Nov 03, 2018 12:50 UTC
  • Ruwaza Njema (5)

(Kumuiga al-Mustafa (saw) katika uadilifu, usawa na kumuhimidi Mwenyezi Mungu)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya tano ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambapo tunachambua fadhila na sifa mbalimbali za akhlaqi aali ya Mtume Mtukufu kwa lengo la kuiga na kuzifuata sifa hizo njema kama tulivyoamrishwa kufanya na Mwenyezi Mungu Mwenyewe Subhanahu wa Taala katika kitabu chake kitakatifu cha Qur'ani. Kutekeleza wajibu huu muhimu humfikisha mwanadamu katika daraja za juu za ukamilifu kwa sababu hilo huwa limetokana na kumfuata shakhsia na mtukufu ambaye amefikia upeo wa ukamilifu wa kimaanawi, naye si mwingine bali ni Bwana wa viumbe wote, Muhammad al-Mustafa (saw)

*********

Wapenzi wasikilizaji tunaanza kipindi hiki kwa kuangazia baadhi ya Hadithi na Riwaya zilizopokelewa katika vitabu vya kuaminika vya Hadithi kuhusiana na akhlaqi ya hali ya juu ya Mtume Muhammad (saw) kuhusiana na uadilifu na usawa katika kuamiliana na wanadamu wenzake, ambapo tunaanza kwa kuashiria Hadithi ifuatayo ya Imam Swadiq (as) ambayo imenukuliwa katika kitabu cha al-Kafi. Imam anasema: 'Mtume (saw) alikuwa akigawa mtazamo wake kwa masahaba zake; akimtazama huyu na kumtazama yule kwa usawa…… na kamwe hakuwahi kunyoosha na kuachilia miguu yake mbele ya masahaba zake.'

 

Riwaya nyingine iliyonukuliwa katika kitabu hicho hicho cha Kuleini kutoka kwa Imam Swadiq (as) kuhusiana na uadilifu na usawa aliouonyesha Mtume Mtukufu (saw) kwa masahaba na wafuasi wake ni hii ifuatayo. Imam anasema: 'Watu wawili walifika mbele ya Mtume (saw); Mtu mmoja kutoka kundi la Answar na mwingine kutoka ukoo wa Thaqif. Yule wa Thaqif akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Nina haja! Mtume (saw) akamjibu: Amekutangulia ndugu yako huyu wa Answar. Yule wa Thaqif akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mimi nina haraka ya safari….. Yule Answar akamwambia Mtume: Nimemuruhusu, ewe Mtume wa Mwenyezi  Mungu!....'

Imepokelewa mwishoni mwa Riwaya hii kwamba Mtume (saw) hakukidhi haja ya yule Thaqafi licha ya kuwa alikuwa anatoka kabila lake la Quraish, ila baada ya kuruhusiwa kufanya hivyo na yule Answari, na kisha baadaye akakidhi haja ya huyo Answari.

*********

Na katika uadilifu na usawa mkubwa ulioonyeshwa na Bwana Mtume kwa masahaba na wafuasi wake ni heshima aliyoionyesha kwa watu kwa mujibu wa viwango vyao vya utukufu na juhudi zao za kumridhisha Mwenyezi Mungu. Ammar bin Hayyan amepokelewa katika kitabu cha al-Kafi akisema: 'Nilimwambia Aba Abdillah as-Swadiq (as) kuhusiana na matendo mema anayonifanyia mimi Ismail mwanangu. Akasema (as): Nilikuwa ninampenda kabla ya hapo, na hivi sasa ninampenda hata zaidi. Hakika siku moja dada wa kunyonya wa Mtume (saw) alimtembelea, na alipomwona alifurahi sana na akamtandikia shuka ili apate kuketi juu yake. Kisha alimzungumzisha kwa bashasha na tabasamu (kwa furaha), hadi ulipofika wakati wa yeye kusimama na kuondoka. Muda si mrefu alifika hapo ndugu wa kiume wa yule dada na wala Mtume (saw) hakumfanyia alivyomfanyia huyo dada yake. Wakamwambia Mtume (saw), ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Umemfanyia dada yake kile ambacho hukumfanyia yeye, hali ya kuwa yeye ni mwanaume? Mtume (saw) akasema: Dalili yake ni kuwa dada yake huyo alikuwa akiwatendea wazazi wake wema zaidi kumliko yeye.'

 

Ama kuhusiana na mfano bora wa Mtume Mtukufu katika kuhimidi na kumshukuru Muumba wake kutokana na neema nyingi na zisizokuiwa na mwisho alizowapa wanadamu humu duniani, Imam Ali (as) amepokelewa katika kitabu cha Amaali cha Sheikh Tousi akisema: 'Kila kulipokucha na jua kuchomoza, Mtume (saw) alikuwa akisema: Alhamdulillahi Rabbil Alameen Hamdan Kathiran Ala Kulli Hala. Na Kisha kusema: Shukran, Shukran mara 360.'

*********

Miongoni mwa mambo ya kuvutia zaidi aliyoyafanya Mtume Mtukufu (saw) kwa ajili ya kuhimidi na kumshukuru Muumba wake ni ibada yake iliyojaa ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu. Imepokelewa katika kitabu cha al-Kafi kutoka kwa Imam Muhammad al-Baqir (as) kwamba alisema: 'Mtume (saw) alikuwa kwa Aisha usiku wake. (Aisha) Akamuuliza Mtume, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni kwa nini unajitaabisha na kujisumbua hali ya kuwa umesamehewa dhambi yako iliyopita na inayokuja? Mtume (saw) akamjibu: Ewe Aisha, ni vipi nitakosa kuwa mja mwenye kushukuru?' Imam Baqir (as) anaendelea kusema: 'Na Mtume (saw) alikuwa akisimama kwa nchi za vidole vya miguu yake hadi vikavimba na hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu akateremsha Aya ya: Taha. Hatukukuteremshia Qur'ani ili upate mashaka.

 

Wapenzi wasikilizaji miongoni mwa mifano bora zaidi ya Mtume Mtukufu (saw) kuhimidi na kumshukuru Muumba wake kutokana na neema nyingi alizompa ni kuifundisha familia yake kuhusiana na umuhimu wa kushukuru neema. Tunasoma katika Riwaya ifuatayo ambayo imenukuliwa katika kitabu cha al-Kafi kutoka kwa Imam Ja'ffar as-Swadiq (as). Anasema: 'Siku moja Mtume (saw) aliingia katika chumba cha Aisha ambapo aliona hapo kipande cha mkate alichokaribia kukikanyaga Aisha. Mtume alikichukua kipande hicho cha mkate na kukila na kisha kusema: Ewe Humaira! Iheshimu neema ya Mwenyezi Mungu kwa sababu inapoiondokea kaumu yoyote ile neema hiyo, huwa hairejei kwa haraka.'

**********

Tunamwomba Mwenyezi Mungu aweze kutupa sote taufiki zaidi ya kuweza kuiga na kumfuata Bwana wa Manabii wote, Mtume wetu Muhammad (saw), Allahumma Ameen.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Ruwaza Njema ambacho mmekisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti Jamhuri ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags