Apr 17, 2018 13:04 UTC
  • Kongamano la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran Iran
    Kongamano la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran Iran

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 37.

Kwa wale wafuatiliaji wa kawaida wa kipindi hiki bila shaka mngali mnakumbuka kuwa mazungumzo yetu katika kipindi kilichopita yaliishia katika kuizungumzia fikra ya Utaifa, ambapo tulisema katika baadhi ya vipindi vya historia, Utaifa ulitumika kuzipa nchi nguvu na uwezo, na katika baadhi ya vipindi ulisaidia kujikomboa nchi zilizokuwa kwenye pingu na minyororo ya Ukoloni. Lakini tukaashiria pia kwamba, kuna baadhi ya zama, ambapo Utaifa ulikuwa sababu ya kuzuka vita vya umwagaji damu kati ya nchi mbalimbali. Suali la kujiuliza hapa ni hili: kuna uhusiano gani kati ya Utaifa na fikra ya Kiislamu, na je Utaifa umekuwa na nafasi gani katika kuwaunganisha au kuwatenganisha Waislamu?  Kuhusiana na nukta hii inapasa tuseme kuwa kuna tofauti za mitazamo baina ya wanafikra wa Ulimwengu wa Kiislamu kuhusu nafasi ya Utaifa katika Uislamu. Tunaweza kuzigawa tofauti hizo za rai na mitazamo katika makundi matatu makuu.

Kundi la kwanza ni la wanafikra wanaoitakidi kuwa hakuna mgongano wowote kati ya kuwepo dini ya ulimwengu mzima sambamba na kukubali uwepo wa mgawanyiko wa kikabila, kimbari na asili za watu wa kaumu na mataifa tofauti; na kwa mtazamo wao hakuna mkinzano baina ya Utaifa na tafsiri ya Umma wa Kiislamu, na kwamba kuwa umma na kuwa na utambulisho mwengine wa utaifa ni jambo lililotiliwa mkazo na Qur’ani Tukufu kwa mujibu wa aya ya 13 ya Suratul Hujurat isemayo: "Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume (mmoja) na mwanamke (mmoja). Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane." Katika nadharia hii, Utaifa unatafsiriwa kuwa ni hisia za upendo wa ndani ya nafsi ya mtu kwa jamaa zake na wananchi wenzake. Watetezi wa fikra hii huwa aghalabu wanatolea ushahidi Hadithi isemayo “Kuupenda wat’ani ni sehemu ya imani” na wanaitakidi kuwa mtu kuwa na mapenzi ya nchi yake sio tu hakukinzani na dini bali wanakuchukulia kuwa ni sehemu ya dini.

 

Kundi la pili ni la wanafikra wa Ulimwengu wa Kiislamu wanaoamini kwamba Utaifa ni moja ya madhihirisho na matunda ya ustaarabu wa Magharibi na utamaduni unaotawala ndani yake; na wanaitakidi kuwa hisia na mielekeo ya utaifa katika fikra za Kimagharibi maana yake ni kwamba pale kundi moja la watu wenye asili, historia na lugha moja wanapojiweka kwenye eneo moja lenye mipaka maalumu ya kijiografia, huwa wamekubali kujiwekea asili na mwanzo mwengine mpya wa kukabiliana na Mwenyezi Mungu ambao wameufanya asili ya thamani zao zote; na kwa kuwa fikra hiyo ni dhihirisho la fikra ya Umwanadamu wa Magharibi yaani Humanism, kwa hivyo Utaifa hauendani na dini ya Uislamu.

