Apr 10, 2016 12:24 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain 115

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi cha 115 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqaain ambavyo hukujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutoka hapa mjini Tehran. Katika miezi ya hivi karibuni tumekuwa tukijadili na kujibu maswali ya kiitikadi yanayohusiana na msingi wa Uimamu ambao ni moja ya misingi muhimu ya Uislamu.

Swali la kwanza ambalo tuliuliza katika kipindi kilichopita lilihusiana na maana ya Uimamu na tofauti iliyopo kati yake na Unabii. 

Aya ya 124 ya Surat al-Baqarah imetujibu swali hili kwa kutwambia kwamba nafasi ya Uimamu sio nafasi ya Unabii. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu aliahidi kumpa rafiki yake Nabii Ibrahim (as) Uimamu mwishoni mwa maisha yake baada ya kumfanya kuwa mja, Nabii, Mtume na rafiki yake. Kwa hivyo Uimamu ni agano la Mwenyezi Mungu ambalo humpa mja wake msafi na mtukufu ambaye hajawahi kuguswa na chembe ya udhalimu. Yaani agano na ahadi hii hupewa waja wema ambao ni maasumu na ambao hawatendi dhambi kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu. Hapa tunapasa kuuliza swali hili kwaba je, Uimamu ni nini? Karibuni kusikiliza jibu la swali hili muhimu.

************

Tunapozirejea aya za Qur'ani Tukufu tunaona kwamba zinazungumzia Uimamu kwa maana ya mwongozo kutoka kwa Mweyezi Mungu lakini sio mwongozo wa kawaida tunaoufahamu sisi bali ni mwongozo maalumu ambao unatajwa kuwa ni mwongozo unaopatikana kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya mbili za 72 na 73 za Surat al- Anbiyaa, baada ya kuzungumzia sehemu ya kisa cha Nabii Ibrahim (as): Naye tukampa Is-haq, na Yaaqub kuwa ni zawadi. Na wote tukawajaalia wawe ni watu wema. Na tukawafanya maimamu wakiongoza kwa amri yetu. Na tukawapa wahyi watende kheri, na wasimamishe Swala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.

Kwa hivyo jambo muhimu hapa kuhusiana na wanaopewa Uimamu na Mwenyezi Mungu ni kuwa mwongozo huo hutokana na amri yake Yeye. Hivyo basi nini maana ya mwongozo unaotokana na amri ya Mwenyezi Mungu?

Swali hili limejibiwa na Qur'ani yenyewe inapotubainishia kwamba amri ya Mwenyezi Mungu ni irada yake ya dhati ambayo kitu chochote hakiwezi kuzuia kuthibiti kwake kama zinavyoashiria ukweli huo aya za 82 na 83 za Surat Yasin zinazosema: Hakika amri yake anapotaka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa. Basi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa.

Na hapa ndipo inapobainika wazi tofauti iliyopo kati ya Unabii na Uimamu na baina ya mwongozo mkuu au jumla na mwongozo maalumu na mahususi. Maelezo zaidi kuhusiana na suala hili yatakujieni hivi punde kwa hivyo endeleeni kuwa nasi ili tupate kunufaika kwa pamoja na maelezo hayo.

***********

Wapenzi wasikilizaji, tunapozingatia aya za Qur'ani Tukufu tunaona kwamba zinabainisha wazi kwamba Mwenyezi Mungu aliwatuma Manabii ili wapate kubashiri na kuwaonya watu. Kwa msingi huo jukumu kuu la Manabii ni kutoa mwongozo jumla kwa maana ya kuonyesha njia na kuwaongoza watu kwenye njia hiyo pamoja na kubainisha hukumu zake. Kwa hivyo wao huwa wanawabainishia watu irada na matakwa ya kisheria ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya nne ya Surat Ibrahim: Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa kaumu yake ili apate kuwabainishia. Basi Mwenyezi Mungu humuacha akapotea amtakaye, na akamwongoza amtakaye. Naye ni Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.

Ama jukumu la Uimamu sio kutekeleza mwongozo huu jumla tu bali ni kushika mikono ya watu na kuwasaidia kufikia haki na mwongozo wa Mwenyezi Mungu, na hilo ndilo jambo linalotajwa kwenye Qur'ani Tukufu kwa ibara ya 'amri ya mbinguni.' Hii ndiyo maana anayoibainisha Allama Tabatabai katika Tafsiri yake ya al Mizaan katika kufasiri kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema Hakika Mimi nimekufanya Imam wa watu.

*************

Ndugu wasikilizaji tofauti hii iliyopo kati ya Unabii na Uimamu imebainishwa pia katika aya kadhaa za Qur'ani Tukufu ambapo Mwenyezi Mungu anamuhutubu Mtume wake (saw) katika aya ya 7 ya Surat ar-Ra'd kwa kusema: Hakika wewe ni mwonyaji tu. Na kila kaumu ina wa kuwaongoza. Imepokelewa katika Tafiri ya Maj'maul Bayaan kupitia Ibn Abbas kwamba alisema: 'Aya hii ilipoteremka Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema: 'Mimi ndiye mwonyaji na Ali ndiye mwongozaji baada yangu. Ewe Ali! Kupitia kwako wataongoka waongofu.'

Imepokelewa katika kitabu cha Ikmal ad-Deen na Baswair ad-Darajaat kwamba Imam Baqir (as) alisema katika kufasiri aya hii: 'Mwonyaji ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na Ali ni mwongozaji. Katika kila zama kuna Imam kutoka miongoni mwetu anayewaongoza katika yale aliyoyaleta Mtume (saw).'

Na Imam Baqir amepokelewa katika hadithi nyingine iliyonukuliwa katika vitabu vya al-Ghaiba cha Sheikh an-Nu'mani na Baswair ad-Darajaat cha Swaffar na vinginevyo katika kufasiri aya hii tukufu kwamba: 'Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ndiye mwonyoji naye Ali ni mwongozaji. Wallahi! Aya hii haijatoweka kutoka kwetu na itaendelea kuwa miongoni mwetu hadi Siku ya Kiama.'

Na hapa wapenzi wasikilizaji inabainika tofauti nyingine iliyopo baina ya Unabii na Uimamu nayo ni kwamba Unabii ulikamilika na kufikia kikomo kwa Mtume Mtukufu (saw) lakini Uimamu utaendelea kuwepo hadi Siku ya Kiama kwa sababu kila kaumu ina mwongozaji.

***********

Na muhtasari wa mambo tuliyojifunza katika kipindi cha leo ni kwamba Uimamu ni cheo muhimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambapo jukumu lake kuu na la kwanza ni kuwaongoza wanadamu kwa irada yake Muumba. Hii ina maana kuwa Imam huwaongoza wanadamu kwa kuwashika mkono ili kuwafikisha kwenye haki kwa amri yake Mwenyezi Mungu, na uongozi huu utaendelea kuwepo hadi Siku ya Kiama.

Na kwa muhtasari huu wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kimekujieni moja kwa moja kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote huku tukikutakieni usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vilivyosalia. Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.