Jumamosi, Juni 2, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 17 Ramadhani mwaka 1439 Hijria, sawia na tarehe Pili Juni mwaka 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia Mtume Mtukufu Muhammad SAW alisafiri kutoka Makka hadi Baitul Muqaddas na kupaa mbinguni kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Aya ya kwanza ya Sura ya al Isra inatoa maelezo kuhusu muujiza huo mkubwa ikisema. "Ametakasika aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya ishara zetu. Hakika yeye ni mwenye kusikia na mwenye kuona." Kwa kuzingatia aya hiyo na hadithi za Mtume Muhammad SAW, wakati mtukufu huyo alipokuwa katika safari ya Miiraji alionyeshwa siri nyingi za Mwenyezi Mungu SW, viumbe vyake Jalali na hatima ya wanadamu katika ulimwengu wa Akhera. Tukio hilo ni miongoni mwa miujiza mikubwa ya Mtume Muhammad SAW na linadhihirisha nafasi ya juu ya mtukufu huyo.

Tarehe 17 Ramadhani miaka 1437 iliyopita, vita vya Badr, moja kati ya vita maarufu vya Mtume Muhammad SAW, vilitokea katika eneo lililoko kati ya Makka na Madina. Badr ni jina la kisima kilichoko umbali wa kilomita 120 kusini magharibi mwa mji wa Madina, ambako kulipiganwa vita vya kwanza kati ya Waislamu na washirikina. Vita vya Badr vilitokea huku washirikina wakiwa na wapiganaji wengi waliokaribia 920 na jeshi la Kiislamu likiwa na wapiganaji 313 na silaha chache. Hata hivyo imani thabiti ya Waislamu iliwafanya washinde vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita, yaani tarehe Pili Juni mwaka 1882 alifariki dunia Giuseppe Garibaldi, kamanda mzalendo na kiongozi wa vita vya umoja wa Italia. Katika kipindi cha ujana wake Garibaldi alijishughulisha na kazi mbalimbali, ambapo baadaye alijiunga na jeshi. Hatimaye Giuseppe Garibaldi alifanikiwa kuwa kamanda wa wapigania uhuru wa Italia. Garibaldi alifanya juhudi kubwa za kuijenga Italia moja; na kwa sababu hiyo akajulikana katika historia ya nchi hiyo kama shujaa wa taifa.

Na siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, mnamo tarehe Pili Juni mwaka 1942 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Mjerumani Marshal Erwin Rommel maarufu kwa jina la Mbwa Mwitu wa Jangwani, alianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya jeshi la Uingereza katika maeneo ya kaskazini mwa Afrika. Kabla ya mashambulizi hayo, Waingereza walikuwa wamefanya hujuma nchini Libya na kuitwaa nchi hiyo kutoka mikononi mwa jeshi la Wajerumani wa Kinazi. Hata hivyo mashambulizi ya jeshi la Erwin Rommel ambayo yalidumu kwa kipindi cha mwezi mmoja yaliwawezesha wanajeshi wake kuidhibiti tena Libya na eneo la al Alamein lililoko kaskazini mwa Misri na karibu na bandari muhimu ya Alexandria. Wajerumani walikaribia kuutwaa mfereji wa kistratijia wa Suez lakini mwezi Novemba mwaka 1942 Waingereza wakafanya mashambulizi makubwa dhidi ya jeshi la Erwin Rommel na hatimaye kulishinda.