May 10, 2019 21:44 UTC
  • Jumamosi, 11 Mei, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 5 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1440 Hijria sawa na tarehe 11 Mei 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 794 iliyopita, yaani tarehe 5 Ramadhani mwaka 646 Hijria Qamaria, alifariki dunia Afdhaluddin Abu Abdillah Khunji, mtoto wa kiume wa Abdul Malik Khunji, katika karne ya 7 Hijria Qamaria. Alizaliwa mwaka 590 Hijria Qamaria katika mji wa Khunji katikati mwa mkoa wa Khalkhal, kaskazini magharibi mwa Iran, ambako alijifunza elimu ya msingi. Msomi huyo wa Kiislamu ambaye alikuwa mtu mwenye hekima na busara, alikuwa mhadhiri wa masomo ya tiba na pia masomo ya Kiislamu kama Fiqhi na Hadithi. Miongoni mwa kazi zake ni kitabu kiitwacho "Kashful Asrar an Qhawamidhul Afkaar Fii Mantiq".***

Miaka 323 iliyopita sawa na tarehe 11 Mei mwaka 1696 Miladia, alifariki dunia mwandishi na mwanafikra wa Kifaransa, Jean de La Bruyère. De la Bruyère alizaliwa mwaka 1645 Miladia, na kuwa wakili baada ya kutabahari katika elimu ya sheria. Hata hivyo baadaye aliachana na kazi ya uwakili na akaanza kufanya kazi serikalini, huku akijifunza masuala ya maadili na tafakuri ya mwanadamu katika zama zake. Mwandishi huyo wa Kifaransa ameandika vitabu vingi vinavyohusu utamaduni, mila na mienendo ya mwanadamu. Kadhalika ametoa mchango mkubwa katika uga wa fasihi ya Kifaransa. ***

Jean de La Bruyère.

Katika siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, inayosadifiana na Ramadhani 5 mwaka 1236 Hijria, al-Haji Mulla Ali Aliyari Tabrizi mmoja wa maulama mahiri wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran. Alitabahari katika elimu za fikihi, hadithi, mashairi na fasihi kama ambavyo alikuwa mahiri pia katika elimu za nujumu na hisabati. Al-Haji Mulla Ali Aliyari Tabrizi aliwahi kufanya safari na kuelekea katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Najaf Iraq ambapo akiwa huko alifanikiwa kunufaika na elimu za wanazuoni mahiri katika zama hizo kama Sheikh Murtadha Ansari na Mirza Shirazi na hivyo kuwa na umahiri mkubwa katika Fikihi na Usuul al-Fikih. Mwanazuoni huyo amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vingi vyenye thamani kubwa. Moja ya vitabu vyake ni "Dalailul Ahkaam fii Sharh Sharai'i al-Islam." ***

Al-Haji Mulla Ali Aliyari Tabrizi

Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita,  alizaliwa Ethel Lilian Voynich mwandishi wa Ki-Ireland. Akiwa na umri wa miaka 21, Bi Lilian alielekea Russia na kusoma fasihi ya lugha ya Kirusi. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanza taratibu kuwa na shauku na fani ya uandishi na fasihi ya lugha. Bi Ethel Lilian aliaga dunia mwaka 1960. ***

Ethel Lilian Voynich

Katika siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, sawa na tarehe 11 mwezi Mei mwaka 1867 Miladia, iliundwa nchi ya magharibi mwa bara Ulaya ya Luxembourg. Awali Luxembourg ilifahamika kama Lutxenbourg katika karne ya 10 hadi 15, ikiwa sehemu ya Utawala wa Roma. Hadi katikati ya karne ya 19, nchi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na serikali na watawala wa madola yaliyokuwa na nguvu na ushawishi wakati huo Ulaya. Luxembourg ambayo imezungukwa na Ubelgiji, Ufaransa na Ujerumani, ilitangazwa kuwa nchi huru katika Kongamano la London lililofanyika Mei 11 mwaka 1867 katika mji huo mkuu wa Uingereza na kuanza kutambulika kimataifa. ***

Luxembourg

Miaka 114 iliyopita katika siku kama ya leo, Salvador Felipe Dali, mchoraji na mchongaji wa sanamu za mawe na mtaalamu wa sanaa ya maandishi au Graphic Arts wa Kihispania alizaliwa. Alianza kuonyesha kipaji chake katika sanaa ya uchoraji akiwa kijana mdogo na kwa muda mfupi tu akawa mashuhuri kimataifa. Salvador Felipe Dali alikuwa na kipaji cha aina yake na ubunifu katika taaluma hizo na ndiye anayehesabiwa nchini Uhispania kuwa mwasisi wa uchoraji wa kisasa. Mwanasanaa huyo stadi aliaga dunia mwaka 1989. ***

Salvador Felipe Dali

Miaka 84 iliyopita katika siku kama ya leo,  kituo cha kwanza cha kurushia matangazo ya televisheni kwa jina la Nipkow kilianza kazi rasmi katika mji wa Berlin huko Ujerumani, hatua ambayo iliwawezesha watu kuanza kutumia runinga au televisheni. Kituo hicho kilipewa jina la Nipkow kwa shabaha ya kumuenzi Paul Gottlieb Nipkow ambaye alikuwa miongoni mwa wavumbuzi asili wa televisheni. Nipkow alivumbua njia ya kubadili picha na kuwa mawimbi na kisha kuyarejesha mawimbi hayo katika sura ya picha. ***

Paul Gottlieb Nipkow

Na miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo, vikosi vya pamoja vya Uingereza na Ufaransa viliingia nchini Ubelgiji kwa shabaha ya kuiunga mkono nchi hiyo iliyokuwa imevamiwa na Ujerumani ya Kinazi. Kuitetea Ubelgiji ni jambo lililokuwa limetiliwa mkazo katika mkataba baina ya Uingereza na Ufaransa. Licha ya Uingereza na Ufaransa kuwa pamoja, jeshi la Ujerumani ya Kinazi si tu kwamba, lilitoa pigo kwa jeshi la Ubelgiji, bali lilivishinda pia vikosi vya Ufaransa na Uingereza na kudhibiti maeneo yote ya ardhi ya Ubelgiji.***

Vita vya Kkwanza vya Dunia