Jumapili, Aprili 14, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 8 Sha’aban 1440 Hijria, sawa na 13 Aprili 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 893 iliyopita alizaliwa Ibn Rushd, mwanafalsafa na mwanafikra maarufu wa Waislamu mjini Andalusia (sehemu ya Uhispania ya sasa). Baba na babu wa Ibn Rushd, wote walikuwa makadhi mjini Andalusia. Akiwa kijana alipata kusoma elimu mbalimbali za zama zake, huku akitabahari zaidi katika elimu za hisabati, sayansi ya elimu asilia, nyota, mantiki, falsafa na udaktari. Kufuatia hali hiyo alipewa kipaumbele na watawala wa silsila ya Muwahhidun ambao walikuwa wakiitawala Andalusia wakati huo, kiasi cha kufikia kuteuliwa kuwa kadhi wa mji wa Córdoba, mji mkuu wa Andalusia. Hata hivyo mwishoni mwa umri wake alichukiwa na watawala na hatimaye akabaidishwa. Mielekeo ya Ibn Rushd ilielemea sana kwenye fikra za Aristotle. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na ‘Tahaafut al-Tuhafat’ ‘Kitabul-Kulliyyaat’ na ‘Faslul-Maqaala.’ Ibn Rushd alifariki dunia Disemba, 1198 Miladia sawa na mwezi Swafar 595 Hijiria.
Siku kama ya leo miaka 879 alizaliwa Ibn Rumiyya mpokezi wa hadithi, mtaalamu wa mimea na dawa wa Kiislamu wa karne ya sita Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Rumiyya alijifunza hadithi kutoka kwa wasomi na wapokezi hadithi wakubwa wa zama hizo na kujifunza pia elimu ya utaalamu wa mimea sambamba na elimu ya dini. Akiwa Andalusia, Ibn Rumiyya awali alianza kuchunguza na kutambua sifa za mitishamba na baadae alifanya safari katika nchi mbalimbali kama Misri, Iraq na Hijaz. Alijishughulisha na masuala ya utafiti wa mitishamba akiwa huko bila kusahau na kujifunza hadithi. Ibn Rumiyya aliandika vitabu vingi kuhusu mitishamba, fiqih na hadithi, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya vitabu hivyo vimepotea.

Siku kama ya leo miaka 173 iliyopita alizaliwa Friedrich Carl Andreas, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na Iran huko nchini Ujerumani. Baada ya kufahamiana na mtaalamu mmoja wa masuala ya mashariki wa nchini Denmark, alivutiwa sana na utamaduni wa Iran ambapo alianza kufanya utafiti kwa kipindi cha miaka minne katika uwanja huo. Katika kukamilisha masomo yake aliamua kutembelea nchi za Iran na India sambamba na kujifunza lugha ya Kifarsi. Kwa karibu kipindi cha miaka 30 alikuwa mwalimu wa lugha ya Kifarsi katika Chuo Kikuu cha Göttingen nchini Ujerumani ambapo wanafunzi wake walipata kufahamu tamaduni za thamani za Iran. Mtaalamu huyo wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ujerumani alifariki dunia mwaka 1930 Miladia.
Siku kama ya leo sawa na tarehe 25 Farvardin miaka 31 iliyopita serikali ya wakati huo ya Iraq ilikiri waziwazi kwamba ilitumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi chote cha miaka minane ya vita hivyo Iran iliwasilisha mashtaka katika jumuiya za kimataifa kwamba Iraq inatumia silaha za kemikali dhidi ya wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu. Wakati huo Iraq haikukiri wala kukadhibisha habari hiyo. Hata hivyo katika siku kama hii ya leo wakati vita vilipokuwa vimepamba moto, serikali ya Baghdad ilikiri kwamba inatumia silaha za kemikali zikiwemo za gesi ya sumu na hatari ya haradali dhidi ya malengo ya kijeshi na kiraia ya Iran. Takwimu zimeonesha kwamba utawala wa Baath wa Iraq ulifanya mashambulizi 3,500 kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha vita hivyo.
Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, Hugo Chavez rais wa zamani wa Venezuela alirejea nchini kwake na kushika hatamu za uongozi baada ya kufeli jaribio la mapinduzi ya kumuondoa madarakani. Chavez Aliingia madarakani mwaka 1999 na kufanya mabadiliko makubwa kwa maslahi ya tabaka la chini. Vilevile alichukua hatua za kusimamia mashirika ya mafuta ya Kimarekani yaliyokuwa yakichimba mafuta ya nchi hiyo. Siasa za kujitegemea za Chavez ziliikasirisha sana Washington. Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana Marekani ilipanga na kuratibu mapinduzi mnamo tarehe 12 Machi mwaka 2002. Licha ya mapinduzi hayo kupata mafanikio katika hatua za awali, lakini wananchi wa Venezuela waliokuwa wameridhishwa na mabadiliko ya Chavez, walipinga uingiliaji wa nchi za nje katika masuala ya ndani ya nchi yao. Hugo Chavez alifariki dunia Machi 5 mwaka 2013 kutokana na maradhi ya saratani akiwa na umri wa miaka 58.