Al-Udhma Burujerdi, naye pia ni miongoni mwa Marjaa-Taqlidi watajika na mmoja wa maulamaa wakubwa ambaye alikuwa siku zote akilipa umuhimu suala la umoja wa Waislamu na kuzikurubisha pamoja madhehebu zao. Yeye alikuwa Marjaa na alimu wa juu kabisa wa Waislamu wa Kishia baada ya Marjaa mkubwa Ayatullah Esfahani aliyefariki dunia mwaka 1325 hijria shamsia. Ayatullah Al-Udhma Burujerdi alikuwa amebobea pia katika fani ya ilmur-rijaal na ya Hadithi za Shia na Suni. Katika zama zote mbili, za kabla na baada ya kuwa Marjaa-Taqlidi wa Ulimwengu wa Kishia, Ayatullah Burujerdi alikuwa akishughulikia masuala ya Waislamu kiujumla na akawa na hima kubwa ya kulifanyia kazi suala la umoja, kusafisha kutu za mifarakano mingi iliyokuwepo, kuzikurubisha pamoja madhehebu na kuwakusanya pamoja Waislamu chini ya bendera ya Uislamu ya Laa ilaha illa Allah, Muhammad Rasul Allah. Kushuhudia hali mbaya na isiyoridhisha waliyokuwa nayo Waislamu, kudhibitiwa nchi za Waislamu na kuwa chini ya mamlaka ya makafiri na kutawala hali ya uadui na ya kutazamana kwa jicho baya baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe, ni mambo yaliyokuwa yakimfanya Ayatullah Burujerdi awe na irada na azma thabiti zaidi juu ya suala la umoja na kuwaunganisha Waislamu. Uelewa mpana wa fikra mpya aliokuwa nao Marjaa Taqlidi huyo kuhusu vyanzo na marejeo ya Hadithi, Fiqhi, Ilmu-Rijal na historia ya Ahlu-Sunnah, sambamba na kutabahari kwake katika vyanzo na marejeo ya Kishia vilimpa uwezo wa kuweza kuzifanyia uhakiki na upembuzi nukta za pamoja na za hitilafu zilizopo baina ya madhehebu za Kiislamu na kuipanua fikra ya kuzikurubisha pamoja madhehebu hizo kadiri usuli na misingi yao ilivyoruhusu. Msaada na uungaji mkono wa kudumu wa kimaada na kimaanawi wa Ayatullah Burujerdi kwa Daru-Taqrib ni ithibati ya umuhimu mkubwa aliokuwa akilipa suala la umoja na mshikamano baina ya Waislamu. Tunaweza hata kusema kuwa baada ya Imam Khomeini (MA) ni nadra kumpata Marjaa Taqlidi aliyefanya jitihada kama zilizofanywa na Ayatullah Burujerdi katika suala la kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mtajiunga nami tena inshaaAllah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki. Basi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.

Tags