Jumatano, Mei 23 2018
Leo ni Jumatano tarehe saba Ramadhani mwaka 1439 Hijria, inayosadifiana na tarehe 23 Mei mwaka 2018 Miladia.
Miaka 1429 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 7 Ramadhan mwaka wa 10 tangu kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad SAW, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, aliaga dunia Abu Talib, ami na mtetezi mkubwa wa Mtume SAW katika mji wa Makka. Baada ya kufariki Abdul Muttalib, babu mtukufu wa Nabii Muhammad SAW, Abu Talib ndiye aliyebeba jukumu la kumlea Mtume, na akawa bega kwa bega na mwana huyo wa nduguye katika hali zote. Baada ya kupewa Utume Nabii Muhammad SAW, Abu Talib hakumwacha mkono mtukufu huyo na akasimama imara kukabiliana na washirikina wa kikureishi. Lakini baada ya kufariki dunia Abu Talib washirikina walishadidisha maudhi na manyanyaso dhidi ya Bwana Mtume SAW, kiasi kwamba kutokana na hali ngumu mno iliyomkabili, hatimaye kwa amri ya Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo alihajiri kwa kuhama Makka na kuhamia Madina ambako aliasisi utawala wa kwanza wa Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 400 iliyopita, yaani tarehe 23 Mei 1618 Milaadia, vilianza vita vya miaka 30 vya kidini barani Ulaya. Madhehebu ya Kikristo ya Kiprotestanti yaliundwa mwanzoni mwa karne ya 16 Milaadia na hivyo kuzusha mpasuko mkubwa katika safu za Wakristo. Baada ya hapo, Wakristo wa madhehebu mawili ya Kikatoliki na Kiprotestanti waliingia vitani kwa karne nyingi. Moja ya vita maarufu baina ya Wakristo wa madhehebu hayo mawili, ni vile vilivyotokea kwenye muongo wa pili wa karne ya 17 Milaadia. Vita hivyo viliendelea kwa muda wa miaka 30 mfululizo. Sehemu kubwa ya vita hivyo ilitokea nchini Ujerumani. Vita hivyo vilikuwa na pandashuka nyingi. Katika kipindi chote cha vita hivyo, nchi za Ufaransa, Sweden na Denmark ziliwaunga mkono Wakristo wa Kiprotestanti na serikali ya Uhispatia na Ufalme wa Roma waliwaunga mkono Wakatoliki. Vita vya miaka 30 baina ya madhehebu mawili ya Wakristo huko barani Ulaya, vilimalizika kwa kutiwa saini makubaliano ya Westphalia mwaka 1648 Milaadia. Ijapokuwa uhasama mkubwa baina ya Wakristo wa Kiprotestanti na Kikatoliki ulitokana na ugomvi wa muda mrefu baina ya madhehebu hayo mawili, lakini sababu kubwa za vita hivyo ilikuwa ni kugombania ardhi na masuala ya kisiasa ya tawala za wakati huo barani Ulaya. Moja ya matokeo muhimu ya vita hivyo ni kumalizika kwa namna vita vya kimadhehebu baina ya madhehebu hayo mawili ya Kikristo na kuanza kupata nguvu mirengo ya utaifa na ya ubaguzi wa rangi na kizazi barani Ulaya.
Na siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, yaani tarehe 23 Mei 1915 Milaadia, Italia ilijiingiza katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Kuingia Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia kulianza wakati nchi hiyo ilipoivamia Austria bila ya sababu yoyote isipokuwa tu kwa tamaa ya kujinufaisha kisiasa na kupanua utawala wake. Muda mchache baadaye, serikali ya Italia ilitangaza vita dhidi ya ufalme wa Uthmania na hivyo kuufanya moto wa vita uwake kwa ukali zaidi. Hata hivyo, licha ya kupata ushindi kundi la nchi Waitifaki, Italia ikiwa moja yao, lakini nchi hiyo haikufaidika kivyovyote na vita hivyo. Matunda pekee iliyopata ni kuwaulisha raia wa Italia baada ya kuwaingia Waitaliano milioni tano na nusu katika vita hivyo. Kwa maneno mengine ni kuwa maamuzi na siasa za Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia zilifeli, kwani haikupata matunda yoyote ya maana kwa kujiingiza kwake kwenye vita hivyo.
Katika siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, alijiua Heinrich Himmler Mkuu wa zamani wa Shirika la Kijasusi na Usalama la Ujerumani ya Kinazi. Himmler alizaliwa mwaka 1900 na alipofikisha umri wa miaka 34 aliweza kupanda cheo na kuwa mkuu wa shirika hilo la kijasusi na usalama la Ujerumani (Gestapo). Heinrich Himmler anahesabiwa kuwa mmoja kati ya viongozi wauaji na wamwagaji damu ambaye aliongoza operesheni kadhaa za mateso na kuuwa watu nchini humo. Himmler alitiwa mbaroni baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya Nurenberg nchini Ujerumani, lakini kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo aliamua kujiua mwenyewe baada ya kunywa sumu.