Apr 21, 2018 10:59 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (48)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 48.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki, bila shaka mngali mnakumbuka kuwa mazungumzo yetu katika kipindi kilichopita yaliishia pale tulipoeleza kwamba ili kuleta umoja na mshikamano ndani ya mataifa yao, viongozi wa nchi nyingi huamua “kujibunia adui” na kumtumia kwa ajili ya kufikia lengo hilo. Tukabainisha kwamba kuwachochea majirani zao ili waanzishe uhasama na vita ni moja ya mbinu zinazotumiwa na viongozi wa nchi zinazokabiliwa na hatari ya mfarakano wa ndani. Na kwa kutaka waondokane na shari ya wapinzani na kuepusha mfarakano kati ya matapo tofauti ya ndani, viongozi hao huanzisha chokochoko dhidi ya majirani zao ili kutokana na jibu hasi watakalotoa waweze kuwasha cheche ya mjadala ndani ya nchi zao wa kuanzisha au kuhuisha utambulisho mmoja utakaoleta umoja baina ya wananchi wote.

 Kwa kutoa mfano ni kwamba moja ya uchambuzi na uhakiki muhimu uliozungumziwa katika duru za kimataifa baada ya kusambaratika Shirikisho la Kisovieti la Urusi ya zamani na kumalizika enzi za Vita Baridi yaani Cold War ni kwamba, katika kipindi chote cha Vita Baridi, Marekani iliweza kubuni hisia za “udhidi” kuhusiana na Ukomunisti na kuleta umoja katika Ulimwengu wa Ubepari chini ya uongozi wake; na kwa utaratibu huo ikaweza kufuatilia na kufanikisha malengo yake katika maeneo mbalimbali duniani kwa kuanzisha vituo vya kujengea satua na ushawishi wake katika nchi nyingi. Baada ya kusambaratika kambi ya Mashariki ya Ukomunisti na kuondoka hali hiyo ya “udhidi” uliibuka mjadala na uchambuzi wa kina kwamba, baada ya kumpoteza adui huyo Marekani itakabiliwa na tatizo kubwa la utambulisho kwa kimombo “Identity Crisis” na Uhalali wa Kisheria yaani “Legitimacy” kwa upande wa ndani na katika uga wa kimataifa. Kwa sababu hiyo tusubiri kushuhudia kudhoofika kwa nguvu za Marekani, isipokuwa tu kama nchi hiyo itaweza kupata kitu kingine cha “udhidi” kitakachochukua nafasi ya Urusi na idiolojia ya Ukomunisti. Nukta nyingine inayopasa kuzingatiwa ni kwamba kuwepo adui wa pamoja tu hakuwezeshi kupatikana umoja na mshikamano wa ndani, lakini kuwa na uelewa wa kuwepo adui huyo wa pamoja na kuitakidi kwamba kuna uhasama na chuki ambazo anazifanya ni miongoni mwa masharti ya lazima kwa ajili ya kujengeka utambulisho ambao ni msingi wa kuwepo umoja. Kwa kutoa mfano ni kwamba, hata kama kutakuwepo na adui, lakini ikiwa utakosekana uelewa kuhusiana na kuwepo kwa adui huyo na anayoyafanya, hautopatikana umoja na mshikamano.

 

Ikiwa tutaichukulia hatua ya kuundwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu wakati huo ya OIC kuwa ni moja ya vielelezo muhimu vya kuleta umoja na kuwa na muelekeo mmoja katika Ulimwengu wa Kiislamu, inapasa tukiri pia kwamba suala la Palestina lilikuwa na taathira kubwa katika uundwaji wa jumuiya hiyo. Ukweli ni kwamba kilichowasha cheche ya mwenge wa kuasisiwa Jumuiya ya Kiislamu ni tukio la mwaka 1969 la kuchomwa moto msikiti mtukufu wa Al Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu. Tukio hilo lililosababishwa na Myahudi mmoja mwenye taasubi liliamsha hasira na ghadhabu za Waislamu duniani na kuwafanya viongozi wa mataifa ya Waislamu waitikie kilio na malalamiko ya wananchi wao na kuwafikishia walimwengu ujumbe wa ghadhabu za Waislamu. Saudi Arabia na Morocco zilikuwa miongoni mwa nchi zilizofanya jitihada kubwa za kufanikisha kuitishwa kikao hicho, ambapo hatimaye mkutano huo wa mataifa ya Waislamu ukafanyika mwezi Septemba mwaka 1969. Viongozi wa nchi 24 za Kiislamu walihudhuria mkutano huo uliofanyika katika mji mkuu wa Morocco, Rabat, ambapo ajenda tatu kuu zilijadiliwa na kuzungumziwa na viongozi hao wa nchi washiriki. Ajenda hizo ni kuchomwa moto msikiti wa Al Aqsa, kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Waarabu na Israel na hali ya mji wa Baitul Muqaddas.

Katika kikao hicho cha kwanza cha Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), mbali na kutiliwa mkazo kuimarishwa mshikamano kati ya nchi za Kiislamu kwa kuzingatia thamani za Kiislamu, washiriki walitangaza kufungamana kwao na Hati ya Umoja wa Mataifa na Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu, kufanya juhudi za kulinda amani na usalama kwa madhumuni ya kupanua ushirikiano baina yao sambamba na kueleza kuchukizwa kwao na tukio la kuchomwa moto msikiti wa Al Aqsa. Viongozi wa nchi 24 washiriki wa kikao hicho walitaka mji wa Baitul Muqaddas urejee katika hali yake ya kabla ya Juni 1967 na wakazitaka nchi zote duniani hususan Ufaransa, Uingereza, Shirikisho la Kisovieti la Urusi pamoja na Marekani zisipuuze mfungamano mkubwa walionao wafuasi wa dini ya Uislamu kwa mji wa Baitul Muqaddas na uamuzi wa serikali za nchi za Kiislamu wa kutaka kukombolewa mji huo. Lakini zaidi ya hayo watangaze rasmi kwamba kuendelea kukaliwa kijeshi na Israel ardhi za nchi za Kiarabu kuanzia Juni 1967 kumezidi kuwatia wasiwasi wananchi na serikali za nchi za Kiislamu na kwa hivyo wachukue hatua zinazotakiwa kuhakikisha askari wote wa Israel wanaondoka haraka katika ardhi hizo. Viongozi wa nchi za Kiislamu waliohudhuria mkutano huo vilevile walitangaza kwamba wanawaunga mkono kikamilifu wananchi wa ardhi ya Palestina na mapambano yao ya kuikomboa ardhi yao na kurejeshewa haki zao.

 

Wapenzi wasikilizaji, Palestina siku zote imekuwa moja ya mihimili mikuu ya hatua zilizokuwa zikichukuliwa na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu wakati huo ambapo katika miaka yote ya shughuli zake, jumuiya hiyo ambayo sasa inajulikana kama Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imekuwa kila mara ikitangaza uungaji wake kwa mapambano ya wananchi wa Palestina; japokuwa mwenendo huo umekuwa na hali zote mbili za ukakamavu na ulegevu na hata kuna wakati umewahi kurudi nyuma zaidi na kuachana na misimamo ya asili ya kutetea “jihadi” ya wananchi wa Palestina. Uamuzi wa kuanzishwa mfuko wa Quds katika kikao cha saba cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa OIC, kuundwa kamati maalumu ya Quds mnamo mwaka 1975 na kuanzishwa ofisi ya Kiislamu ya kuisusia Israel ni miongoni mwa hatua za kivitendo zilizochukuliwa na taasisi hiyo ya mataifa ya Kiislamu. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nayo pia wakati iliposhika uenyekiti wa OIC ilizitumia ipasavyo fursa zilizopo katika jumuiya hiyo ya mataifa ya Kiislamu kwa ajili ya kuimarisha umoja wa umma wa Kiislamu. Katika kipindi hicho, Iran ilichukua misimamo thabiti na ya wazi kabisa ya kulaani vikali hatua za kujipanua, za ukandamizaji na za kigaidi za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Vilevile kwa kuzingatia kwamba katika kipindi hicho Israel iliendeleza tena ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, suala ambalo liliibua wasiwasi katika Ulimwengu wa Kiislamu; kwa kutumia diplomasia makini na amilifu, Iran iliutumia ipasavyo uwezo wa nchi za Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na utawala huo ghasibu. Katika kipindi hicho cha uenyekiti wake wa OIC, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwatangazia walimwengu kwa uwazi zaidi hatua na vitendo vya kinyama vinavyofanywa na utawala dhalimu wa Israel na kuuwekea utawala huo haramu mashinikizo makali; na kwa njia hiyo ikaweza kuandaa mazingira mwafaka ya kupatikana umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu na msimamo na muelekeo wa pamoja kati ya nchi wanachama wa OIC.

 Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umemalizika. Hivyo tusite hapa kwa leo hadi tutakapokutana tena inshallah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika sehemu ya 49 ya mfululizo huu.

Tags