Sep 18, 2019 10:47 UTC
  • Ruwaza Njema (16)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 16 ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho huzungumzia Hadithi za watukufu mbalimbali na hasa wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw) kuhusu tabia njema za Mtume huyo ambazo sote Waislamu tunapasa kuziiga na kuzifanyia kazi katika maisha yetu ya kila siku.

Katika kipidi cha leo tutachambua Hadithi kadhaa zinazozungumzia sifa njema za mtukufu huyo (saw) kutoka katika vitabu vya kuaminika, karibuni.

**********

Wapenzi wasikilizaji, tunaanza na Hadithi ifuatayo ambayo imenukuliwa na kukaririwa madhumuni yake katika Hadithi kadhaa ambazo zimepokelewa katika vitabu vya madhehebu zote mbili kuu za Kiislamu yaani Shia na Suni. Mmoja wa wapokezi wa Hadithi hiyo ni Sa'd bin Maadh (MA). Tunasoma Hadithi hiyo ambayo imenukuliwa na Ahmad bin Khalid al-Barqi (MA) ambaye anasema katika kitabu chake muhimu cha al-Mahasin akimnukuu Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) kwamba alisema: 'Mtume (saw) alitembea katika mazishi ya Sa'd bila ya kuvaa joho, na alipoulizwa, je, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, unatembea bila Joho? Alisema: Niliwaona Malaika wakitembea bila joho nami nikapenda kuwaiga.'

*********

Sheikh al-Barqi vilevile amemnukuu Imam Swadiq (as) akisimulia kisa kingine kutoka kwa Mtume (saw) ambapo aliwaiga Malaika na hivyo kutufanya na sisi tupate hamu ya kuiga na kufanya kama alivyofanya mtukufu huyo (saw). Imam Swadiq (as) anasema: 'Mtume (saw) alikuwa ameketi na masahaba zake. Ghafla akawa amesimama kwa wasiwasi na kupokea jeneza lililokuwa limebebwa na watu wanne kwenye mabega yao kutoka eneo la al-Habash. Aliwaambia: Liwekeni chini. Kisha akafunua uso wa maiti na kuuliza: Ni nani kati yenu anayemfahamu? Imam Ali (as) akasema? Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mimi ninamfahamu mtu huyu. Huyu Mtu anatoka katika kabila la Bani Riyaah, ambaye kila mara aliponiona alikuwa akisema: Ninaapa kwa jila la Mwenyezi Mungu kwamba ninakupenda. Mtume (saw) akasema: Ewe Ali! Hakupendi ila muumini na hakuchukii ila kafiri. Hakika wanashiriki mazishi yake (maiti huyu) makundi elfu sabini ya Malaika na katika kila kundi kuna Malaika elfu sabini. Kisha Mtume alimtoa kwenye jeneza (tusi/kitanda) au nguo aliyokuwa amefunikwa na kumkosha, kumvisha kafani, kumswalia na kisha kusema: Malaika wamemfupishia njia na hakika hilo limetokana na kuwa mtu huyu alikuwa akikupenda sana ewe Ali!

 

Hadithi nyingine ya kuvutia tunayokunukulieni hapa wapenzi wasikilizaji kuhusiana na tabia na nyendo njema za Mtume wetu Mtukufu (saw) na ambayo imenukuliwa kutoka kwa Wasii wake mwaminifu al Imam Ali al-Muratdha (as) katika kitabu cha  al-Aamali cha Sheikh Tusi ni hii inayosema kwamba kundi moja la waumini lilimwambia Imam wao huyo mpendwa (as): 'Ewe Ali, tusifie Mtume wetu tuwe ni kana kwamba tunamwomba kwa macho yetu kwa sababu tuna hofu kubwa naye. Hii ni sehemu ya maneno aliyoyatamka Imam (as): Alikuwa mkarimu kuliko watu wote, shujaa zaidi, mkweli zaidi na mtekelezaji ahadi kuliko wote. Alikuwa mbora na mlainifu zaidi kitabia na mwenye heshima zaidi katika kuamiliana na watu wengine. Mtu aliyemwona ghafla alimwogopa na aliyeketi pamoja naye na kumfahamu alimpenda. Sijawahi kumwona mtu kama yeye, kabla na baada yake (saw).'

*********

 Abu Ja'ffar Ahmad bin Muhammad al-Barqi (MA) anasema katika kitabu chake muhimu na cha kuaminika cha al-Mahasin kwamba Abbas bin Musa al-Kadhim (as) alisema: 'Nilimuuliza baba yangu al-Kadhim (as) kuhusu maatam – yaani maombolezo anayofanyiwa mtu aliyeaga dunia – naye Imam (as) akasema: 'Ilipomfikia Mtume (saw) habari ya kuuawa Ja'ffar bin Abi Talib (as), alienda kwa Asma bint Umais, mkewe Ja'ffar na kumuuliza: Wana wangu wako wapi? Yaani wanaye Ja'ffar… Asma akawaita nao walikuwa watatu; Abdallah, Aun na Muhammad. Mtume (saw) akapanguza vichwa vyao, na hapo Asma akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Unapanguza vichwa vyao ni kana kwamba ni mayatima. Mtume (saw) akashangazwa na busara na akili yake na kumuuliza: Ewe Asma! Haujui kwamba Ja'ffar (MA) ameuawa shahidi? Hapo Asma akalia na Mtume (saw) akamwambia: Usilie kwani Malaika Jibril (as) amenifahamisha kwamba Ja'ffar ana (amepewa) mabawa mawili kwenye Pepo, ambayo ni ya yakuti nyekundu. Asma akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nakuomba uwakusanye watu na uwaambie fadhila za Ja'ffar ili wasije wakazisahau. Hapo Mtume (saw) akapanda mimbar na kuwajulisha watu fadhila za Ja'ffar. Kisha aliteremka na kwenda nyumbani kwake (Mtume) na kusema: Ipelekee chakula familia ya Ja'ffar. Tokea hapo hiyo ikawa ni suna.'

 

Wapenzi wasikilizaji, imepokelewa katika kitabu hichohicho cha al-Mahasin kutoka kwa Imam Ja'ffar (as) kwamba alisema: 'Ja'ffar bin Abi Talib (as) alipouawa, Mtume (saw) alimuamuru Fatwima (as) ampelekee chakula Asma bin Umais kwa muda wa siku tatu na kuomboleza naye, na tokea hapo hiyo ikawa ni suna kwamba watu waliofiwa watayarishiwe chakula kwa muda wa siku tatu.'

*********

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakushukuruni kwa kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags