Sep 18, 2019 11:32 UTC
  • Ruwaza Njema (22)

Assalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Tuna furaha kujiunga nanyi tena katika kipindi kingine cha Ruwaza Njema ambapo kwa juma hili tutazungumzia baadhi ya Hadithi za Mtume Mtukufu (saw). Katika kipindi cha juma hili tutazungumzia baadhi ya tabia njema za Mtume Mtukufu (saw) juu ya kuamiliana vyema na kuwahurumia viumbe wa Mwenyezi Mungu na kuondoa huzuni kwenye nyoyo zao, hivyo kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi ili tupate kunufaika kwa pamoja na yale tuliyokuandalieni, karibuni.

***********

Tunaanza na riwaya iliyonukuliwa na fakihi mkubwa wa Kiislamu, Ash-Shaikh Hassan bin Zayn ad-Dīn Ibn Nūr ad-Dīn ʻAlī Ibn Aḥmad, mashuhuri kwa jina la as-Shahid at-Thani katika kitabu chake cha ar-Rasail kutoka kwa al-Hussein bin Zaid ambaye anasema: 'Nilimuuliza Ja'ffar bin Muhammad as-Swadiq (as) kwa kusema: Nifanywe kuwa fidia kwako, je, Mtume alikuwa akifanya mzaha? Imam (as) akasema: Mwenyezi Mungu amemsifu kwa sifa ya 'una tabia tukufu' kutokana na mzaha. Hakika Mwenyezi Mungu aliwateuwa Mitume (waliomtangulia Mtume Mtukufu) hali ya kuwa walikuwa na aina fulani ya ukali na ukavu na akamteua Muhammad (saw) hali ya kuwa ana upole na huruma. Na miongoni mwa upole wake huo kwa umma wake ni kufanya nao mzaha ili yeyote kati yao asihisi uoga na kutomtazama kutokana na utukufu wake. Kisha Imam Swadiq (as) akasema: Baba yangu Muhammad alinihadithia kutoka kwa baba yake Ali bin Hussein kutoka kwa baba yake Ali (as) kuwa alisema: 'Mtume (saw) alipomwona mmoja wa masahaba zake akiwa na huzuni alimfanyia mzaha ili kumfurahisha na kumwambia: Mwenyezi Mungu hapendi kumwona mtu akiwa amekunja uso mbele ya ndugu zake.'

Na tunasoma katika kitabu cha Akhlaki cha Abu Qassim al-Kufi hadithi ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam Ja'ffar (as) ambaye anasema: 'Si muumini mtu asiyefanya mzaha. Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa akifanya mzaha na kutozungumza ila haki.'

Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Allah kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Allah sana. (Surat al Ahzab, 33:21)

 

Ndugu wasikilizaji, moja ya sifa bora za ukarimu wa Mtume wetu Mtukufu (saw) kwa waja wa Mwenyezi Mungu ni kuwakirimu kwa kwa kuwaongoza kwenye njia nyoofu, na ni kwa nini isiwe hivyo, hali ya kuwa yeye ni yule asiyezungumza kwa matamanio na matakwa ya mtu binafsi? Kwa mfano Sheikh Ahmad al-Barqi (MA) ananukuu katika kitabu chake cha al-Mahasin hadithi ambayo imepokelewa na Muammar bin Khalid ambaye anasema: 'Mfanyakazi wa nyumbani wa Abu Hassan al-Ridhwa (Imam Ali Ridha as) kwa jina la Sa'd aliaga dunia na Imam akaniomba nimshauri katika kutafuta mtu (mfanyakazi mwingine) mwenye tabia nzuri na mlinda amana. Nikamwambia: Mimi nikushauri wewe?! Akajibu huku akiwa amekasirika: Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa akiwashauri masahaba zake na kisha kufanya alivyoamua kwa msingi wa ushauri huo.'

Na miongoni mwa sifa za kuvutia za Mtume Muhammad (saw) ni kuwa kwake na huruma na mpole mbele ya waja wa Mwenyezi Mungu na kuwaongoza wale waliopotea njia. Kwa mfano imepokelewa katika kitabu cha Makarim al-Akhlaq hadithi kutoka kwa Jabir al-Answari (MA) inayophusiana na tabia njema za Bwana Mtume (saw) katika medani ya vita. Inasema: 'Mtume alikuwa akitembea mwishoni mwa watu. Akiwasaidia wasiojiweza, akiwabeba kwenye kipandio chake na kuwaongoza.'

Na tunazingatia Riwaya hii ambayo imenukuliwa katika kitabu cha al-Ja'fariyaat, kutoka kwa Imam Ali al-Murtadha (as) anayesema: 'Mtume (saw) alipita karibu na watu waliokuwa wamemtundika kuku sehemu ya juu huku wakiwa wanamrushia mishele. Mtume akauliza: Ni nani hawa? Mwenyezi Mungu awalaani.!'

*********

Al-Allama as-Sheikh at-Tabarsi (MA) ananukuu katika kitabu chake cha Makarim al-Akhlaq Hadithi kutoka kwa Imam Ali (as) inayosema: 'Mtume (saw) hakuwahi kumpa mkono mtu yoyote yule na kisha kuuvuta mkono wake kabla mtu yule aliyemsalimia kuvuta mkono wake mwenyewe na kamwe mtu hakufika mbele yake kwa haja au mazungumzo naye akawa wa kwanza kuyakatiza mazungumzo hayo na kumwacha pake yake, bali alijadiliana naye hadi mwisho wa mazungumzo. Hakuwahi kuonekana akinyoosha miguu yake mbele ya mtu yeyote, na alipolazimika kuchagua moja kati ya mambo mawili alichagua lililokuwa gumu zaidi kulitekeleza. Kuhusiana na ulipizaji kisasi wa dhulma na mabaya aliyofanyiwa, hakuwa akilipiza kisasi isipokuwa alipolazimika kufanya hivyo kwa ajili ya kuzuia kuvunjwa sheria za Mwenyezi Mungu. Katika hali hiyo hasira ilikuwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na sio kwa ajili yake binafsi. Hakuwahi kula chakula hali ya kuwa ameegemea kitu hadi alipoaga dunia. Hakuulizwa haja yoyote naye akawa ametoa jibu hasi. Hakuwahi kukataa kukidhia haja ya mwenye kuomba. Alipokuwa na uwezo wa kumpa alichoomba alimpa, la sivyo, alikuwa akimridhisha kwa kumwambia maneno mazuri na ya kuvutia. Swala zake, hali ya kuwa zilikuwa timilifu na kamilifu, zilikuwa nyepesi zaidi kuliko swala zote na hotuba zake zilikuwa fupi kuliko hotuba zote na alijiepusha na mambo ya pembeni ambayo hayakuwa na udharura wa kusemwa. Watu walikuwa wakihisi uwepo wake karibu nao kutokana na harufu yake nzuri.'

Ruwaza Njema

 

Tunaendelea kuchambua maneno ya Maulana Amir al-Mu'mineen Ali (as) katika kumsifu bwana na ndugu yake, mpendwa na mbora wa viumbe wa Mwenyezi Mungu, Mtume Mtukufu (saw). Anasema (as): 'Watu walikuwa wakijua Mtume amekaribia kutokana na harufu yake nzuri na ya kuvutia. Alipokuwa akila chakula na watu, alikuwa wa kwanza kuanza kula na wa mwisho kuacha kula (ili watu wasiache kula kwa kumuonea haya). Alipokula alianza kula sehemu iliyokuwa mbele yake isipokuwa kuhusiana na tende ambapo alipeleka mkono wake kwingine. Alipokunywa maji alikuwa akiyakunywa mara tatu na kwa kituo. Alikuwa akiyameza taratibu na sio mara moja. Alikuwa akila na kunywa kwa kutumia mkono wake wa kulia na vilevile akitumia mkono huo huo kutoa na kuchukua vitu. Hakuwa akichukua wala kupeana kitu chochote ila kwa kutumia mkono huo wa kulia. Akitumia mkono wake wa kushoto katika mambo mengine. Alipokuwa akiitana, alikuwa akiita mara tatu, alipokuwa akizungumza alikuwa akizungumza taratibu na alipoomba idhini ya kuingia aliomba mara tatu. Maneno yake yalikuwa wazi na mepesi kiasi cha kueleweka na kila mtu aliyeyasikia. Alipozungumza, meno yake yaling'ara ni kana kwamba nuru ilikuwa ikitoka mdomoni kwake. Alikuwa akiwatazama watu kwa muda mfupi ili wasiogope, na wala hakuwa akiwazungumzisha watu mambo ambayo hawakupenda kuyasikia……'

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa mmepata kunufaika na yale tuliyokuandalieni kwa juma hili. Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa yake Mola, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.

 

Tags