Jan 05, 2019 08:58 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 818, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 139 hadi 141 ambazo zinasema:

وَإِنَّ يُونُسَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ

Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume.

إِذْ أَبَقَ إِلَى الْفُلْكِ الْمَشْحُونِ

Alipo kimbia katika jahazi lilio sheheni. 

فَسَاهَمَ فَكَانَ مِنَ الْمُدْحَضِينَ

Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walio shindwa. 

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia habari za kaumu ya Nabii Lut (as). Katika kuendelea kuzungumzia kwa muhtasari habari za Mitume mbalimbali, aya tulizosoma zinamzungumzia Nabii Yunus (as). Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaokoa Mitume wake kadhaa, akiwemo Nabii Nuh, Ibrahim, Musa, Harun, Ilyas na Lut (as) na shari ya maadui zao, akawashinda wapinzani wao na kuwateremshia adhabu. Lakini kuhusu Nabii Yunus (as), hali ilikuwa namna nyingine kabisa. Kilichotokea hasa ni kwamba, wakati watu wa kaumu yake walipoona ishara za kushukiwa na adhabu walitubia; na Allah SW akawatakabalia na kuwarehemu; na badala yake akamtahini kwa kumtia kwenye msukosuko Nabii Yunus (as) kwa sababu ya kuitelekeza kaumu yake. Kwa mujibu wa hadithi na mapokezi ya historia, Nabii Yunus (as), kama walivyokuwa Mitume wengine, aliwapa maonyo na indhari watu wa kaumu yake kwa kuwataka waache shirki, kuabudu masanamu na kufanya mambo maovu. Lakini hawakuyajali kabisa maneno yake, na ni watu wachache tu miongoni mwao ndio waliomwamini Mtume huyo. Mwenyezi Mungu alimteremshia Wahyi Nabii Yunus kwamba baada ya muda si mrefu adhabu itawashukia watu hao. Yeye aliamua kuondoka kwenye mji ule akiandamana na mmoja wa waliomwamini na kuelekea upande wa baharini. Walipofika pwani walikuta merikebu iliyojaa mizigo na abiria, wakaomba na wao waruhusiwe kuabiri chomboni; na wenye merikebu hiyo wakawakubalia, wakawachukua na wao. Walipofika katikati ya bahari, merikebu yao ilishambuliwa na nyangumi aliyekuwa tayari ameshachanua kinywa chake. Wenye chombo walibaini kwamba lazima wamtoe mhanga abiria mmoja la sivyo hatari inayowanyemelea itawafika wote walioabiri jahazini. Kwa hivyo wakaamua kupiga kura ili kumchagua abiria watakayemtosa kwenye kinywa cha nyangumi, ili aiache merikebu na wasafiri waliosalia wabaki salama. Kura ikamwangukia Nabii Yunus; kwa hivyo ikabidi yeye atoswe kinywani mwa nyangumi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mitume wanapaswa wawe na subira, uvumilivu mkubwa na kifua kipana. Kwa hivyo kama wataonyesha kuwa na uvumilivu mdogo, Mwenyezi Mungu atawatahini na kuwatia kwenye msukosuko mkubwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuijua historia na yaliyojiri katika maisha ya Mitume, umma na kaumu zilizopita kunatupa funzo na somo kwa ajili ya maisha yetu ya leo katika dunia hii iliyojaa dhulma na ukafiri. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika mazingira yenye hali sawa kwa ajili ya kuchagua watu wanaotakiwa, unaweza kutumiwa utaratibu wa kura, kwani kufanya hivyo kumejuzishwa pia katika Uislamu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 142 hadi 144 ambazo zinasema:

فَالْتَقَمَهُ الْحُوتُ وَهُوَ مُلِيمٌ

Basi samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa.

فَلَوْلَا أَنَّهُ كَانَ مِنَ الْمُسَبِّحِينَ

Na lau asingelikuwa ni katika wanao mtakasa (Mwenyezi Mungu), 

لَلَبِثَ فِي بَطْنِهِ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ

Bila ya shaka angeli kaa tumboni mwake mpaka siku ya kufufuliwa.

Kama ilivyoelezwa katika aya tulizosoma, nyangumi yule alikuwa ameamriwa na Mwenyezi Mungu ammeze Nabii Yunus; kwa hivyo kwa takdiri ya Mola, kura ikamwangukia Mtume huyo. Lakini Mola huyohuyo aliyemwamuru nyangumi ammeze Nabii Yunus, ni mweza wa kumbakisha hai Mtume wake huyo tumboni mwa samaki huyo kwa muda wowote ule autakao. Wakati Nabii Yunus alipoona hajadhuriwa hata kidogo na nyangumi yule na ameweza kubaki hai ndani ya tumbo lake, ndipo alipobaini nini hasa kilichotokea. Hapo akamwelekea Allah, akamwomba maghufira na kutubia kwa kutotimiza wajibu wake ipasavyo. Kukiri na kuungama kwa Nabii Yunus kulikoandamana na majuto na kujilaumu nafsi yake, kulimfanya arehemewe kwa kuandaliwa mazingira ya kuokoka. Nyangumi yule alielekea hadi ufukweni, akafungua kinywa chake, na Yunus (as) akatoka tumboni mwake. Ni wazi kwamba, kama si msamaha aliopata kwa Mola, Nabii Yunus angesalia ndani ya tumbo la samaki huyo mkubwa mpaka Siku ya Kiyama. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wakati mwingine wanyama hufanya mambo ya ajabu na yasiyo ya kawaida kwa amri ya Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wakati tunapotanzwa na kukabiliwa na matatizo, suluhisho lake si kukwepa jukumu na masuulia. Kwani si hasha kufanya hivyo kukatusababishia matatizo makubwa zaidi. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kustaghafiru na kumsabihi Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa njia za kuokoka na majanga na matatizo. Ni kama alivyofanya Nabii Yunus (as), ambapo baada ya kumezwa na kukwama kwenye giza la ndani ya tumbo la samaki, alimuelekea Allah SW, Mola pekee wa haki na kumwomba msamaha na maghufira.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 145 hadi 148 za sura yetu ya Ass'affat ambazo zinasema:

فَنَبَذْنَاهُ بِالْعَرَاءِ وَهُوَ سَقِيمٌ

Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yu mgonjwa.

 وَأَنبَتْنَا عَلَيْهِ شَجَرَةً مِّن يَقْطِينٍ

Na tukamuoteshwa mmea wa kabila ya mung'unye.

وَأَرْسَلْنَاهُ إِلَىٰ مِائَةِ أَلْفٍ أَوْ يَزِيدُونَ

Na tulimtuma kwa watu laki moja au zaidi.

 فَآمَنُوا فَمَتَّعْنَاهُمْ إِلَىٰ حِينٍ

Basi wakaamini, na tukawastarehesha kwa muda.

Aya hizi, ambazo zinasimulia sehemu ya mwisho ya mkasa uliompata Nabii Yunus ndani ya tumbo la samaki, zinasema: Kwa amri ya Mwenyezi Mungu, nyangumi alielekea hadi pwani ya bahari, akafungua mdomo wake na kumtema Yunus (as). Mtume huyo, ambaye kama ilivyotarajiwa, alikuwa taabani na amedhoofu sana, hakuweza hata kuinua mguu kutembea akajionyoosha palepale alipokuwa. Mwenyezi Mungu akaotesha mmea wa jamii ya mung'unye pembeni yake; na kwa majani yake makubwa akaufunika mwili wake ili kumhifadhi na kumkinga na joto la jua na vilevile kuitibu na kuiponya ngozi yake. Na hivyo ndivyo Nabii Yunus alivyookoka kwa tadbiri ya Mola. Alianza kidogo kidogo kupata nafuu mpaka akawa tayari kwa safari ya kurejea kwa watu wa kaumu yake. Wakati alipowasili kwenye mji wake alistaajabu kuwaona watu walewale waliokuwa washirikina na waabudu masanamu, takribani wote wanamwabudu Mwenyezi Mungu; na adhabu iliyokuwa iwafike haikuteremshwa na badala yake Allah SW amewapa muhula wa kuendelea kuishi maisha yao ya kawaida hadi mwisho wa uhai wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kaumu ya Nabii Yunus ilirehemewa na Allah kutokana na kutubia na kumwamini Mola, kama ambavyo dua na tasbihi alizoleta Nabii Yunus zilimsaidia na kumwezesha kupata auni na msaada wa Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tusivunjike moyo hata chembe na kuwasusia wafanya maovu kwa kuhisi kwamba hawawezi kuacha mabaya na kutubia. Kwani si hasha wakazinduka, wakabadilika ghafla moja na kutubia kwa Mola.  Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kutubia kwa makosa yaliyopita, kunamwandalia mtu neema katika mustakabali wake. Kaumu ya Nabii Yunus ilitubia, na kwa sababu hiyo Allah akaiondolea adhabu na kuiteremshia neema. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 818 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atukubalie toba zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags