Alhamisi, 31 Mei, 2018
Leo ni Alkhamisi tarehe 15 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, mwaka 1439 Hijria inayosadifiana na tarehe 31 Mei mwaka 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita, yaani tarehe 15 Ramadhani mwaka wa tatu Hijria:
Alizaliwa Imam Hassan al-Mujtaba (as), mmoja wa Ahlul-Bait wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Imam Hassan (as) alikulia na kupata malezi na usimamizi wa babu yake Bwana Mtume SAW, mama yake Bibi Fatwimat Zahraa binti ya Mtume na baba yake, yaani Imam Ali (as). Baada ya kuuawa shahidi baba yake mwaka wa 40 Hijiria, mtukufu huyo alifanya kazi kubwa ya kusimamia na kuwaongoza Waislamu. Mwanzoni Waislamu wengi walimbai na kumpa mkono wa utiifu Imam Hassan, lakini mfumo wa utawala wa Bani Umayyah uliokuwa ukiongozwa na Muawiya mwana wa Abu Sufiyan ambao wakati huo ulikuwa na nguvu kubwa, ulianzisha uadui na chuki dhidi ya Imam huyo. Hatimaye Imam Hassan (as) alijiandaa kukabiliana na Bani Umayyah, lakini viongozi wengi wa jeshi lake walidanganyika na ahadi za uongo za maadui na kumuacha peke yake Imam, hali iliyomlazimisha mtukufu huyo kufanya suluhu na mtawala huyo wa Bani Umayyah kwa lengo la kuilinda na kuinusuru dini tukufu ya Uislamu.

Miaka 186 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 31 Mei mwaka 1832 aliuawa Évariste Galois, mtaalamu mwenye kipawa cha hisabati wa Ufaransa. Galois alizaliwa tarehe 25 Oktoba mwaka 1811 katika mji mmoja ulioko karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Paris. Alipotimiza umri wa miaka 12, Galois alianza kusoma athari mbalimbali za kihistoria na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha ukweli wa hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa. Galois aliuawa katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 21 baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Imeelezwa kuhusiana na Galois kuwa laiti gwiji huyo wa hisabati asingeuliwa alipokuwa katika rika hilo la ujana utaalamu wa hisabati leo hii ungekuwa umepiga hatua mbele zaidi kwa miaka mia tatu.

Siku kama ya leo miaka 1056 iliyopita, yaani tarehe 15 Ramadhani mwaka 383 Hijria:
Aliaga dunia katika mji wa Nishabur kaskazini mashariki mwa Iran Abubakr Muhammad bin Abbas Kharazmi, msomi na mwanafasihi mtajika wa Kiislamu. Kharazmi alikuwa hodari mno wa kubainisha mambo kwa ghibu na alikuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mashairi na historia ya Waarabu. Abubakr Muhammad bin Abbas Kharazmi ameacha athari iitwayo "Rasail" ambayo ni tunu kubwa katika fasihi ya Kiarabu na ambayo ni maarufu kwa jina la Rasail Kharazmi.

Na siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 31 Mei mwaka 1910 Afrika Kusini ilipata uhuru kwa kuungana maeneo manne yaliyokuwa makoloni ya Uingereza katika eneo la kusini mwa Afrika. Muungano huo wa makoloni hayo uliiwezesha nchi hiyo kupata uhuru wake kamili mwaka 1931, lakini Wazungu walio wachache walitwaa hatamu za madaraka ya nchi. Hata hivyo baada ya mapambano magumu na ya miaka mingi ya wazalendo weusi wakiongozwa na shujaa Nelson Mandela, hatimaye mwaka 1991 utawala wa wazungu wachache ulilazimika kuhitimisha mfumo wake wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
