Feb 06, 2019 14:17 UTC
  • Ruwaza Njema (11)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu ya 11 ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambapo kwa leo tutazungumzia sifa njema ya Mtume Mtukufu (saw) ambaye ni mbora wa viumbe, ya kusamehe watu na kuwaongoza kwenye heri kuu, hata tunapokuwa na uwezo wa kulipiza kisasi kwa mabaya waliyotufanyia.

Tumeamrishwa kufuata mfano mwema wa mja mwema huyu wa Mwenyezi Mungu ambaye ni bwana na kiongozi wa maadili mema ulimwenguni, kama anavyoashiria suala hilo Nabii mwenyewe wa Rehema (saw) katika Hadithi ambayo imepokelewa katika kitabu cha al-Kafi ambapo anasema: 'Je, nikuonyesheni akhlaki iliyo bora zaidi duniani na Alhera? Wakasema: Ndio, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume (saw) akasema: Kuwa (dumisha) na uhusiano na aliyekata uhusiano nawe, mpe aliyekunyima na msamehe aliyekudhulumu.'

Sifa na akhlaki hii adhimu na ya kuvutia ya al-Habib al-Mustafa iling'ara sana ambapo kwa leo tutajaribu kuizungumzia kwa kifupi katika kipindi hiki, hivyo kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi.

Sheikh al-Kuleini amenukuu katika kitabu chake cha al-Kafi Hadithi moja kupitia Imam al-Baqir (as) kwamba alisema: 'Wakati walipomleta mbele ya Mtume (saw) yule mwanamke aliyekuwa ametia sumu katika nyama ya kondoo kwa ajili ya kumdhuru, Mtume (saw) alimuuliza: Ni kwa nini ulifanya kitendo hiki? Yule mwanamke alimjibu: Kama ni Nabii basi sumu hii haitamdhuru na kama ni mfalme (tu anayedai unabii) basi nitakuwa nimewaondolea watu shari inayotokana naye….. Hapo Mtume (saw) akamsamehe.'

Na imepokelewa katika kitabu hichohicho cha al-Kafi kupitia Imam Baqir (as) kwamba Mtume (saw) alipoingia mjini Makka katika siku ya kukombolewa kwake, aliufungua mlango wa al-Kaaba na kuamuru masanamu yote yaliyokuwa humo yavunjwe na kisha baada ya kushukuru na kumhimidi Mwenyezi Mungu kutokaa na msaada wake huo mkubwa aliwauliza maadui wake walitarajia nini kutoka kwake baada ya kutesa na kumuudhi yeye na wafuasi wake kwa miaka mingi. Maadui hao wakajibu kwamba hawakutarajia chochote kutoka kwake ila huruma na msamaha kwa sababu alikuwa mwingi wa huruma na msamaha. Hivyo Mtume akawasamehe wote na kuwaachilia huru.

Ni wazi kuwa kujipamba kwa sifa hizo nzuri na za kuvutia kimaadili ni moja ya sababu za kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu ambapo kukithirisha maombi ya kutaka msaada huo ni miongoni mwa misingi muhimu ya akhlaki za Mtume Mtukufu (saw). Imepokelewa katika kitabu cha Aamali cha Sheikh Tusi kupitia Fatwimat az- Zahra (as) kwamba alisema: 'Kila mara Mtume (saw) alipoingia msikitini, alikuwa akimswalia Mtume (saw) na kusema: Allahumma nighufirie dhambi zangu na nifungulie milango ya rehema, na alipotoka msikitini, alimswalia Mtume (saw) na kusema: Allahumma nighufirie dhambi zangu na unifingulie milango ya fadhila zako.'

