Sep 22, 2019 02:27 UTC
  • Jumapili, 22 Septemba, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 22 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria, sawa na tarehe 22 Septemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1682 iliyopita, yaani sawa na tarehe 22 Septemba mwaka 337, vilianza vita vya miaka 13 kati ya Iran na Roma katika utawala wa Shapur II (Dhul Aktaf), wa silsila ya watawala wa Sasania na ambavyo katika historia vilifahamika kama vita vya duru ya kwanza. Vita vya duru ya pili vilianza mwaka 359, ambapo katika duru zote, Wairani waliibuka na ushindi. Katika duru ya kwanza ambapo vita hivyo vilidumu hadi mwaka 350, Waroma walipoteza kila kitu walichokuwa wakikidhibiti eneo la mashariki mwa bahari ya Mediterranean, huku mfalme wao akiuawa katika duru ya pili ya vita hivyo.

Sanamu la Shapur II

Siku kama ya leo miaka 981 iliyopita alifariki dunia mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi, ambaye ni mashuhuri kwa jina la Sheikhul Twaaifa. Sheikh Tusi alizaliwa katika mji wa Tus kaskazini mwa Iran na akaelekea Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu ya juu baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa Iraq na miaka kadhaa baadaye akaweka msingi wa chuo kikuu cha kidini cha Najaf. Kituo hicho cha kidini kina historia ya miaka elfu moja na ni moja ya vituo muhimu mno vya elimu ya Kiislamu. Sheikh Tusi ameandika vitabu vingi sana katika taaluma mbalimbali. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani Tukufu ya al Tibyan na vitabu vya hadithi na fiqhi vya al Istibsar na al Tahdhiib.

Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, nchi ya Bulgaria ilijipatia uhuru kutoka kwa utawala wa Othmania. Bulgaria  ilianza kutawaliwa na utawala huo tangu mwishoni mwa karne ya 14. Wakati huo maudhi dhidi ya Wakristo yalianza na kuendelea kwa karibu miaka 500 ya udhibiti wa Othmania kwenye nchi hiyo. Katika kipindi hicho kulishuhudiwa uasi wa mara kadhaa wa raia wa Bulgaria. Na hatimaye mwaka 1878 Miladia nchi hiyo ikajipatia uhuru na kujitangazia mamlaka ya ndani. Hatimaye tarehe 22 Septemba mwaka 1908 Miladia mfalme wa wakati huo wa Bulgaria alitangaza uhuru kamili wa nch hiyo yaani katika siku kama ya leo.

Bendera ya Bulgaria

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, nchi ya Mali iliyo kaskazini magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru. Karibu miaka elfu mbili iliyopita nchi ya Mali ilikuwa na utamaduni mkubwa na uliong'ara. Hata hivyo nchi hiyo tangu karne ya 18 hadi ya 19 Miladia ilikuwa moja ya tawala za ufalme wa Sudan. Baada ya Morocco kutwaa baadhi ya maeneo yaliyokuwa chini ya tawala za ufalme wa Sudan ikiwemo Mali, tawala mbalimbali za kikabila nchini Mali zilifanikiwa kuingia madarakani. Satwa ya Wafaransa nchini Mali ilianza mnamo karne ya 19 na hadi kufikia mwaka 1898 nchi hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Ufaransa. Hata hivyo Mali ambayo ilikuwa ikiitwa Sudan ya Ufaransa, mwaka 1958 ilianza kujitawala na mwaka 1960 ikajipatia uhuru wake kamili.

Bendera ya Mali

Na siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, majeshi ya dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein yalianza mashambulio makubwa ya anga na nchi kavu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya Iran. Jeshi la Iraq lilikuwa limefanya uvamizi na mashambulizi kadhaa katika maeneo ya mpakani ya Iran miezi kadhaa nyuma. Magari ya deraya na vikosi 12 vya jeshi la nchi kavu la Iraq viliyashambulia maeneo ya mipaka ya kusini magharibi mwa Iran. Mapambano makali ya wananchi wa Iran yaliwalazimisha askari wa dikteta Saddam kurejea nyuma hadi kwenye mipaka inayotambulika kimataifa.

Shambulizi la Saddam dhidi ya Iran