Jumanne, tarehe 24 Septemba, 2019
Leo ni Jumanne tarehe 24 Muharram mwaka 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 24 Septemba 2019.
Miaka 41 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vikosi vya usalama vya utawala wa Baath nchini Iraq vikishirikiana na utawala wa Shah viliizingira nyumba ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu huko Najaf. Kwa kuzingatia uhusiano wake mzuri na utawala wa Shah, utawala wa zamani wa Iraq ulimtaka Imam Khomeini asifanye mahojiano na waandishi wa habari, kutoa taarifa, kuhutubia wala kuzungumzia hali ya mambo ya Iran dhidi ya utawala wa Shah. Imam Khomeini aliwajibu kwa kusema kuwa: "Nitatekeleza wajibu wangu wa kisheria popote pale nitakapokuwa." Baada ya hapo, serikali ya wakati huo ya Iraq, ilimlazimisha Imam Khomeini kuondoka Iraq na hatua hiyo ikaandaa uwanja wa hijra ya kihistoria ya Imam Khomeini ya kuelekea Paris, Ufaransa na kupamba moto harakati za Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Guinea Bissau ilitangaza uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mreno. Guinea Bissau iligunduliwa mwaka 1446 na Mwana Mfalme Henry aliyekuwa akitawala Ureno pamoja na wenzake na kuwa koloni la nchi hiyo. Guinea Bissau ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Guinea Ureno, ilikuwa miongoni mwa vituo vya biashara ya utumwa ya wazungu katika karne za 17 na 18. Na hatimaye ilipofika mwaka 1974, Ureno ikakubali kuwa huru nchi ya Guinea Bissau. Guinea Bissau iko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Atlantic.
Katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, ndege za kijeshi za Ujerumani zilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya mji mkuu wa Poland, Warsaw. Mashambulio hayo yalifanyika sambamba na kuanza Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na yaliendelea kwa muda wa siku tatu. Hatimaye wananchi wa mji huo walisalimu amri mbele ya majeshi ya Ujerumani baada ya mapambano na siku kumi na moja. Mashambulio hayo ya kinyama yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 15,000.
Na siku kama ya leo miaka 169 iliyopita aliaga dunia msomi mkubwa wa Kiislamu Al Haj Mulla Muhammad Taqi Esterabadi. Msomi huyo alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Alipata idhini na daraja ya ijtihadi kwa Muhammad Taqi bin Muhammad Rahiim Eehran Isfahani aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Sahib Hidayatul Mustarshidiin baada ya kupata elimu kwa maulamaa wakubwa na mashuhuri wa zama hizo katika mji mtukufu wa Najaf kwa kipindi cha miaka 14. Alirejea nchini Iran mwaka 1271 Hijria Shamsia na kufariki dunia katika eneo la Esterabad.
