Apr 08, 2018 12:41 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (32)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 32.

Bila shaka wapenzi wasikilizaji mngali mnakumbuka kuwa katika vipindi vitatu vilivyopita tumezungumzia chimbuko la fikra ya kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu kwa lengo la kufikia umoja wa Kiislamu na hasahasa fikra na mitazamo ya waasisi wawili wakuu wa rai hiyo ambao ni Sheikh Mahmoud Shalt'ut, Mufti Mkuu wa Misri ambaye pia alikuwa Sheikh Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar wakati huo na Ayatullah Al-Udhma Burujerdi, mmoja wa Marjaa Taqlidi wakubwa wa ulimwengu wa Kishia. Tulinukuu maneno ya Shahidi Ayatullah Mortadha Motahhari, kuhusiana na nafasi muhimu ya Ayatullah Burujerdi katika kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu. Kwa mujibu wa Ayatullah Motahhari, mtazamo wa Ayatullah Al-Udhma Burujerdi kuhusu suala la “Ukhalifa” na “Uimamu” ni kuwa, hiyo ni kadhia ya historia na kwamba njia aliyotumia Imam Ali (as) katika kuamiliana na makhalifa inaonyesha kwamba, kwa ajili ya maslaha ya Uislamu haipasi kulishupalia na kulichochea suala hili, bali inapasa kufikiria masuala mengine yatakayowafanya Waislamu wawe wamoja katika kukabiliana na maadui mbalimbali wanaowakabili.

Kwa upande wa Sheikh Mahmoud Shalt'ut, kutokana na muelekeo wa kimaendeleo aliokuwa nao katika ufahamu wa Uislamu, Mufti Mkuu huyo wa Misri alikuwa akiitakidi kwamba kama zilivyo madhehebu nyengine za Ahlu-Sunnah inajuzu kisharia kufuata hukumu za kiibada za madhehebu ya Jaafari, ambayo ni maarufu kama Shia'tul-Imamiyyah Al-Ithnaashariyyah. Mnamo tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal mwaka 1378 hijria, sambamba na maadhimisho ya Maulidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW kwa mujibu wa mapokezi ya madhehebu ya Shia yanayosadifiana pia na kuzaliwa Imam Jaafar Sadiq (as) Imam wa fiqhi ya Jaafari, Sheikh Mahmoud Shalt'ut alitoa fatua ya kujuzisha kufuata madhehebu ya Shia. Matini ya fatua hiyo ambayo aliitoa mbele ya hadhara ya wawakilishi wa madhehebu ya Shia Imamiyyah, Zaydiyyah, Hanbali, Shafi'i, Maliki na Hanafi, inasema: "dini ya Uislamu haijamkalifisha mfuasi wake yeyote kufuata madhehebu maalumu; bali kila Muislamu anaweza kufuata madhehebu yoyote ambayo imenukuliwa kwa njia sahihi, na hukumu zake zimeandikwa kwenye vitabu mahususi vya madhehebu hiyo; na kila mtu anayefuata moja ya madhehebu hizi nne (za Shafi'i, Hanbali, Maliki na Hanafi) anaweza kuhamia madhehebu nyengine. Madhehebu ya Jaafari, maarufu kama madhehebu ya Imamiyyah Ithnaashariyyah ni madhehebu ambayo inajuzu kisharia kufuata kama inavyojuzu kufuata madhehebu za Ahlu-Sunnah. Kwa hivyo inafaa Waislamu wabainikiwe na ukweli huu na kujiweka mbali na taasubi mbaya na zisizofaa walizonazo kuhusiana na madhehebu maalumu; kwa sababu dini ya Mwenyezi Mungu na sharia zake hazifuati madhehebu mahususi na wala haitohodhiwa na kumilikiwa na madhehebu maalumu. Bali viongozi wa madhehebu zote walikuwa ni mujtahidi; na ijtihadi zao zinakubalika mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; na kwa wale watu ambao si wenye rai na ijtihadi, wao wanaweza kufuata madhehebu yoyote wanayotaka na kutekeleza hukumu za fiqhi za madhehebu hiyo; na kuhusiana na hili hakuna tofauti yoyote baina ya masuala ya kiibada na ya miamala".

Image Caption

 

Mbali na kuzungumzia athari za taasubi katika kuchochea na kusababisha mifarakano baina ya Waislamu, Sheikh Mahmoud Shalt'ut anasisitizia pia nafasi ya njama za maajinabi katika kuwafarakanisha Waislamu na kueleza kwamba Ukoloni hautokuwa radhi daima kuona Umma wa Kiislamu umeungana na kuwa kitu kimoja; kwa sababu unajua kwamba endapo utaungana, utasimama pamoja kukabiliana na tamaa za wakoloni. Kuhusiana na nukta hiyo marehemu Mirza Khalil Kamrei anasimulia kumbukumbu moja kuhusu Sheikh Shalt'ut inayomfanya mtu aelewe ukubwa wa njama za Ukoloni. Mirza Khalil Kamrei anasimulia kama ifuatavyo: "Mimi nilifanya safari kuelekea Misri, nikakutana mara mbili na Sheikh Shalt'ut; na katika kukutana kwetu kuna siri ambayo alinisimulia. Alinambia: "Mimi tokea zamani, takriban miaka thelathini nyuma nilikuwa na hamu ya kuona vitabu vya fiqhi ya Imamiyyah, nikataka nipatiwe vitabu vya fiqhi ya Imamiyyah kutoka Iraq na Iran, lakini hadi hivi karibuni wakati Misri ilipotoka kwenye minyororo ya Ukoloni, vitabu hivyo vilikuwa havifiki na vilikuwa vikifanyiwa sensa; lakini baada ya kukombolewa Mfereji wa Suez, vitabu vyenu vilikuja, nikavisoma na kila kitu kikanibainikia wazi kabisa; na ndipo nikatoa fatua ile pasina kuathiriwa na kiongozi yeyote au kauli yoyote ile".

Katika hatua aliyoichukua kwa madhumuni ya kukabiliana na taasubi za kimadhehebu na vilevile njama za maajinabi, wakati wa safari aliyofanya huko Baitul Muqaddas kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa Kiislamu kuhusu Palestina, Sheikh Mahmoud Shalt'ut aliungana pamoja na maulamaa wengine kusali Sala ya jamaa iliyosalishwa na Ayatullah Kashif Al-Ghit'aa.

 

Wapenzi wasikilizaji natumai mpaka hapa tumeweza kupata mwanga wa kiwango fulani kuhusu nafasi na mchango muhimu uliotolewa na maulamaa hao wawili wa Kishia na Kisuni katika kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu. Hata hivyo jambo la kusikitisha ni kwamba msingi uliowekwa na wanazuoni hao katika suala la kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu umekuja kubomolewa na harakati na makundi potofu kutoka madhehebu za Shia na Suni, makundi ambayo yameubomoa na kuuvuruga msingi huo wa kuleta umoja na kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu uliojengwa na wanazuoni hao wawili. Harakati hizo zimekuwa na nafasi kubwa katika kuzusha hitilafu, vita na umwagaji damu baina ya Waislamu. Harakati hizo mbili ni ile ya Masalafi na Matakfiri katika madhehebu ya Suni, na harakati ya Ushia wa Uingereza ulioko miongoni mwa Mashia.

Wasikilizaji wapenzi, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki kwa leo umemalizika, hivyo sina muda kuishia hapa huku nikitumai kuwa mumeelimika na kunufaika na yote mliyoyasikia katika mfululizo huu. Tutakutana tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo, ambapo tutakuja kuzungumzia harakati hizo mbili potofu ambazo zimechangia kuvurugika msingi wa umoja na kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags