Apr 08, 2018 12:44 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (33)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 33.

Kwa wale wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki bila shaka mngali mnakumbuka kuwa mwishoni mwa mazungumzo yetu katika sehemu ya 32 ya kipindi hiki nilikuahidini kuwa katika kipindi chetu cha leo tutazungumzia misingi ya fikra na mielekeo ya harakati na matapo mawili potofu yaliyoko miongoni mwa wafuasi wa madhehebu mbili za Suni na Shia, ambayo ni tapo la Ukufurishaji na lile la Ushia wa Kiingereza. Matapo haya mawili ambayo yamezipa kisogo jitihada kubwa zilizofanywa na Sheikh Mahmoud Shalt’ut na Ayatullah Burujerdi za kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu kwa ajili ya kuwa na umoja wa Kiislamu, yamekuwa na taathira kubwa katika kuwasha moto wa fitna, hitilafu, vita na umwagaji damu baina ya Waislamu.

Wakufurishaji au Masalafi ni moja ya harakati za kifikra na kisiasa iliyoko katika madhehebu ya Suni ambayo haikubaliani na muelekeo wa kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu wa Sheikh Mahmoud Shalt’ut. Mbali na kuipinga fatua aliyotoa ya kujuzisha kufuata madhehebu ya Shia Imamiyyah Ithnaashariyyah, Matakfiri wamewasha moto wa hitilafu na fitna baina ya Waislamu kwa hukumu yao ya kuhalalisha kumwaga damu ya Mashia. Usalafi ni tapo linaloitakidi kuwa fikra na matendo ya kundi fulani la masahaba na waliowafuatia wao, yaani Matabiina ni hoja na marejeo ya kufuatwa kisheria kwa ajili ya maisha ya zama za sasa. Wafuasi wa itikadi ya Kisalafi wanatambulika kama watu wenye fikra potofu kwa sababu, kwa upande mmoja wameachana na misingi ya fiqhi ya madhehbu nne za Ahlu-Sunnah, na kwa upande mwengine, kwa hatua yao ya kufungua mlango wa ijtihadi kwa kutegemea ufahamu wa masahaba, wamefungua njia ya kuibuliwa baadhi ya fatua zisizo sahihi za kiutashi na za kufurutu mpaka. Harakati hii, tab’an ina chimbuko la kihistoria pia. Vuguvugu la itikadi za aina hii lilianza kwenye karne ya nne hijria, lakini baadaye likaratibiwa kama fikra maalumu na Ibnu Taymiyah na wanafunzi wake; na hatimaye likahuishwa tena katika zama hizi na Muhammad bin Abdulwahhab na kutekelezwa kupitia watawala wa Aal Saud.

Kwa kunasibishwa na jina la Muhammad bin Abdulwahhab, Masalafi wanajulikana pia kwa jina la Mawahabi. Katika muelekeo huohuo “Utakfiri” ni anuani ya mtu au harakati ambayo chimbuko lake huwa aghalabu imetokana na tafsiri mbalimbali za Kisalafi na Kiwahabi. Kinyume na vipimo vinavyotumika rasmi katika hukumu na sharia za dini, watu wenye fikra ya Utakfiri kwa maana ya ukufurishaji huwatuhumu Waislamu wengine wote kuwa ni watu waliokufuru na kutoka kwenye dini kwa sababu tu ya kutokuwa na itikadi sawa na yao.

 

Sheikh Yusuf Al-Qardhawi ni mmoja wa watu ambao wamekuwa na nafasi kubwa katika ubunifu wa nadharia ya harakati hii potofu ya kufarakanisha umma katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kwa hatua yake ya kuitilia shaka fatua ya Sheikh Mahmoud Shalt’ut, Qardhawi amekuwa sababu ya kufufuka tena mielekeo ya hisia za chuki na uadui dhidi ya Shia katika Ulimwengu wa Kiislamu. Alipohutubia vijana mjini Cairo, Misri katika kikao kilichoandaliwa na muungano ulio chini ya uongozi wake na ambacho kilifanyika kwa anuani ya “Maulamaa wa Baadaye”, Sheikh Yusuf Qardhawi alisema: “Sheikh Mahmoud Shalat’ut hajatoa fatua ya kujuzisha kufuata madhehebu ya Jaafari katika masuala ya kiibada.” Akijibu suali aliloulizwa kuhusiana na kutolewa na fatua hiyo, Qardhawi alisema: “nileteeni mimi hiyo fatua… fatua hii iko kwenye kitabu chake gani?... mimi sijawahi kuiona fatua hii… nani miongoni mwenu anasema amewahi kuiona fatua hii kwenye kitabu au jarida fulani?”

Akiendelea kuitilia shaka fatua ya kihistoria ya Sheikh Mahmoud Shalt’ut, Sheikh Yusuf Qardhawi aliongezea kwa kusema: “mimi nimeishi na Sheikh Shalt’ut miaka na miaka na nimekuwa miongoni mwa watu walio karibu naye sana. Mimi sijawahi kuona fatua kama hii. Sikuwahi kumuona yeye kusema kitu kama hiki. Mimi nimekusanya na kutayarisha vitabu vinne vilivyoandikwa na Sheikh Shalt’ut; Sheikh Ahmad Al-Asal, mkuu wa zamani wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Islamabad ndiye aliyeshirikiana na mimi; na katika utangulizi wa chapa ya mwanzo ya kitabu cha Shalt’ut, tumeshukuriwa mimi na yeye (Sheikh Al-Asal).”

Umoja wa Kiislamu

 

Pamoja na hayo utiliaji shaka uliofanywa na Sheikh Yusuf Qardhawi na maulamaa wengine wa tapo la Ukufurishaji kuhusiana na fatua ya kihistoria ya Sheikh Mahmoud Shalt’ut hauna ushahidi wa kihistoria wa kuweza kuutetea, bali ushahidi wote uliopo unatilia nguvu ukweli kuhusu kutolewa kwa fatua hiyo. Jarida la Al-Bashaair liliandika katika toleo lake la tarehe 14 Machi mwaka 2009 makala ambayo ndani yake imemnukuu Sheikh Jamal Qut’b, mmoja wa maulamaa wa Al-Azhar akieleza kwamba, wawili hao, yaani Qardhawi na Al-Asal hawakukusanya maandiko yote ya Sheikh Shalt’ut; na hakuna mtu yeyote awezaye kukana kwamba fiqhi ya Shia na Zaydiyyah imekuwa ikifundishwa katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar hata kabla ya zama za Sheikh Shalt’ut.

Siku ya pili yake tovuti ya Islam Online ilichapisha makala iliyoandikwa na Sheikh Isam Talima kwa anuani isemayo: “Naam, Sheikh Shalt’ut ametoa fatua ya kujuzisha kufuata madhehebu ya Jaafari katika masuala ya kiibada.” Katika makala yake hiyo, Sheikh Talima aliandika: “mimi hapa sitaki kujadili kuhusu kuwa sahihi au kutokuwa sahihi fatua ya Shalt’ut. Ninachojadili mimi ni kuthibiti au kutothibiti kutolewa kwa fatua hii. Kwanza lazima niseme kwamba Sheikh Shalt’ut alitoa fatua hii. Fatua hii imetolewa kama ilivyo kwa anuani ya ‘Fatua ya Kihistoria’ kwenye jarida la “Risalatul-Islam” lililokuwa likichapishwa mjini Cairo na Daru-Taqrib Bainal-Madhahibil-Islamiyyah. Katika utangulizi wa maelezo hayo, mhariri mkuu wa jarida anaeleza kwamba, kurasa za mwanzo za jarida zimelipa nafasi maalumu tukio muhimu la kihistoria ambalo ni fatua ya muadhamu Ustadh Mkuu Sheikh Mahmoud Shalt’ut, Sheikh wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar, Allah ampe umri mrefu na aujaalie umma wa Kiislamu uendelee kuneemeka na elimu, kheri na juhudi zake.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mtajiunga nami tena inshaaAllah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo ili kuendelea na maudhui hii katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags