Apr 29, 2019 00:59 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Apr 29

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.....

Iran yatwaa ubingwa wa Mieleka Asia

Wanamieleka shupavu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametwaa ubingwa wa Mashindano ya Ubingwa wa Milekea ya Asia ya Xi'an nchini China, baada ya kuzoa medali lukuki. Iran ilitawazwa mshindi katika mashindano hayo ya kikanda siku ya Jumatano, baada ya kuchota alama 220, na medali kochokocho zikiwemo saba za dhahabu. Katika siku ya kwanza ya mashindano hayo, wanamieleka wa Iran walizoa medali dhahabu tatu na shaba mbili. Jumatano ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya mashindano hayo, wanamieleka wa Iran walizoa medali nne za dhahabu na moja ya fedha katika kategoria mieleka ya Freesstyle (ya kujiachia). Kila mara mwanamieleka wa Iran alipotwaa dhahabu, wimbo wa taifa wa Iran ulihinikiza katika ukumbi huo wa michezo nchini China. India imeibuka ya pili kwa alama 155, huku Kazakhstan ikifunga orodha ya tatu bora kwa kuchota alama 129.

Wanamieleka wa Iran

 

Hii ni mara ya 26 kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Ubingwa wa Milekea ya Asia ya Xi'an. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei amewaongoza maafisa wa ngazi za juu serikali katika kutuma salamu za tahania kwa wanamieleka hao wa Kiirani. Katika ujumbe wake wa siku ya Alkhamisi, Ayatullah Khemenei amewapongeza wanamieleka wa Iran kwa kuipaisha na kuipeperusha bendera ya Jamhuri ya Kiislamu katika mashindano hayo ya kikanda nchini China. Mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka tokea mwaka 1979 huwa yanaandaliwa na Kamati Shirikishi ya Mieleka Asia (AAWC).

Wairani walioshinda medali za dhahabu ni Reza Atri baada ya kumkarana bla mafuta Kang Kumsong wa Korea Kusini kwa alama 9-3 katika safu ya kilo 57, Behnam Ehsanpour kwa kumdondosha Mchina LIU Minghu kwa alama 2-1 katika kitendo cha kilo 61, Bahman Teymouri kwa kumzidi nguvu na maarifa Parveen RANA wa India kwa alama 3-0 katika kategoria ya kilo 79, Kamran Ghasempour kwa ku,mpeleka mchakamchaka raia wa Kygyzystan, Aligarizhi GAMIDGADZHIEV kwa alama 10-0 katika safu ya kilo 86. Dhahabu ya tano ya Iran ilitwaliwa na Alireza Karimi baada ya kumshinda raia wa India Viky Viky kwa alama 11-0 katika mieleka ya wenye kilo 92, huku Reza Yazdani akiipa Iran dhahabu ya sita kwa kumchachafya Batzul ULZIISAIKHAN wa Mongolia kwa ponti 7-4 katika kategoria ya kilo 97 na dhahabu ya mwisho ya Iran ilitiwa mkononi na Yadollah Mohebbi baada ya kumdondosha Deng Zhiwei wa China kwa alama 2-1 katika safu ya kilo 125. Medali za shaba za Iran zilitwaliwa na Peyman Biabani (65kg), Younes Emami (70kg) na Mohammad Nokhodi (74kg).

Voliboli; Klabu ya Shahrdari Varamin ya Iran mabingwa wa Asian

Klabu ya Shahrdari Varamin ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiye bingwa wa Mashindano ya Wanaume ya Vilabu Bingwa Barani Asia Mwaka 2019, baada ya kuifanya vibaya Panasonic Panthers ya Japan katika mpambano wa fainali siku ya Ijumaa. Katika mchezo huo uliopigwa katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taipei, klabu ya Iran ilitoka nyuma ikiwa na nakisi ya seti mbili, na kuitandika Panthers seti (25–20, 25–16, 22–25, 20–25, 14–16).

Wanavoliboli wa Shahrdari Varamin ya Iran

 

Mkufunzi wa Shahrdari Varamin ya Iran, Rahman Mohammadirad amepongeza ushindi huo kwa kusema kuwa, "Tuna faraha sana kwa kushinda mechi ya fainali. Tulishindwa na Panthers katika hatua za awali. Tunatumai kuwa balozi mwema wa Iran tutakapoliwakilisha bara Asia katika Mashindano ya Voliboli ya Klabu Bingwa Duniani baadaye mwaka huu, yatakayoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani FIVB.

Mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama Asian Men's Club Volleyball Championship, yanayofanyika kila mwaka na kuandaliwa na Shirikisho la Voliboli Asia kwa ushirikiano na Chama cha Voliboli cha Chinese Taipei (CTVA), yalianza Aprili 18 na kumalizika Aprili 26.

Baiskeli; Mwanamke wa Kiirani ashinda medali

Somayeh Yazdani ameingia katika madaftari ya kumbukumbu, baada ya kuwa mwanamke wa kwanza Muirani kulishindia taifa hili medani katika mashindano ya dunia ya uendeshaji baiskeli. Binti huyo wa Kiirani alitunukiwa medali ya shaba baada ya kuibuka mshindi wa tatu katika Mashindano ya Uendeshaji Baiskeli Barani Asia nchini Uzbekistan siku ya Jumamosi.

Somayeh Yazdani

 

Binti mwingine wa Kiirani aliyeshiriki mashindano hayo yanayojulikana kwa Kimombo kama Asian Road Cycling Championships, Mandana Dehqani, aliibuka wa 11. Mwanamke wa Kiuzbeki ameupa maana usemao mcheza kwao hutuzwa, kwa kutunikiwa medali ya dhahabu baada ya kuibuka mshindi, huku nafasi ya pili ikitwalia na raia wa Korea Kusini. Wanatakaofanikiwa katika mashindano haya ya kikanda watajikatia tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Tokyo mwaka ujao 2020.  

Cameroon bingwa wa Afcon U-17

Timu za taifa za soka za vijana za Guinea na Cameroon, siku ya Jumapili zilishuka dimbani kumenyana katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wasiozidi umri wa miaka 17. Fainali hiyo ilichezwa katika uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam nchini Tanzania, ambapo Cameroon iliishia kutwaa taji hilo la kibara. Timu ya taifa ya Cameroon imetwaa ubingwa wa fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 baada ya kuifunga Guinea kwa mikwaju ya penalti 5-3 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam Tanzania. Katika mchezo huo ambao ndio umekamilisha mashindano hayo, ulishuhudia timu hizo zikimaliza dakika 90 ya mchezo bila kufungana ndipo mikwaju ya penlati ilipotumika. Hii ni mara ya pili kwa Cameroon kutwaa ubingwa wa kombe hilo. Mchezaji wa Cameroon Steve Mvoue amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo. Guinea ilikuwa ya kwanza ya kufuzu baada kuifunga Nigeria mabao 10-9 kupitia mikwaju ya penalti, baada ya mechi hiyo kumalizika kwa sare ya 0-0 katika muda wa kawaida. Mambo yalikuwa vivyo hivyo kwa Cameroon, ambayo waliwashinda Angola mabao 5-4 pia kupitia mikwaju ya Penalti. Nigeria na Angola nazo, zitamenyana katika mechi ya kumtafuta mshindi wa tatu, siku ya Jumamosi. Licha ya kufika katika hatua hiyo, timu hizo nne zimefuzu kucheza fainali ya kombe la dunia kwa vijana nchini Brazil mwezi Oktoba. Mwaka 2017 wakati michuano hii ilipofanyika nchini Gabon, Guinea ilifika katika hatua ya nusu fainali, na kumaliza nafasi ya tatu. Cameroon nao, walifika katika hatua ya makundi mwaka 2017. Guinea haijawahi kushinda taji hili lakini mbali na mwaka 2017, mwaka 2015 na 1995 walimaliza katika nafasi hiyo. Cameroon ilitwaa taji hilo mara ya kwanza mwaka 2003, wakati fainali hiyo ilipofanyika katika Jamhuri ya Eswatini, huko nyuma ikifahamika kama Swaziland.

Riadha: Kenya yang'ara tena London Marathon

Mwanariadha nyota wa Kenya, Eliud Kipchoge ameandikisha rekodi mpya sambamba na kuingia katika madaftari ya kumbukumbu kwa kushinda mbio za London Marathon mara nne mtawalia. Kipchogfe ametetea ubingwa wake kwa kuweka rekodi ya aina yake akiwashinda wapinzani wake wa Uhabeshi kwa umbali wa karibu kilomita tatu. Katika mbio hizo za aina yake siku ya Jumapili, Kipchoge alitumia saa 2:02:37 na kuvunja rekodi yake mwenyewe aliyoweka mwaka 2016 katika mbio hizo kwa kutumia muda wa saa 2:03:05. Wanariadha kutoka Ethioipia Mosinet Geremew and Mule Wasihun wameshika nafasi ya pili na ya tatu. Mwaka wa jana Kipchoge alitajwa kuwa mwanariadha mashuhuri duniani. Mwanariadha bingwa wa Uingereza mwenye asili ya Ethiopia Mo Farah ambaye hivi karibuni ameingia kwenye mzozo na mwanariadha Haile Gebrselassie alimaliza katika nafasi ya tano. Kwa upande wa wanawake, mwanadada Brigid Kosgei mwenye umri wa miaka 25 amefanya maajabu baada ya kuwashinda wakubwa wake katika mashindano hayo baada ya kutumia 02:18:19 na kumshinda Mkenya mwenzake Vivian Cheruiyot aliyetumia 02:20:51 huku muethiopia Roza Dereje akikamata nafasi ya tatu kwa kutumia 02:20:51.

La Liga: Bercolona tena!

Klabu ya Barcelona imenyakua ubingwa wake wa 8 wa Ligi Kuu ya Soka ya Uhispania (La Liga) katika kipindi cha miaka 11 baada ya kuifunga Levante bao 1-0 kwenye mchezo wa Jumamosi. Barcelona usiku wa April 27 ilikabidhiwa rasmi taji lao la La Liga msimu wa 2018/2019, ikiwa ni taji lao la 26 la La Liga. Kiungo nyota Lionel Messi aliyetokea benchi katika kipindi cha pili alipachika bao la ushindi dakika ya 62 na kuifanya klabu hiyo kuwa bingwa mara 26 katika historia ya La Liga, ikiwa ni ya pili nyuma ya Real Madrid iliyonyakua ubingwa huo mara 33.

Lionel Messi

 

Na kwa kutamatisha, Shirikisho la Wachezaji wa Soka la Kulipwa nchini Uingereza (PFA) limemtangaza beki wa Liverpool Virgil van Dijk kuwa mshindi wa tuzo ya PFA kwa mwaka huu 2019, akimpiku Raheem Sterling wa Mancheser City ambaye alikuwa ametajwa kuwa n nafasi kubwa zaidi ya kutwaa tuzo hiyo. Dijk alitunukiwa tuzo hiyo katika hafla itayofanyika jijini London Uingereza siku ya Jumapili Aprili 28.

Mchezaji bora wa msimu uliopita Muhammed Salah raia wa Misri anayechezea Liverpool msimu huu sio miongoni mwa wanaowania tuzo hiyo.

……………………TAMATI.………………