Feb 06, 2019 14:22 UTC
  • Ruwaza Njema (12)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran na karibuni kusikiliza sehemu ya 12 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Ruwaza Njema.

Katika kipindi cha juma hili tutazungumzia unyenyekevu wa Mtume Mtukufu (saw) kwa Mwenyezi Mungu, Subhanahu wa Taala na waja wake, muamala mzuri na huruma yake kwao na vilevile kukubali mwaliko na zawadi zao, jambo ambalo bila shaka ni katika maadili mema na alama ya wazi ya ukarimu na heshima kwao, na vilevile kuwafurahisha, suala ambalo ni katika mambo yanayomridhisha sana Mwenyezi Mungu. Kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi.

*******

Sheikh Swaduq (MA) ananukuu Riwaya ifuatayo kutoka kwa Imam Swadiq (as) kwamba alisema: 'Mtu mmoja alifika mbele ya Mtume (saw) na kuona nguo yake (Mtume) ikiwa imechakaa. Alimpa dirhamu 12 ili apate kununua nguo mpya. Mtume (saw) akasema: Ewe Ali! Chukua dirhamu hizi uninunulie nguo nipate kuvaa. Imam Ali (as) akasema: Nilienda sokoni na kununua nguo ya dirhamu 12 na kumletea Mtume (saw). Mtume aliitazama na kusema: Ewe Ali! Nitafurahi iwapo utaniletea nguo nyingine isiyokuwa hii. Je, unadhani aliyekuuzia atakubali kuichukua? Nilisema: Sijui. Akasema: Nenda uone itakuaje. Nilienda kwa muuzaji na kumwambia: Mtume wa Mwenyezi Mungu haipendi nguo hii, bali anataka nyingine, hivyo ichukue tafadhali. Muuzaji alinirejeshea zile dirhamu nami nikazirejesha kwa Mtume (saw). Mtume aliandamana na Ali (as) kwenda sokoni ili kununua nguo nyingine. Wakiwa njiani walikutana na mjakazi mmoja ambaye alikuwa ameketi kando ya barabara huku akiwa analia. Mtume alimuuliza: Kuna nini? Binti yule akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Familia yangu ilinipa dirhamu nne ninunue kitu lakini zimepotea hivyo naogopa kurudi nyumbani. Mtume (saw) alimpa dirhamu nne na kumwambi arejee nyumbani. Kisha Mtume (saw) alienda sokoni na kununua shati kwa dirhamu nne na kisha kulivaa na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hilo. Aliondoka sokoni kurejea nyumbani. Alimwona mtu asiyekuwa na nguo ambaye alikuwa akisema: Mtu atakayenivisha Mwenyezi Mungu atamvisha vazi la peponi. Hapo, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akavua nguo aliyokuwa amenunua na kuivaa punde kidogo na kumvisha mwombaji huyo. Kisha akarejea sokoni na kununua shati jingine kwa zile dirhamu nne zilizokuwa zimebaki, akalivaa, akamshukuru Mwenyezi Mungu na kurejea nyumbani kwake. Akiwa njiani, alimwona yuleyule mjakazi akiwa ameketi njiani huku akiwa analia. Alimuuliza: Ni kwa nini haurejei nyumbani? Akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw)! Nimechelewa, hivyo naogopa kupigwa. Mtume (saw) akasema: Tangulia, twende unionyesha nyumba yenu. Waliandamana hadi Mtume (saw) alipofika mbele ya mlango wa nyumba yao, alisimama na kusema: Salamu ziwe kwenu enyi wenye nyumba! Lakini hakupata jibu lolote kutoka kwenye nyumba hiyo. Mtume (saw) alitoa tena salamu lakini hakupata jibu lolote kama ilivyokuwa mara ya kwanza. Alitoa salamu kwa mara ya tatu na hapo ndipo akajibiwa na watu wa nyumba hiyo waliosema: Salamu, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mtume (saw) akawauliza: Ni kwa nini hamkutoa jibu nilipokusalimuni mara ya kwanza na ya pili? Wakajibu: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tulisikia salamu zako lakini tulipendelea tuendelee kuzisikia kutoka kwako! Mtume (saw) akasema:  Mjakazi huyo amekuja nyumbani kwa kuchelewa, msimkaripie (msimuadhibu). Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tumemwachilia huru kwa baraka za kuja kwako kwetu. Hapo Mtume akasema: Ninamshukuru Mwenyezi Mungu. Nilikuwa sijawahi kuona dirhamu zenye baraka kubwa kama dirhamu hizi 12. Kupitia dirhamu hizi Mwenyezi Mungu ameweza kuwavisha watu wawili waliokuwa hawana nguo na kumwachilia huru mtu mwingine.'

Bwana Mtume Muhammad SAW ameleta mshikamano baina ya watu wa matabaka yote duniani

 

Ndugu wasikilizaji, Sheikh al-Barqi amenukuu katika kitabu chake cha al-Mahasin naye Sheikh Kuleini katika kitabu chake cha al-Kafi, wakimnukuu Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba alisema: 'Iwapo nitaalikwa na muumini kula hata mguu wa kondoo, nitaitikia mwaliko wake na hilo ni katika dini, na iwapo mushrik au mnafiki atanialika kula nyama ya ngamia mzima, sitaukubali mwaliko huo na hilo ni katika dini. Mwenyezi Mungu ameniharamishia mimi kupokea zawadi au kula chakula cha mushrikina na wanafiki.'

Wanazuoni wawili hawa vilevile wamenukuu Hadithi kutoka kwa Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) ambapo anasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: 'Ninamuusia aliyeko na asiyekuwepo hivi sasa katika umma wangu, aitikie mwaliko wa Mwislamu hata kama atakuwa umbali wa maili tano kwa sababu hilo ni katika dini.'

***********

Ndugu wasikilizaji na anatunukulia Imam Swadiq (as) mfano mwingine wa sifa na tabia nzuri na za kuvutia za Mtume Mtukufu (saw) ambaye ni mbora wa tabia njema kati ya viumbe na wanadamu wote. Amepokelewa katika kitabu cha al-Kafi akisema: 'Katika zama za ujahili, Waarabu walikuwa katika makundi mawili, Hilli na Hums. Hums walikuwa ni Qureish na Hilli walikuwa makabila (koo) mengine ya Waarabu. Kila mtu Katika kabila la Hilli alipasa kupata hifadhi (kumkimbilia) kutoka kwa mtu wa kabila la Hums ili ampe nguo ya kufanyia tawafu, la sivyo alilazimika kufanya tawafu akiwa uchi. Mtume (saw) alikuwa mwenyeji wa Ayyadh bin Hummar Majashii', mtu aliyekuwa na heshima kubwa na katika zama hizo za ujahili alikuwa kadhi wa watu wa Ukadh. Kila alipokuwa akiingia Makka alikuwa akivua nguo zake zilizajaa dhambi na uchafu na kuvaa za Mtume (saw) kwa sababu zilikuwa safi na takatifu na kwenda nazo kufanya tawaf na kisha kuzirejesha kwa Mtume (saw). Wakati Mtume (saw) alipobaathiwa na kupewa Utume na Mwenyezi Mungu, Ayyadh alimletea Mtume (saw) zawadi lakini Mtume hakuipokea na kumwambia: Ewe Ayyadh! Iwapo utakuwa Mwislamu nitaipokea zawadi yako. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameniharamishia kupokea zawadi kutoka kwa mushrikina (watu wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu). Baada ya hapo Ayyadh alisilimu na kuboresha Uislamu wake na kisha kumletea Mtume (saw) zawadi naye akaipokea.'

***********

Na kufikai hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu kwa leo ambapo tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi hiki ambacho kimekujieni kutoka mjini Tehran kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi wa Barakatuh.

 

Tags