Jumamosi, 02, Machi, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe 24 Mfunguo Tisa Jamadithani 1440 Hijria sawa na tarehe Pili Machi 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 896 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Ahmad Bin Ali Baihaqi Sabzavari, mmoja wa maulama wakubwa wa elimu ya Qur’ani wa mjini Neishabur. Ali Baihaqi Sabzavari alitabahari katika elimu ya fasihi lugha ya Kiarabu kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake na vilevile katika tafsiri ya Qur’an Tukufu. Msomi huyo wa Kiislamu pia alikuwa mahiri katika qiraa ya Qur’an Tukufu. Ali Baihaqi Sabzavari ameandika vitabu mbalimbali vikiwemo vile vya ‘Taajul-Maswadir’ ‘Al-Muhit bi Ilmilil Qur’an.’***
Miaka 824 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria aliaga dunia Yahya bin Qassim Tha'alabi aliyejulikana kwa lakabu ya Abu Zakaria mwanafasihi na mshairi mtajika wa Kiarabu. Alibobea pia katika fikihi, lugha na tafsiri ya Qur'ani na kuondokea kuwa mmoja wa wasomi na wanazuoni mahiri katika zama zake. Kwa miaka mingi Abu Zakariya alikuwa akifundisha katika Chuo cha Nidhamiya mjini Baghdad. Alimu huyo ameacha pia athari za vitabu ikiweni diwani mashairi. ***
Katika siku kama ya leo miaka 123 iliyopita mwanafizikia wa Kifaransa Henri Becquerel alivumbua mionzi ya nunurishi yaani radioactive. Henri alifikia mafanikio hayo baada ya kufanya tafiti katika mada za urani na vitu vinginevyo. Becquerel alikuwa akichunguza urani ndipo alipogundua mionzi hiyo. Utafiti wa mwanafizikia huyo wa Kifaransa ulimfanya atunukiwe tunzo ya amani ya Nobel mwaka 1903 na miaka mitano baadae aliaga dunia.***
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, nchi ya Morocco ilipata uhuru. Morocco iko kaskazini mwa Afrika katika Ukingo wa Bahari ya Mediterranean na Bahari ya Atlantic na inapakana na Algeria na Sahara Magharibi. Ukoloni wa madola ya Ulaya dhidi ya nchi hiyo, ulianza tangu karne ya 15 Miladia. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Morocco dhidi ya wakoloni wa Uhispania na Ufaransa yalipelekea nchi hiyo kupata uhuru wake mwaka 1956. ***
Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Chama cha Wananchi cha Rastakhiz au Rastakhiz Party of People kiliasisiwa nchini Iran kwa amri wa Muhammad Reza mfalme wa mwisho wa ukoo wa Kipahlavi. Kwa muktadha huo, Iran ikawa imebadilika rasmi na kuwa nchi ya chama kimoja na baadhi ya vyama vichache vilivyokuwa vikifanya harakati zao chini ya utawala huo wa kifalme vikavunjwa. Chama cha Rastakhiz kikawa wenzo wa Mfalme kwa ajili ya kufikia malengo yake haramu hususan katika kuimarisha udikteta wake na kudhibiti zaidi wananchi kupitia uanachama wa chama hicho. Kutokana na upinzani wa wananchi , vibaraka wa utawala wa Kifalme walikuwa wakiwatisha wananchi na kuwalazimisha kuwa wanachama wa chama hicho na waliokuwa wakikataa kufanya hivyo walikuwa wakiandamwa na tuhuma za kuiuza nchi. Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye alikuwa uhamishoni alitoa ujumbe na kuwataka wananchi wa Iran kupinga udikteta wa chama cha Rastakhiz. Upinzani wa wananchi kwa chama cha Rastakhiz ulikuwa mkubwa kiasi kwamba, chama hicho hakikudumu isipokuwa miaka mitatu na nusu tu tangu kuanzishwa kwake na kikavunjwa kufuatia harakati za wananchi. ***
Na siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani, alimu, fakihi mkubwa na mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu ulimwenguni alifariki dunia. Alizaliwa mjini Golpayegan moja ya miji ya Iran na kusoma masomo ya dini kwa maustadhi stadi na waliokuwa wametabahari kielimu katika zama hizo akiwemo Ayatullah Hairi. Ayatullah Golpayegani alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Qum-Iran baada ya kuasisiwa kwake. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika nyuga mbalimbali. ***