Jumanne, tarehe 22 Oktoba, 2019
Leo ni Jumanne tarehe 23 Safar 1441 Hijria sawa na Oktoba 22 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, aliaga dunia Arnold Joseph Toynbee mwanahistoria mtajika wa Uingereza. Alizaliwa mwaka 1889. Toynbee alikuwa akifundisha taaluma ya Historia ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha London. Msomi huyo ameandika vitabu vingi katika uga wa historia na baadhi ya vitabu vyake ni A Study of History, Change and Habit, Choose Life na Civilization on Trial.
Tarehe 30 Mehr miaka 67 iliyopita, Dakta Hussein Fatimi, Waziri wa Mambo ya Nje wa muda wa serikali ya Dakta Muswadiq, aliyekuwa Waziri Mkuu wa muda wa Iran wakati huo alitangaza kukatwa uhusiano wa kisiasa kati ya Iran na Uingereza. Uamuzi huo ulikabidhiwa kwa balozi mdogo wa Uingereza mjini Tehran, baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri. Dakta Fatimi alisema Tehran imeamua kukata uhusiano na Uingereza kutokana na upuuzaji wa serikali ya London kwa matakwa ya wananchi wa Iran ya kujipatia haki zao, hususan katika uwanja wa kutaifisha sekta ya mafuta. Dakta Fatimi aliwataka viongozi wa London wabadili siasa zao kuhusiana na Iran.
Katika siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, Paul Cezanne mchoraji maarufu wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67. Alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na fani ya uchoraji tangu akiwa mdogo, lakini kutokana na msisitizo wa baba yake aliingia Chuo Kikuu na kusoma taaluma ya sharia. Hatimaye akiwa na umri wa miaka 24, baba yake alimruhusu kuendelea na masomo katika taaluma ya uchoraji. Mwanzoni mabango ya uchoraji ya Paul Cezanne hayakupata wafuasi wengi na athari zake za uchoraji zilikabiliwa na ukosoaji mkubwa. Mwenendo huo uliendelea hadi alipofikisha umri wa miaka 50 ambapo hatua kwa hatua alianza kupata umashuhuri kutokana na kuuza mabango yake ya uchoraji.
Miaka 140 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia msomi mkubwa na mtaalamu wa fiq'hi wa Kiislamu Sheikh Muhammad Baqir Agha Najafi Isfahani. Sheikh Agha Najafi alizaliwa mnamo mwaka 1234 Hijiria nchini Iran na baada ya kusoma elimu mbalimbali za kidini mjini Isfahan, alielekea Najaf huko Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake. Baada ya kurejea kutoka Najaf msomi huyo aliweka makazi yake mjini Isfahan na kujikita katika kufundisha na kuwalea wanafunzi sambamba na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na "Lubbul-Fiq'h" na "Lubbul-Usuul."