Apr 05, 2018 01:26 UTC
  • Alkhamisi tarehe 5 Aprili 2018

L:eo ni Alkhamisi tarehe 18 Rajab 1439 Hijria sawa na Aprili 5, 2018.

Siku kama ya leo miaka 1429 iliyopita alifariki dunia mtoto mdogo wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ibrahim akiwa na umri wa miezi 18 tu. Ibrahim ambaye alifariki dunia kutokana na maradhi alikuwa mtoto wa kiume pekee wa Mtume ambaye hakuzaliwa na Bibi Khadija (as). Mama yake alikuwa Maria al Qibtiyya ambaye alitumwa na mfalme wa Misri ya wakati huo kuwa hadimu na mtumishi wa Mtume na aliolewa na mtukufu huyo baada ya kusilimu. Kifo cha Ibrahim kilimhuzunisha sana Mtume (saw) kwa sababu mtukufu huyo alikuwa akimpenda sana mtoto huyo.  

Kaburi la Ibrahim, mtoto wa Mtume Muhammad (saw)

Tarehe 18 Rajab miaka 1013 iliyopita alifariki dunia Ibn Samh huko katika mji wa mjini Andalucia. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa mtaalamu wa hesabu, nyota na tabibu. Alizaliwa katika mji wa Cordoba, Andalucia mnamo mwaka 370 Hijiria. Msomi huyu wa Kiislamu alifanya utalii na utafiti mwingi katika elimu za hesabu na nyota, sambamba na kuwalea wanafunzi wa zama zake. Kuna vitabu kadhaa vilivyoandikwa na Ibn Samh kwa lugha ya Kiarabu na miongoni mwavyo ni pamoja na kitabu kiitwacho "Al Madkhalu Ila al Handasah", "Al Muamalat" na "Kitabuz Zayj."

Siku kama ya leo miaka 433 inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 1585, yalifanyika mauaji ya halaiki katika mji wa Harlem nchini Uholanzi, ambako kilikuwa kitovu cha wapigania uhuru nchini humo. Mauaji hayo yalifanyika kwa amri ya Mfalme wa Uhispania. Jumla ya watu elfu sita wanaaminika kuwa waliuawa kwenye shambulio hilo. Hatimaye Uholanzi ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Uhispania 1609. 

Mji wa Harlem nchini Uholanzi

Siku kama ya leo miaka 224 iliyopita, aliuawa Georges Danton, aliyekuwa miongoni mwa vinara wa mapinduzi ya Ufaransa. Danton licha ya kusomea taaluma ya sheria, alikuwa mhamasishaji mahiri katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa. Danton alikuwa akiamini kuwa, sanjari na kuzuia machafuko na maafa ya kibinadamu, utawala wa kifalme nchini Ufaransa ulipaswa kutokomezwa. Amma Robes Pierre mmoja kati ya vinara wakubwa wa mapinduzi ya Ufaransa ambaye pia alikuwa mshindani wa Danton alichukua uamuzi wa kumtia mbaroni Danton na hatimaye kumuuwa. 

Georges Danton

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 1956, yalimalizika mashambulizi ya kinyama ya majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza. Majeshi ya utawala ghasibu wa Israel, siku ya tarehe 4 Aprili, yaliwauwa watu 56 na kuwajeruhi wengine 30 wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee. Nchi za Magharibi na jamii ya kimataifa hazikutoa radiamali yoyote kuhusiana na jinai hizo za Wazayuni.