Hadithi ya Uongofu (129)
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Kipindi chetu kilichopita kiliendelea kuzungumzia maudhui ya maamkizi na kusalimiana pamoja na umuhimu wake katika Uislamu. Tulisema kuwa, wanadamu wote popote walipo katika kona ya dunia wanapokutana husalimiana na kuamkuana ili kuonyesha huba na upendo uliopo baina yao. Waislamu nao kwa upande wao wakiwa na lengo la kuvutia urafiki na udugu husalimiana na kutoleana salamu. Salamu kwa Waislamu ni muhimu mno kiasi kwamba, ni katika nembo rasmi za Waislamu ambapo husalimia pindi wanapokutana. Kwa maana kwamba, jambo la kwanza wanalolifanya Waislamu baada ya kukutana ni kusalimiana na kutoleana salamu ambayo ni mashuhuri kama "Assalaamu Alaykum". Aidha tulinukunukulieni hadithi kutoka kwa Imamu Ja'afar bin Muhammad Swadiq AS ambaye amenukuliwa akisema: Katika ishara za unyenyekevu ni kumsalimia kila unaekutana naye. Leo tutazungumzia suala la kupeana mikono, umuhimu na faida zake. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki, hii ikiwa ni sehemu ya 29 ya mfululizo huu. Karibuni.
Uislamu unatilia mkazo maalumu suala la umoja na mshikamano wa watu katika mhimili wa itikadi ya Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Ili kufikia katika umoja huu, kuna haja ya nyoyo za watu kuwa na huba, huruma na uhusiano wa kirafiki baina yao. Kusalimia ni moja yya mifano ya wazi ya kivitendo ya kuleta uhusiano huu. Kwa mujibu wa wataalamu wa elimu ya saikolojia ni kwamba, salamu ni taa ya kijani ya mfungamano wa kijamii.
Wakati watu wawili wanapokutana, nyuso zao hutizamana, midomo hufunguka na kutamka neno salamu na hivyo kuonyesha huba na urafiki. Linalofuatia baada ya hapo na ili kudhihirisha zaidi huba na upendo wao hupeana mikono na kuminya mikono hiyo. Thamani ya kitendo hicho ni kubwa kiasi kwamba, Imamu Muhammad al-Baqir AS anasema: Wakati Muumini anapotoka nyumbani kwake kwa ajili ajili ya kwenda kumtembelea ndugu yake Muumini, Mwenyezi Mungu humuandikia thawabu kwa kila hatua anayoipiga na humfutia dhambi na humpandisha daraja. Wakati Muumini anapogonga mlango, milango ya mbinguni humfungukia na wakati anapokutana na ndugu yake na akapeana naye mkono huwakutanisha pamoja uso kwa uso na hujifakharisha kwa Malaika wake na kusema: Enyi Malaika! Waangalieni waja hawa wawili ni kwa namna gani wanatembeleana kwa ajili yangu na kuoneshana huba na upendo. Inastahiki kwangu mimi kutowaadhibu kwa moto wa Jahanamu.
Kwa hakika dini Tukufu ya Kiislamu kama ambavyo imetilia umuhimu suala la urafiki na mahaba, imezingatia mno suala la izza, heshima na utukufu wa mwanadamu. Kupiga magoti na kuonyesha taadhima na unyenyekevu ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu na mtu hana haki kuinama na kuonesha unyenyekevu mbele ya wanadamu wenzake.
Kwa mujibu wa maarisho ya Uislamu, Waislamu kwa daraja zozote watakazokuwa nazo, wanapokutana wanapaswa kusalimiana na kupeana mikono.
Mtume SAW amenukuuliwa akisema kuwa: Wakati mnapokutana, amkuaneni na peaneni mikono kwani kupeana mikono ni salamu bora kabisa, na kufanya hivyo hupelekea kuondoa vinyongo, chuki na husuda.
Imekuja katika adabu za kupeana mikono kwamba: Wanaopeana mikono wabananishe viganja vyao vya mikono hali ya kuwa vidole vimetengana, na kadiri inavyowezekana kila mtu ajitahidi kuchelewa kuondoa mkono wake kutoka katika mkono wa mwenzake. Mtume SAW alikuwa akifanya suna hii nzuri. Alipokuwa akipeana mkono na mtu alikuwa hauondoi mpaka mtu aliyepeana naye mkono alegeze mkono wake au auondoe. Aidha katika kupeana mikono suala la kubinya mikono nalo limeusiwa. Tab'an, ubinyaji mkono huo chimbuko lake linapaswa kuwa huba na upendo na haupaswi kuwa sababu ya mtu mmoja kuumia. Kwa maana kwamba, wakati mtu anapobinya mkono wa mwenzake wakati wa kupeana mikono hapaswi kuubinya kiasi cha mwenzake kuhisi maumivu. Imam Muhammad bin Ali al-Baqir AS amesema: Watu wawili waumini wanapopeana mikono, mkono wa rehma wa Mwenyezi Mungu huwa baina ya mikono yao, na mkono huo wa huba na upendo wa Mwenyezi Mungu huwa zaidi kwa mtu ambaye anampenda zaidi mwenzake.
Kuhusiana na suala hilo hilo la kupeana mikono Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: Unapokutana na ndugu yako katika dini, mpe mkono na udhihirishe furaha na bashasha ili wakati wa kutengana naye dhambi zako ziondoke kama yanavyodondoka majani ya miti; na hii hali ya kupeana mikono baina ya Waislamu wawili madhali ipo (yaani mikono hiyo haijaachana) Mwenyezi Mungu huwa ni msimamzi wao.
Wapenzi wasikilizaji, Imam Ali bin Abi Twalib AS anaendelea kubainisha zaidi maudhui ya kuupeana mikono kwa kusema kuwa: Peaneni mikono hata na maadui au watu ambao hamuwapendi, kwani Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 34 ya Surat Fussilat kwamba:
Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa liliojema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu.
Miongoni mwa adabu nyingine za kupeana mikono ni kukariri mara kwa mara kitendo hicho. Kwa mfano kama mtu yuko safarini, katika kikao auu mjumuiko fulani ni vizuri kupeana mikono na watu wengine hata mara kadhaa. Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Ubeidah anasimulia kwamba: Nilikuwa pamoja na Imam Muhammad Baqir AS katika moja ya safari zake. Kwanza mimi nilikuwa nikipanda kipando, kisha Imam alikuwa akifanya hivyo pia. Baada ya kupanda katika vipango, Imam alikuwa akitusalimia na kutuuliza hali kama vile ndio kwanza tunaonana. Kisha alikuwa akipeana mikono na sisi. Kila wakati tulipokuwa tukiteremka kutoka katika vipando, Imam Baqir AS alikuwa akitusalimia tena, akipeana mikono na sisi na kisha kutujulia hali na kisha alikuwa akisema: Kwa kupeana mikono, waumini wawili husamehewa dhambi zao kama majani ya miti yanavyodondoka na kupuputika. Jicho la rehma ya Mwenyezi Mungu huwa pamoja nao mpaka watakapotengana.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha leo cha Hadithi ya Uongofu ambapo tulizungumzia umuhimu wa kupeana mikono wakati wa kusalimiana katika Uislamu umefikia tamati. Tukutane tena wiki ijayo kwa majaaliwa yake Mola jalia.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh….