Apr 09, 2019 04:26 UTC
  • Jumanne, 9 Aprili, 2019

Leo ni Jumanne tarehe Tatu Sha'aban 1440 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 9 Aprili 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib (as) mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). Kipindi bora cha maisha ya Imam Hussein (as) ni cha miaka sita wakati mtukufu huyo alipokuwa pamoja na Mtume Mtukufu wa Uislamu. Imam Hussein (as) alijifunza maadili mema na maarifa juu ya kumjua Mwenyezi Mungu kutoka kwa baba yake Imam Ali (as) na mama yake Bi Fatimatul-Zahra (as), ambao walilelewa na Mtume Mtukufu. Imam Hussein alishiriki vilivyo katika matukio mbalimbali wakati Uislamu ulipokabiliwa na hatari. Daima alilinda turathi za thamani kubwa za Mtume kwa kutoa darsa na mafunzo kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kiitikadi, kifikra na kisiasa. Imam Hussein (as) alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu mwaka 50 Hijria, baada ya kuuawa shahidi kaka yake yaani Imam Hassan bin Ali bin Abi Talib (as). Hatimaye Imam Hussein (as) aliuawa shahidi huko Karbala, Iraq mwaka 61 Hijria wakati akitetea dini tukufu ya Kiislamu. ***

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, magaidi wa utawala ghasibu wa Israel walifanya mauaji ya kinyama katika kijiji cha Deir Yassin huko magharibi mwa Baitul Muqaddas. Mauaji ya umati dhidi ya wakazi wa kijiji cha Dier Yasin ambacho kilikuwa na watu karibu mianne yalifanywa njia ya kuasisi dola la Kiyahudi katika ardhi ya Wapalestina. Mauaji hayo yaliongozwa na makundi matatu ya kigaidi ya Wayahudi ambayo ni Irgun la Menachem Begin, Haganah la David Ben-Gurion na Stern Gang lililokuwa likiongozwa na Isaac Shamir. Eneo la Dier Yassin lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Wazayuni kutokana na kuwa katika njia ya Baitul Muqaddas na karibu na pwani. Baada ya kukivamia kijiji cha Deir Yassin, Wazayuni hao waliwaua kinyama wakazi wake ambao hawakuwa na hatia yoyote. Mauaji hayo yaliwalazimisha Wapalestina wengi wa eneo hilo kukimbia makazi yao kwa kuhofia kukaririwa mauaji kama hayo ya kinyama. ***

Mauaji ya umati ya Wazayuni huko Deir Yyassin

Tarehe 9 Aprili miaka 27 iliyopita Waserbia wa Bosnia waliokuwa wakiungwa mkono na kusaidiwa na dikteta wa zamani wa Yugoslavia Slobodan Milosevic, walianza mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo katika mji wa Belgrade. Mauaji hayo yalianza baada ya kutangazwa matokeo ya kura ya maoni hapo tarehe Mosi Machi 1992 ambayo kwa mujibu wake asilimia 99 ya washiriki walipiga kura ya kujitenga Bosnia Herzegovina na Yugoslavia ya zamani. Hata hivyo Waserbia wachache wa Bosnia walipinga suala hilo la kuanzisha uasi kisha baadaye wakajitangazia mamlaka ya Seribia katika maeneo yao. Milosevic aliwaunga mkono Waserbia na kuanzisha vita vikubwa zaidi vya mauaji ya kimbari barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Hadi vita hivyo vinamalizika mwaka 1995 zaidi ya Waislamu laki moja wa Bosnia walikuwa wameuawa kwa umati. Zaidi ya Waislamu wengine milioni mbili pia walilazimika kuwa wakimbizi. ***

Slobodan Milosevic

Na miaka 13 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Farvardin 1386 ilipewa jina la Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia nchini Iran baada ya kutangazwa habari ya mafanikio makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika teknolojia ya nyuklia na kurutubisha madini ya urani kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Wasomi na wataalamu wa Iran walifanikiwa kukamilisha mfumo wa kuzalisha nishati ya nyuklia licha ya mbinyo na vikwazo vya nchi za kibeberu. Kwa utaratibu huo Iran iliingia katika kundi la nchi zenye teknolojia ya nyuklia duniani. Mwaka mmoja baadaye Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kuzalisha nishati hiyo viwandani. Mafanikio hayo makubwa ya Iran yalipatikana chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na licha ya vikwazo vya nchi za Magharibi. ***

Siku ya Taifa ya Nyuklia nchini Iran

 

Tags