Msikiti wa Mtume Muhammad SAW mjini Madina

 

Yazid Kanasi anamnukuu Imam Baqir (as) katika Hadithi iliyopokelewa katika kitabu cha al-Kafi akielezea kisa kimoja cha Mtume Mtukufu (saw) kwamba kabla ya kudhihiri Uislamu yaani katika zama za ujahilia, Mtume alielekea katika mji wa Taif huko Hijaz na kuingia katika nyumba ya mmoja wa wakazi wa mji huo. Mwenyeji wake alimkaribisha na kumkirimu kwa wema Mtume (saw). Mtume alipobaathiwa na kupewa utume na Mwenyezi Mungu, watu walimwendea mtu huyo na kumuuliza: 'Je, unajua Mtume aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu ni nani? Akajibu: 'La'. Wakamwambia: 'Yeye ni Muhammad bin Abdullah, yatima wa Abu Talib na ni yuleyule ambaye siku na tarehe fulani alikuja Taif na kuingia nyumbani kwako ambapo limkaribisha na kumkirimu vizuri.' Baada ya mtu huyo kufahamu hilo aliamua kwenda kwa Mtume (saw) na alipofika huko alimsalimu na kisha kusilimu. Alimuuliza Mtume (saw): 'Je, unanifahamu?' Mtume (saw) akamuuliza: 'Wewe ni nani?' Akajibu: 'Mimi ni mmiliki wa ile nyumba uliyoingia ulipofika Taifa siku fulani katika zama za ujahili, ambapo nilikukaribisha na kukukirimu'. Mtume (saw) akamwambia: 'Karibu sana, sasa unaweza kusema haja yako.' Akasema: 'Ninaomba kupewa kondoo mia mbili wakiwa na wachungaji wake.' Mtume (saw) aliamuru atimiziwe haja yake hiyo na kisha akawaambia masahaba zake: 'Laiti mtu huyu angeniomba haja kama ile aliyoiomba bibi kizee wa Bani Israel kutoka kwa Nabii Musa (as)!' Masahaba wakamuuliza: 'Je, ni haja gani hiyo aliyoiomba bibi kizee huyo wa Bani Israel kutoka kwa Nabii Musa?' Akajibu: 'Kabla ya Musa kuondoka Misri kuelekea ardhi takatifu ya Sham, Mwenyezi Mungu alimteremshia Wahyi akimtaka aifukue mifupa ya Nabii Yusuf (as) na kwenda nayo katika ardhi hiyo takatifu. Ili kutekeleza jukumu hilo, Musa alianza kutafuta kaburi la Yusuf na kuulizia sehemu lilikokuwa. Mzee mmoja alifika mbele yake na kumwambia: Hakuna mtu yoyote anayefahamu sehemu lililoko kaburi la Yusuf isipokuwa bibi kizee mmoja. Nabii Musa (as) aliagiza bibi huyo aitwe na alipofika alimuuliza: 'Je, unajua sehemu liliko kaburi la Yusuf?' Akajibu: 'Ndio.' Akamuuliza: 'Je, utanionyesha sehemu hiyo ili nami nikupe kila utakachotaka?!' Bibi kizee akasema: 'Sitakuonyesha sehemu ya kaburi hilo hadi uahidi kunipa nitakachotaka mimi (na sio wewe).' Musa akasema: 'Ninaahidi kukupa Pepo.' Bibi kizee akasema: 'La! Unapasa kuahidi kunipa nitakachotaka mimi.' Mwenyezi Mungu akamteremshia Wahyi Nabii Musa (as) akimwambia: 'Usione ugumu kumpa anachotaka yeye.' Musa akamwambia: 'Sawa, sema chochote unachotaka nami nitakupa.' Bibi kizee yule akasema: 'Takwa langu kwako ni kuwa Siku ya Kiama na kwenye Pepo, niwe katika daraja moja (sehemu moja) na wewe! Hapo Mtume Mtukufu (saw) akasema: 'Laiti mtu huyu angeliniomba ombi kama lile aliloliomba bibi kizee yule wa Bani Israel (kutoka kwa Nabii Musa (as)).

Tunamwomba Mwenyezi Mungu atupe sote wasikilizaji wapenzi, taufiki ya kuwa pembeni ya Mtume Mtukufu (saw) Peponi kwa baraka za kufuata na kutekeleza kivitendo tabia na maadili yake mema.

Tunakushukuruni nyote wasikilizaji wapenzi kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho kimekujieni moja kwa moja kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, kwaherini.

 

Tags