Oct 21, 2019 09:17 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Oktoba 21

Karibu mpenzi msikilizaji katika dakika hiki chache za kutupia jicho baadhi ya matukio muhimu yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika uga wa michezo kitaifa na kitaifa....

Soka ya Ufukweni; Iran ya 3

Timu ya taifa ya Soka ya Ufukweni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa medali ya shaba baada ya kuipuku Italia katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kwenye mashindano ya World Beach Games. Iran iliichachafya Italia katika mikwaju ya penati, baada ya timu mbili hizo kutoa sare ya mabao 5-5 katika kitimutimu hicho cha Jumatano.

Timu ya taifa ya soka ya ufukweni ya Iran

 

Kabla ya hapo, Iran ilikuwa imechabangwa na Russia 6-2 katika mchezo wa nusu fainali uliochezewa katika ufukwe wa Katara mjini Doha, Qatar. Italia ilipoteza pia katika mchezo wake wa nusu fainali iliposhuka dimbani kuvaana na Brazil, ambapo iliadhibiwa mabao 7-5. Nchi 97 zimeshiriki mashindano hayo ya dunia ya soka ya ufukweni, yaliyoandaliwa na Muungano wa Kamati za Olimpiki Duniani ANOC.

Iran kuishtaki Bahrain FIFA

Mashabiki wa timu ya taifa ya soka ya Bahrain wamekosolewa vikali kwa kuuvunjia heshima wimbo wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wakati wa mechi kati ya timu hiyo na Iran. Masoud Soltanifar, Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itawasilisha malalamishi rasmi kwa Shirikisho la Soka Duniani FIFA. Amesema, "Kitendo cha kuuvunjia heshima wimbo wa taifa wa Iran kilichofanywa na mashabiki wa Bahrain kiko dhidi ya moyo wa michezo na tunataka wakuu wa FIFA na Shirikisho la Soka Asia wachukue hatua za kisheria dhidi ya kitendo hicho."

Masoud Soltanifar, Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran

 

Mashabiki hao wa Bahrain walifanya kioja hicho cha kupiga kelele na kuudhihaki wimbo huo wa taifa wa Iran Jumanne usiku wakati wa mchuano wa mzunguko wa pili wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Qatar mwaka 2022. Iran ilikubali kichapo cha bao 1-0 katika mchezo huo wa Kundi C uliopigwa katika Uwanja wa Riffa nchini Bahrain. Baharain ilipata ushindu huo hafifu kupitia mkwaju wa penati.

Tanzania yatinga CHAN 2020 baada ya muongo mmoja

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars imetinga fainali za Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani CHAN mwaka ujao 2020, baada ya kupita muongo mmoja. Hii ni baada ya kuigaragaza Sudan siku ya Ijumaa katika jiji la Khartoum, katika mchezo wao wa marudiano wa kuwania kufuzu kucheza fainali za CHAN 2020. Tanzania ilienda Sudan ikiwa imepoteza 1-0 katika mchezo wake wa kwanza nyumbani jijini Dar es Salaam. Tanzania ikiwa ugenini Sudan ilifanikiwa kupindua matokeo na kupata ushindi wa magoli 2-1. Magoli ya Taifa Stars yalifungwa na Erasto Nyoni dakika ya 49 na Ditram Nchimbi dakika ya 78.

Michuano ya CHAN ya mwaka jana

Matokeo yakamalizika kwa jumla ya 2-2 lakini Tanzaia inafuzu fainali za CHAN baada ya kuwa imefunga magoli mengi ugenini. Timu hiyo ya taifa ya kandanda ya Tanzania ilipokewa kwa ushujaa iliporejea nyumbani katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere. Hii ni mara ya kwanza kwa Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za CHAN toka 2009, abapo iliitoa Sudan na kwenda Ivory Coast. Wallace Karia ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzani TFF anabakia kuwa Rais wa kwanza wa taasisi hiyo kuweka rekodi ya kuwa katika utawala na kufanikisha Taifa Stars kufuzu CHAN na AFCON 2019 kwa mwaka mmoja; lakini pia ndani ya miaka miwili ya utawala wake amefanikisha pia timu ya Soka ya Ufukweni kufuzu AFCON ya beach soccer.

Wakati huohuo, timu ya za taifa za soka za Uganda na Rwanda zimejikatia tiketi ya kushiriki mashindno hayo ya kikanda ya CHAN mwakani. Uganda Cranes imesonga mbele kwa mara ya tatu mfufulizo baada ya kuiadhibu vikali Burundi kwa kuizaba jumla ya magoli 6-0. Vijana wa Amavubi wa Rwanda nao wamejikatia tiketi ya kushiriki CHAN 2020 baada ya kuisasambua Ethiopia jumla ya mabao 2-1 katika mechi mbili walizocheza.

Raga; Kenya yatwaa Safari 7's

Timu ya taifa ya Kenya ya mchezo wa raga kwa wachezaji saba kila upande imetwaa taji la kimataifa la Safari Sevens baada ya kuicharaza vibaya Afrika Kusini katika mchuano wa fainali uliopigwa Jumapili katika Uwanja wa RFUEA ulioko jijini Nairobi. Timu hiyo inayofahamika kama Morans iliwafanya vibaya vijana wa Blitzebokke wa Afrika Kusini na kuwabwaga kwa alama 19-14. Katika kipindi cha kwanza, Morans wa Kenya walikuwa kifua mbele kwa alama 19 kwa nunge, kutokana na kazi ya ziada iliyofanywa na wachezaji Jeff Oluoch, Geoffrey Okwatch na Alvin Otieno. Kenya iliipelekea mchakamchaka timu hiyo ya Afrika Kusini licha ya kuwa ni mabingwa mara tatu wa mashindano ya dunia ya World Rugby Seven Series.

Huku hayo yakijiri, Afrika Kusini siku ya Jumapili ilizima ndoto ya mweeji Japan ya kufikia nusu fainali ya Kombe la Dunia la Raga kwa kuibamiza 26-3 katika hatua ya robo fainali huko Tokyo na kujikatia tiketi ya kupambana na wakali Wales katika nusu fainali ya mashindano hayo. Japan iliitambia Afrika Kusini kwa 34-32 katika kombe la dunia mwaka uliopita lakini mechi ya Jumapili iliyochezewa Tokyo ilikuwa zamu yao kulipiza kisasi dhidi ya mabingwa hao mara mbili duniani wa raga. Afrika Kusini sasa imetinga nusu fainali na itacheza na Wales walioishinda Ufaransa kwa 20-19 mapema Jumapili. Springboks ya Afrika Kusini iliyowahi kushinda Kombe la Webb Ellis mwaka 1995 na 2007, sasa ina ndoto ya kulinyakua kombe la dunia la mwaka huu 2019.

Dondoo za Hapa na Pale

Timu ya soka ya 'As Roma' ya nchini Italia imekuwa klabu kubwa ya kwanza barani Ulaya kuanzisha ukurasa wake katika mtandao wa Twitter kwa lugha ya Kiswahili. Ukurasa wa klabu hiyo mashuhuri nchini Italia na barani Ulaya ambayo ilianzishwa mwaka 1927 utakuwa ukiandika habari zake kwa lugha adhimu ya Kiswahili. Ukurasa huo wa lugha ya Kiswahili ulizinduliwa rasmi jana, na inaaminika lengo kuu la 'As Roma' ni kuwafikia mamilion ya watu wanatumia lugha ya Kiswahili katika eneo la Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani. Baada ya kuzinduliwa ukurasa huo, wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili katika maeneo mbalimbali wameonekana wakipongeza hatua hiyo na kuanza kutoa maoni yao katika ukurasa huo.

Ukurasa wa Twitter wa AS Roma

 

Kwengineko, nyota wa soka raia wa Argentina, Lionel Messi anaongoza kwa kuvunja rekodi nyingi zaidi katika historia ya Barcelona, kwa kushinda kiatu cha dhahabu mara 6. Nyota huyo wa Argentina alipokea tuzo hiyo ya kiatu cha dhabu katika sherehe zilizoandaliwa jijini Barcelona. Katika msimu uliopita wa La Liga Messi alipachika magoli 36, huku Mbabpe aliyepachika magoli 33 katika ligi ya Ufaransa  alishika nafasi ya pili katika kinyanganyiro hicho cha kuwania kiatu cha dhahabu. Katika michezo 692 aliyoichezea Barcelona amepachika wavuni magoli 639.

Lionell Messi akihutubia baada ya kutuzwa Golden Boot

Na wanariadha wanawake wenye jinsia mbili sasa watalazimika kushusha nusu ya viwango vyao vya homoni za kiume chini ya sheria mpya iliyotolewa na Shirikisho la Riadha Duniani IAAF. Sheria hiyo inawahusu wanariadha wenye homoni nyingi za kiume kama Caster Semenya wa Afrika Kusini. Chini ya sheria hiyo mpya, wanariadha wenye jinsia mbili hawatakiwi tena kutambuliwa na sheria kwa jinsia zao bali watahitajika kutoa tamko lililosainiwa, la kujitambua kuwa ni wanawake.

Baraza la Shirikisho la Riadha Duniani lililokutana Doha, limepitisha sheria hiyo inayotaka kupunguza homoni za kiume kwa wanariadha wanawake na kuwa chini ya nanomoles tano kwa lita hali ambayo inapaswa kuendelea kwa kipindi cha angalau miezi 12 kabla ya kutangazwa kuwa wanastahili kushindana kwenye mbio za wanawake. Kiwango cha awali kilikuwa ni nanomoles 10.

.......................................TAMATI............................