Mar 18, 2018 10:48 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (30)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 30.

Kwa wale wafuatiliaji wa kawaida wa kipindi hiki bila ya shaka mtakuwa mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulianza kuzungumzia chimbuko la kujengeka fikra ya kuasisi jumuiya ya kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu baina ya maulamaa wa Kishia na Kisuni na hasahasa fikra na mitazamo ya waasisi wake wawili yaani Sheikh Mahmoud Shalt'ut, Mufti Mkuu wa Misri na Sheikh wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar na Ayatullah Al-Udhma Burujerdi, mmoja wa Marjaa Taqlidi wakubwa zaidi katika Ulimwengu wa Kishia. Tulisema kuwa istilahi ya kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu ilizungumziwa kwa mara ya kwanza karibu miaka sabini iliyopita na taasisi ya "Daru-Taqrib Bainal-Madhahibil-Islamiyyah" mjini Cairo Misri. Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1327 hijria shamsia na jopo la maulamaa wakubwa wa Kisuni na Kishia. Tukafafanua kwamba baada ya Daru-taqrib kufanya uhakiki mpana na kufikia hitimisho kwamba hauwezi kupatikana mwafaka na kuzikurubisha pamoja madhehebu katika mijadala ya ilmul-kalam na ya kiitikadi likiwemo suala la Ukhalifa na Uimamu bali hata huenda mijadala juu ya masuala hayo ikasababisha kuibuka upya hitilafu, iliamua kuelekeza juhudi zake katika kutatua hitilafu za kifiqhi, ambazo hatimaye zilizaa matunda kwa fatua iliyotolewa na Sheikh Mkuu wa Al-Azhar Mahmoud Shalt’ut. Katika fatua yake hiyo, Sheikh Shalt’ut alisema, wafuasi wa madhehebu nne za Ahlu-Sunnah wanaweza kurejea katika masuala ya fiqhi kwenye madhehebu nyenginezo ikiwemo ya Imamiyyah Ithnaasharia; yaani kwa kufuata hukumu zilizotolewa na mafuqahaa wa madhehebu hizo. Lakini pia Sheikh Shalt’ut alitoa idhini ya kusomeshwa fiqhi ya madhehebu ya Shia sambamba na masomo ya fiqhi ya madhehebu za Ahlu Sunnah, hatua ambayo ilitoa mwanga mpya kwa wahadhiri na watafiti wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar. Sambamba na Sheikh Shalt’ut tukaeleza pia kwamba Ayatullah Al-Udhma Burujerdi, naye pia ni miongoni mwa Marjaa-Taqlidi watajika na mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kishia ambaye alikuwa siku zote akilipa umuhimu suala la umoja wa Waislamu na kuzikurubisha pamoja madhehebu zao.

 

Katika masuala ya Fiqhi ya Utabikishaji, Ayatullah Burujerdi alikuwa akiyapa umuhimu masuala yanayohitilafiwa; yaani alikuwa akiitakidi kwamba masuala ya kifiqhi, yasijadiliwe katika upeo wa madhehebu za Imamiyyah pekee lakini yanapasa yajadiliwe pia katika upeo wa madhehebu zote za Kiislamu, ambapo katika kila suala muhimu linalohitilafiwa, hoja za madhehebu zote zizingatiwe na kutiliwa maanani. Kwa sababu hiyo, alikichapisha kitabu cha "Masaailul-Khilaf" cha Sheikh Tusi baada ya mashaka mengi aliyopata ya kukifanyia masahihisho; na kila baada ya muda alikuwa akikichukua kitabu hicho kwenye darsa zake, akawa anazisoma ibara alizokusudia za maelezo ya Sheikh Tusi ili wanafunzi wake waweze kuzoea kidogo kidogo njia yake hiyo ya usomeshaji.

Ubunifu huo wa Ayatullah Burujerdi, uliwawezesha mujtahidi wa Kishia, mbali na kurejea vitabu vya fiqhi vya Shia Imamiyyah waweze pia kuvitalii vitabu vya fiqhi vya madhehebu nyengine. Kwa kufanya hivyo waliweza kubaini jitihada na umakini wa ufuatiliaji mambo uliofanywa na madhehebu hizo katika masuala ya kifiqhi na wakati huohuo kufikia kwenye nukta kwamba fiqhi ni elimu ya pamoja baina ya madhehebu zote za Kiislamu ambazo zote zina mafungamano ya pamoja, huku kila moja ikiwa na taathira kwa nyengine; na hivi sasa pia kila moja ikiwa na uwezo wa kufaidika na rai za madhehebu nyengine hususan katika masuala mapya yanayoibuka katika Fiqhi. Ayatullah Burujerdi alikuwa akiamini kwamba kuzitalii fatua maarufu za Ahlu Sunnah katika zama za Maimamu wa Ahlul Bayt (AS) humwezesha faqihi kuzifahamu hadithi na kauli za Maimamu, kwa sababu maelezo ya watukufu hao yalizingatia fatua zilizotolewa na maulamaa wa Kisuni. Wanafunzi wake wanasimulia kuwa, baadhi ya wakati Ayatullah Burujerdi alikuwa akisema: "Fiqhi ya Shia iko pembeni ya fiqhi ya Ahlu Sunnah; kwa sababu katika zama hizo, hukumu walizokuwa wakifuata na kutekeleza Waislamu zilikuwa ni fatua zilizokuwa zikitolewa na maulamaa wao; na wapokezi na masahaba wa Maimamu walikuwa wakiwauliza masuali watukufu hao, na wao Maimamu wakawa wanatoa majibu kwa kuzingatia fatua hizohizo."

 

Mtazamo wa ukurubishaji pamoja madhehebu wa Ayatullah Burujerdi ulikuwa na athari kwa fatua iliyokuja kutolewa na Sheikh Mahmoud Shalt'ut. Katika mtazamo wa Sheikh Shalt'ut moja ya masuala muhimu zaidi katika kufikiwa umoja ni kupatikana nukta ya pamoja ambayo madhehebu zote zina mwafaka na mtazamo mmoja juu yake. Sheikh Mkuu huyo wa Al Azhar anaitaja Qur'ani kuwa ndio nukta yenyewe ya pamoja huku akilielezea suala hilo kwa kusema: "Uislamu unawaita watu kwenye umoja; na mhimili na nguzo ambayo Waislamu wanatakiwa washikamane nayo na kukusanyika pamoja kando yake imeelezwa kuwa ni kushikamana na Kamba ya Mwenyezi Mungu. Jambo hili limeelezwa katika aya nyingi za Qur'ani tukufu. Maelezo ya wazi kabisa ya jambo hili yamo kwenye kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Suratu Aal Imran aliposema: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu pamoja wala msifarikiane. Mwenyezi Mungu amekataza mifarakano kwa sura mutlaki ambayo inajumuisha pia mifarakano kwa sababu ya taasubi. Hadithi sahihi inasema: Hakuna taasubi katika dini ya Uislamu. Katika sehemu nyengine, Sheikh Shalt'ut anakitaja Kitabu cha Allah na Sunna za Mtume wake kuwa nukta za pamoja baina ya madhehebu zote. Yeye anatafautisha kati ya hitilafu za kielimu zinazotokea kwenye duru za kielimu na taasubi za kiukereketwa wanazokuwa nazo baadhi ya watu wa kawaida. Katika kulizungumzia jambo hilo, Sheikh Shalt'ut anasema: "Hitilafu katika rai ni jambo la lazima kijamii na la kawaida ambalo haliwezi kuepukika; lakini hilo ni tofauti na hitilafu zinazozusha taasubi za kimadhehebu na mgando wa fikra. Taasubi zinakata Kamba ya mfungamano baina ya Waislamu na kupalilia mbegu za uadui na chuki ndani ya nyoyo zao; lakini kuhitilafiana kwa sababu ya kutafiti hakika na ukweli wa mambo sambamba na kuheshimu mtu fikra za wapinzani wake ni jambo la kupongezwa na lenye kukubalika.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mumenufaika na kuelimika na yale yote mliyoyasikia katika sehemu hii ya 30 ya mfululizo huu. Katika kipindi chetu kijacho inshaa Allah tutaendelea kuzungumzia historia ya dhana ya kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu katika fikra za Ayatullah Al-Udhma Burujerdi na Sheikh Mahmoud Shalt’ut. Basi hadi wakati huo kwa majaaliwa ya Mola nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags