Jumamosi, 27 Oktoba, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 17 Mfunguo Tano Safar 1440 Hijria, mwafaka na tarehe 27 Oktoba 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 544 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la Abus-Su’ud, faqihi na mfasiri wa Kiislamu katika kijiji cha Mudares karibu na mji wa Istanbul huko Uturuki. Baada ya kuhitimu masomo yake, Abus-Su’ud alijishughulisha na ufundishaji na kufanya kazi ya ukadhi mjini Istanbul, kazi aliyoendelea nayo hadi mwisho wa uhai wake. Abus-Su’ud alikuwa hodari katika masuala mbalimbali ya kijamii na aliweza kuandaa sheria za kiidara kwa mujibu wa dini ya Kiislamu katika utawala wa Othmania. Mbali na kuzungumza lugha ya Kituruki, alizungumza pia lugha za Kifarsi na Kiarabu. Msomi huyo wa Kiislamu ametunga mashairi pia katika lugha hizo. Miongoni mwa vitabu vya Abus-Su’ud ni pamoja na ‘Irshadul-Aqlis-Saliim’ ‘Dua Nameh’ ‘Qanun Nameh’ na ‘Mafrudhaat'.***

Katika siku kama ya leo miaka 185 iliyopita, kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Sheikh Abdul Rahim Sultanul-Qurrai Tabrizi, qaari mkubwa wa Qur’ani Tukufu na mmoja wa walimu mashuhuri wa fani ya qiraa, huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kujifunza fani hiyo kutoka kwa baba yake, Sultanul-Qurrai Tabrizi alifahamiana na Sheikh Shamil Dagestani na kushirikiana naye. Wakati Sheikh Shamil Dagestani alipoandaa jeshi kwa ajili ya kupambana na Warusi, Sultanul-Qurrai alifanya safari kuelekea Dagestan ili kushiriki katika harakati hiyo. Baadaye alirejea Tabriz na kuanzisha hawza ya kisomo cha Qur’ani na ni wakati huo ndipo akapewa lakabu ya Sultanul-Qurrai. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na ‘Risala katika elimu ya Tajwidi’ Sultanul-Qurrai alifariki dunia mwaka 1336 Hijiria mjini Tabriz. ***

Miaka 113 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Norway ilivunja muungano wake na Sweden na kujitangazia uhuru. Kabla ya karne ya 14 Norway ilikuwa nchi yenye ushawishi na moja ya madola vamizi. Hata hivyo mnamo mwaka 1380 ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Denmark na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo kwa muda wa karne 4. ***

Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, baada ya Japan kupigana vita na nchi mbili za China na Russia kwa miaka kadhaa na kupata ushindi katika vita hivyo, iliunganisha rasmi ardhi ya Korea na ardhi yake. Korea iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Japan hadi mwaka 1945 wakati Japan iliposhindwa katika Vita vya Pili vya Dunia. ***

Na miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Muhammad Ayub Khan alifanya mapinduzi nchini Pakistan na kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Tukio hilo lilitokea miaka 11 baada ya Pakistan kupata uhuru, ambapo Jenerali Muhammad Ayub Khan aliyekuwa mmoja wa makamanda wa jeshi alichukua hatamu za uongozi baada ya kufanya mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji damu. Kufuatia mapinduzi hayo, Iskander Mirza aliyekuwa Rais wa kwanza wa Pakistan akalazimika kuachia madaraka. Baada ya mapinduzi hayo, Muhammad Ayub Khan ambaye alichukua nyadhifa za Urais na Waziri Mkuu alitangaza serikali ya kijeshi nchini humo. Hata kama baada ya miaka 7 Ayub Khan aliibuka mshindi katika uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini humo mwaka 1965, lakini alianza kukabiliwa na mashinikizo baada ya kuongezeka matatizo ya kiuchumi na kisiasa. Hatimaye mwaka 1969, Ayub Khan aliachia ngazi na kukabidhi uongozi wa nchi kwa enerali Yahya Khan aliyekuwa mkwewe . ***