Kundi hili la wanafikra wanatilia nguvu hoja yao kwa kutegemea Hadithi mbalimbali ikiwemo ile isemayo: "Enyi watu nyinyi nyote mnatokana na Adam, na Adam ametokana na udongo. Hakuna ubora kwa Mwarabu juu ya asiyekuwa Mwarabu isipokuwa kwa kumcha Mwenyezi Mungu". Kwa mtazamo wa wanafikra hao maana ya umma mmoja katika Uislamu si kaumu au watu wenye asili maalumu; bali ni umma unaoundwa na watu mbalimbali wa kaumu, asili, rangi, mila na desturi tofauti, ambao kitu kinachowaunganisha pamoja ni imani na itikadi yao kwa misingi ya dini; na kwa mujibu wa hukumu ya wazi kabisa ya Qur’ani, ubora wa watu unatokana elimu na uchamungu au kwa amali na idili yao katika dini. Kwa hivyo wanafikra hao wanaupinga na kuukana Utaifa na badala yake kubainisha sifa maalumu na jumuishi kwa ulimwengu mzima za dini ya Uislamu. Na kundi la tatu la wanafikra ni wale wenye mtazamo wa kati na kati baina ya makundi hayo mawili ya mwanzo. Ayatullah shahidi Murtadha Mutahhari ni chemchemu ya wanafikra wa kundi hilo.  Kwa mtazamo wake yeye, Utaifa si kitu cha kulaumiwa na kukemewa katika upande wake chanya, yaani kuwa na upendo nao; na Uislamu unazikubali na kuzitambua akthari ya haki hizo. Lakini wakati huohuo unakosoa na kulaumu upande hasi wa Utaifa. Bila ya kutaka kuingia kwenye mjadala wa kinadharia wa kuujadili uhusiano wa Utaifa na fikra ya umoja na ujengaji umma mmoja wa Kiislamu inapasa tuseme kuwa tajiriba na uzoefu ulioshuhudiwa kivitendo unathibitisha ukweli huu, kwamba licha ya baadhi ya taathira zake chanya hususan katika kusaidia uhuru na ukombozi wa nchi nyingi wa kujivua na pingu na minyororo ya ukoloni, Utaifa umekuwa zaidi chachu ya kuzusha mifarakano baina ya nchi za Kiislamu.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akizungumza na Waislamu wa madhehebu mbalimbali kuhusiana na udharura wa umoja na mshikamano baina yao

 

Ikiwa tutakubaliana na tafsiri ya shahidi Mutahhari kuhusu Utaifa na umma mmoja tutaweza pengine kudai kwamba pande hasi na zenye athari mbaya za Utaifa yaani kuzusha mifarakano ni nyingi zaidi kuliko pande zake chanya na zenye athari nzuri yaani za mapenzi kwa nchi. Ndiyo kusema kwamba katika Ulimwengu wa Kiislamu, badala ya kusaidia kuleta mshikamano na muelekeo mmoja baina ya nchi za Kiislamu, Utaifa umechangia zaidi kuleta utengano na mifarakano baina ya nchi hizo. Hata hivyo tusisahau pia kuashiria nafasi ya madola maajinabi katika kushamirisha na kutilia nguvu pande hasi za Utaifa kwa madhumuni ya kufikia malengo yao haramu. Imam Khomeini (MA) ambaye ni mmoja wa walinganiaji wa umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu katika uga wa nadharia na uchukuaji hatua kivitendo ameufafanua vizuri mfungamano huo kwa kusema: “Madola makubwa ambayo yanataka yawanyongeshe Waislamu, yaghusubu maliasili zao na kupora mali zao, tangu miaka mingi nyuma yalikuwa yakipanga mipango na njama mbalimbali, ambapo moja ya mipango yao hiyo ni suala la mielekeo ya Utaifa. Uislamu umekuja kuwaunganisha pamoja watu wa mataifa yote ya dunia; Waarabu, Waajemi, Waturuki, Wafarsi na kujenga umma mmoja mkubwa uitwao Umma wa Uislamu… Hawa wanaozusha mifarakano baina ya Waislamu kwa jina la utaifa na mielekeo ya kimakundi na kitaifa, hawa ni askari wa majeshi ya shetani na wasaidizi wa kazi zinazofanywa na madola makubwa na wapinzani wa Qur’ani tukufu.” (Sahifa ya Nuru, Juzuu ya 13, ukursa wa 225).

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mtajiunga nami tena inshaaAllah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki ambapo tutakuja kuendelea na maudhui yetu hii. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags