Apr 08, 2018 12:38 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (31)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 31.

Katika vipindi viwili vilivyopita tulizungumzia chimbuko la kihistoria la kuasisiwa jumuiya ya kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu baina ya maulamaa wa Kishia na Kisuni hususan rai na fikra za shakhsia wawili miongoni mwa waasisi wa fikra hiyo, yaani Sheikh Mahmoud Shalt'ut, Mufti Mkuu wa Misri na Sheikh Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar na Ayatullah Al-Udhma Burujerdi, mmoja wa Marjaa Taqlidi wakubwa wa ulimwengu wa Kishia. Katika vipindi hivyo tulieleza kuwa mtazamo wa ukurubishaji madhehebu wa maulamaa hao wawili wakubwa ulikuwa na taathira kubwa katika kupatikana muelekeo mmoja baina ya Waislamu na kujenga misingi ya nadharia ya umoja wa Kiislamu. Ni kutokana na muelekeo huo ndipo Sheikh Shalt'ut akatoa fatua yake muhimu na ya kihistoria inayoeleza kwamba wafuasi wa madhehebu nne za Ahlu Sunnah wanaweza kufuata madhehebu nyengine ikiwemo ya Imamiyyah Ithnaasharia kwa maana ya kufuata hukumu zinazotolewa na mafuqahaa wa madhehebu hizo. Tumeeleza pia kwamba Ayatullah Al-Udhma Burujerdi, alikuwa mmoja wa Marjaa na maulamaa wakubwa, ambaye daima alikuwa akilipa umuhimu maalumu suala la umoja wa Waislamu na kuzikurubisha pamoja madhehebu zao. Yeye alikuwa akiitakidi kwamba masuala ya kifiqhi, yasijadiliwe katika duara la madhehebu za kifiqhi za Imamiyyah pekee, bali yazungumziwe katika duara pana zaidi la madhehebu zote za Kiislamu; na rai na hoja za madhehebu zote zizingatiwe katika kila suala muhimu ambalo madhehebu zote zinahitilafiana.

Chuo Kikuu cha al Azhar nchini Misri

 

Shahidi Ayatullah Murtadha Mutahhari amezungumzia mchango na nafasi ya Ayatullah Burujerdi katika suala la kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu kwa kuandika kama ifuatavyo: “Ayatullah Burujerdi, kinyume na baadhi ya maulamaa wa zama hizi ambao wanalizungumzia suala la “Ukhalifa” na “Uimamu” kwa namna inayosababisha kushtadi hitilafu, yeye alikuwa akiitakidi kwamba hili ni suala la kihistoria; na njia aliyotumia Imam Ali (as) katika kuamiliana na makhalifa inaonyesha kuwa, kwa ajili ya maslaha ya Uislamu haipasi kulishupalia na kulichochea suala hili, bali inapasa kufikiria masuala mengine yatakayowafanya Waislamu wawe wamoja katika kukabiliana na maadui mbalimbali; na hata alikuwa akiwahutubu baadhi ya maulamaa wa vyuo vya kidini vya Hawza kwa kuwaambia: “suala la Ukhalifa si hitajio la leo la Waislamu la kutufanya tugombane. Vyovyote lilivyokuwa, kwa sasa ni suala la kihistoria; lenye faida hii leo kwa hali waliyonayo Waislamu ni kwamba inapasa tujue wapi pa kuchukulia hukumu zetu”. Yeye alikuwa na hamu ya kuona yanakuwepo maelewano mazuri baina ya Shia na Suni, ambayo kwa upande mmoja yatahakikisha umoja wa Kiislamu ambao ni madhumuni makubwa ya dini hii takatifu unafikiwa; na kwa upande mwengine Ushia, fiqhi na mafundisho yake yataweza kutambulishwa kama vile yalivyo hasa katika jamii ya Masuni ambayo inaunda idadi kubwa zaidi ya Waislamu. Katika zama za Umarjaa wake, kwa mara ya kwanza baada ya karne kadhaa, uhusiano wa kirafiki na utaratibu wa kuandikiana barua ulianzishwa baina ya kiongozi huyo wa Waislamu wa Kishia na kiongozi wa Waislamu wa Kisuni Sheikh Abdulmajid Salim; na baada ya kufariki Sheikh Abdulmajid, mawasiliano hayo yakaendelea baina yake na Sheikh Mahmoud Shalt'ut, Mufti na Sheikh Mkuu wa Chuo cha Al-Azhar".

******

Misingi ya kifikra ya umoja wa Kiislamu ya Ayatullah Burujerdi ilijengeka kutokana na taathira ya baadhi ya maulamaa wa kipindi alipokuwa masomoni. Alimu huyo mkubwa wa Kiislamu alikuwa akiitakidi kwamba hitilafu baina ya madhehebu tano za Kiislamu za Shia, Hanafi, Hanbali, Maliki na Shafi'i, hazisababishwi na masuala yanayohusiana na usuli na misingi mikuu ya dini na kwamba mpasuko baina ya madhehebu za Kiislamu imekuwa na itaendelea kuwa sababu kuu ya hali ya kudhoofika nchi za Kiislamu, sambamba na madola ya kibeberu na ya maajinabi kuyadhibiti na kuyatawala mataifa ya Waislamu.

Kwa sababu hiyo mnamo mwezi wa Mfunguo Tatu Dhulhijjah mwaka 1328 hijria alitoa hukumu na kutangaza kuwa ni wajibu kuwepo "umoja baina ya Waislamu" na "kujiepusha na yale yote yanayosababisha mpasuko na unafiki" baina yao. Kutokana na mitaala na utafiti mkubwa na mpana aliofanya katika vitabu na rai za kifiqhi za maulamaa na madhehebu tofauti za Kisuni, Ayatullah Burujerdi alifikia kwenye hitimisho kwamba ikiwa mtu atakuwa na uelewa wa muhtawa na yaliyomo kwenye fatua maarufu za Ahlu-Sunnah katika zama za Maimamu maasumu (alayhimu-ssalam), itakuwa rahisi zaidi kwake kuelewa muhtawa wa hadithi na madhumuni ya maneno ya watukufu hao. Kwa sababu hiyo, yeye alikuwa akiamini kwamba kutalii na kuhakiki vitabu vya Ahlu-Sunnah ni miongoni mwa utangulizi wa lazima wa kufahamu fiqhi na kufikia daraja ya Ijtihadi; na yeye mwenyewe alikuwa amebobea na kutabahari kwa kiwango cha juu katika uwanja huo. Uelewa huo na kujishughulisha kwake kwa karibu na fiqhi ya Kisuni tunaweza kukutaja kama msingi mwengine uliochangia fikra zake kuhusu umoja wa Kiislamu.

 

Kama tulivyotangulia kueleza kuhusu fikra za Sheikh Mahmoud Shalt'ut juu ya umoja na kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu, ni kwamba moja ya misamiati mikuu katika fikra za Mufti na Sheikh Mkuu huyo wa zamani wa Al-Azhar ilikuwa ni msimamo wa Uislamu wa kupinga "taasubi". Yeye alikuwa akiitakidi kwamba Mwenyezi Mungu amekataza mifarakano kwa sura mutlaki ambayo inajumuisha pia mifarakano kwa sababu ya taasubi. Sheikh Shalt'uti alitafautisha kati ya hitilafu za kielimu zinazotokea kwenye duru za kielimu na taasubi za kiukereketwa wanazokuwa nazo baadhi ya watu wa kawaida na akiitakidi kwamba hitilafu katika rai ni jambo la lazima kijamii na la kawaida ambalo haliwezi kuepukika; lakini suala hilo ni tofauti na hitilafu zinazozusha taasubi za kimadhehebu na mgando wa fikra. Alikuwa akisisitiza kuwa taasubi zinakata Kamba ya mfungamano baina ya Waislamu na kupalilia mbegu za uadui na chuki ndani ya nyoyo zao; lakini kuhitilafiana kwa sababu ya kutafiti hakika na ukweli wa mambo sambamba na kuheshimu mtu fikra za wapinzani wake ni jambo la kupongezwa na lenye kukubalika. Alipoulizwa kama, kwa kuwa baadhi ya watu wana mawazo kwamba ili ibada na hukumu za miamala anayofanya Muislamu iwe sahihi lazima afanye hivyo kwa kufuata moja kati ya madhehebu nne tu maarufu bila kujumuisha madhehebu ya Shia Imamiyyah na madhehebu ya Zaydiyyah, je wewe unakubaliana kikamilifu na rai hii na unahisi haijuzu kufuata madhehebu ya Shia Imamiyyah? Sheikh Shalt'ut alijibu kwa kusema: "Uislamu haujamwajibishia mfuasi wake yeyote kufuata madhehebu maalumu; kila Muislamu ana haki kwa kuanzia tu kufuata yoyote katika madhehebu, ambayo maandiko na hukumu zake zimeratibiwa na kubainishwa kwa usahihi katika vitabu maalumu vya madhehebu hiyo. Na kila mtu anayefuata madhehebu moja anaweza kuamua kufuata madhehebu nyengine yoyote, na hakuna ubaya wowote ule kwake yeye.

*******

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mtajiunga nami tena inshaaAllah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki. Basi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.

Tags