Jumapili, Septemba 15, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 15 Mfungo Nne Muharram 1441 Hijria, sawa na 15 Septemba 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1088 iliyopita, yaani tarehe 15 Muharram mwaka 353 Hijiria, alifariki dunia Ibn Sakan mwanazuoni na mpokezi mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijiria. Ibn Sakan alizaliwa mwaka 294 Hijiria huko mjini Baghdad, Iraq ambapo alisafiri katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Aidha Ibn Sakan alikusanya hadithi nyingi katika miji mbalimbali kama vile Mā Warāʾ an-Nahr (Transoxiana), Khorasan, Iraq, Sham na Misri na mwishowe akaweka makazi yake nchini Misri. Mpokezi huyo wa hadithi ameacha athari nyingi mojawapo ni kitabu cha historia kinachohusu maswahaba wa Mtume SAW, kinachoitwa Al Huruf fis-Swahaba.
Siku kama ya leo, miaka 852 iliyopita, sawa na tarehe 15 Muharram mwaka 589, alizaliwa Ali bin Mussa bin Ja'far maarufu kwa jina la Ibn Twaus, faqihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika eneo la Hillah nchini Iraq. Ibn Twaus alipitisha kipindi cha utotoni katika mji huo na baadaye alihamia mjini Baghdad ambako aliishi kwa kipindi cha karibu miaka 15. Ibn Twaus alipata umashuhuri mkubwa katika elimu na ucha-Mungu na ameandika vitabu vingi ambavyo ni marejeo ya taaluma za Kiislamu. Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni "al Luhuuf" ambacho ndani yake alizungumzia kwa namna bora zaidi matukio ya Siku ya Ashura na harakati ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika medani ya vita vya Karbala. Kitabu kingine mashuhuri cha mwanazuoni huyo ni "Al Iqbalu Biswalihil Aamal". Ibni Twaus alifariki dunia mwaka 664 akiwa na umri wa miaka 75.
Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, yaani sawa na tarehe 15 Septemba mwaka 1821, nchi za Amerika ya Kati za Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru kutoka kwa mkononi Uhispania. Tangu karne ya 19 iliyoenda sambamba na nchi nyingi za eneo hilo kuanzisha wimbi la kupigania uhuru wao, kuharibika hali ya mambo ndani ya Uhispania na kudhoofika kwa serikali kuu ya kijeshi ya Madrid, kulipelekea nchi kadhaa za Amerika ya Latini kuamua kujitangazia uhuru. Baada ya nchi hizo tano kujitangazia uhuru ziliunda Muungano wa Amerika ya Kati. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa muda mrefu ambapo ulivunjika mwaka 1838, huku kila moja ya nchi hizo ikianza kujitawala na kujiendeshea mambo yake yenyewe.
Na siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, yaani tarehe 24 Shahrivar 1289 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Hakim Jahangir Khan Ghashghaei mwanafalsafa mkubwa na msomi mashuhuri wa Kishia. Awali alikuwa mwalimu na alipofikiasha umri wa miaka 40, alielekea mjini Isfahan kwa ajili ya kujiendeleza kielimu katika fani ya mziki. Ni wakati huo ndipo ghafla alipata hamu ya kujiendeleza zaidi kielimu ambapo alielekea katika shule ya mji huo na kuanza kujifunza maarifa ya Kiislamu. Akiwa mjini Isfahan alipata kusoma kwa wasomi wakubwa, elimu za tiba, hisabati na nyota. Pia alisomea elimu ya Irfan na akhlaq (maadili). Baada ya hapo alijishughulisha na ufundishaji ambapo kwa kipindi cha miaka 40 aliweza kuwafundisha wasomi wengi kama vile Seyyed Hossein Borujerdi, Agha Zia ul Din Araghi, Abu l-Hasan al-Isfahani, Muhammad Ali Shah Abadi, Sayyid Hassan Modarres, Haj Rahim Arbab, Allamah Muhammad Hussein Fadhil Tuni, Sayyid Muhammad Kadhim Iswar na makumi ya wengine. Allamah Hakim Jahangir Khan Ghashghaei alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 83 na kuzikwa mjini Isfahani.