Jan 23, 2020 02:27 UTC
  • Alkhamisi tarehe 23 Januari 2010

Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Januari 23 mwaka 2020.

Januari 23 mwaka 1556 yaani miaka 464 iliyopita, moja kati ya mitetemeko mikubwa kabisa ya ardhi duniani ulitokea katika jimbo la Shaanxi nchini China. Zilzala hiyo ilisababisha hasara kubwa katika jimbo hilo lililokuwa likihesabiwa kuwa na wakazi wengi zaidi nchini China. Watu wapatao 830,000 walipoteza maisha kufuatia janga hilo kubwa na la kutisha la mtetemeko wa ardhi katika jimbo hilo la Shaanxi.

Katika siku kama ya leo miaka 101 iliyopita yaani tarehe 23 Januari 1919, Chama cha Kifashisti cha Italia kiliasisiwa na Benito Mussolini. Wanachama wa chama hicho walikuwa wakivaa mashati meusi kama sare zao. Sare hiyo ilipelekea wafuasi wa chama hicho kujulikana kwa jina la watu wa " Mashati Meusi'.'' Fikra za Kifashisti zilikuwa zimejengeka juu ya misingi ya kuunda dola moja kubwa la kidikteta na fikra hizo zilikuwa zikipingana na aina yoyote ya uhuru. Oktoba mwaka 1922, Benito Mussolini na wafuasi wake waliuteka mji wa Roma na yeye mwenyewe akashika hatamu za uongozi akiwa Waziri Mkuu. Kuanzia hapo kiongozi huyo alianza kutekeleza malengo na sera za Chama cha Kifashisti. Hata hivyo mwaka 1945, mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia Benito Mussolini alitiwa mbaroni na wazalendo na kisha akanyongwa.

Benito Mussolini

Miaka 70 iliyopita katika siku kama ya leo, Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) liliutangaza mji wa Baitul Muqaddas ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu, kuwa mji mkuu wa utawala huo badala ya Tel Aviv. Uamuzi huo uliofikiwa na Bunge hilo miaka miwili tu baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Wapalestina, uliwakasirisha mno Waarabu na Waislamu. Njama hiyo ya Israel iliyolenga kupata ridhaa ya nchi nyingine ili ziutambue rasmi mji huo kama mji mkuu wake na hivyo zihamishie balozi zao katika mji huo, haikuwa na natija, kwani hadi leo mji wa Tel Aviv ungali unatambuliwa kama mji mkuu wa utawala huo vamizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset)

Na katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita baada ya kupatikana uhakika kamili wa uamuzi wa Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kurejea hapa Iran akitokea uhamishoni Ufaransa, nchini Iran kuliundwa Kamati ya Mapokezi ya Imam. Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 50 na ilijumuisha wananchi kutoka vyama na makundi mbalimbali ya mapinduzi. Jukumu kuu la kamati hiyo lilikuwa ni kumpokea Imam na kuchunga usalama wake, kuhakikisha kunakuweko nidhamu, usalama na kuandaa sherehe za mapokezi ya kurejea Imam Khomeini hapa nchini.

Mapokezi ya Imam Khomeini

 

Tags