Mar 15, 2020 02:28 UTC
  • Jumapili tarere 15 Machi 2020

Leo ni Jumapili tarehe 20 Rajab, 1441 Hijiria sawa na tarehe 15 Machi 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1428 iliyopita, yaani sawa na tarehe 20 Rajab mwaka wa 13 Hijiria, vilitokea vita vya Yarmuk kati ya jeshi la Kiislamu na jeshi la utawala wa kifalme wa Roma ya Mashariki katika bonde lililojulikana kwa jina hilo huko Palestina. Ushindi wa Waislamu huko Sham, yaani Syria ya sasa ulimpelekea mfalme wa Roma kuandaa jeshi kubwa kwa ajili ya kupigana na Waislamu. Lakini, Waislamu waliweza kutoa pigo kwa wanajeshi wa mfalme huyo wa Roma licha ya kuwa na idadi ndogo ya wapiganaji na suhula chache za kivita. Kufuatia ushindi huo Waislamu walisonga mbele na kufika eneo la Mashariki la Ufalme wa Roma na mwaka mmoja baada ya hapo Waislamu wakafanikiwa kuchukua udhibiti wa mji wa Baitul Muqaddas pasina umwagaji damu.

Eneo kulipojiri vita vya Yarmuk

Siku kama ya leo miaka 166 iliyopita yaani sawa na tarehe 15 Machi 1854 Miladia, alizaliwa tabibu maarufu wa Kijerumani kwa jina la Emil Adolf von Behring. Behring aliendeleza utafiti wa Louis Pastor, mwanakemia wa Kifaransa wa zama hizo katika uwanja wa kutambua na kuzuia maradhi yanayoambukiza na kupata mafanikio makubwa katika suala hilo. Emil Adolf von Behring alitunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia mwaka 1901.

Emil Adolf von Behring

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, sawa na tarehe 25 Esfand 1285 Hijiria Shamsia, alizaliwa Parvin E'tesami, mwandishi na malenga wa kike mwenye kipawa cha hali ya juu wa Iran huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran, katika familia ya wasomi na wataalamu wa fasihi. Baba yake Yusuf E'tesami al-Mulk ni mmoja wa wafasiri na waandishi wakubwa wa zama zake ambapo nyumba yake ilikuwa makutano ya wataalamu wa fasihi kama vile Malek osh-Sho'arā Bahar na Allamah Dehkhodā. Parvin E'tesami alijifundisha fasihi ya Iran na Kiarabu kwa baba yake ambapo tangu akiwa mdogo alikuwa na kipawa kikubwa cha kusoma mashairi. Aidha katika safari zake zote ndani na nje ya nchi alikuwa pamoja na baba yake ambapo alipata uzoefu mkubwa katika uga wa mashairi. Ameacha vitabu kadhaa vya mashairi na kasida zinazozungumzia thamani za kibinaadamu, kimaadili na kijamii. Malenga huyo mkubwa alifariki dunia mwaka 1320 Hijiria Shamsia akiwa na umri wa miaka 35.

Parvin E'tesami

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, utawala wa zamani wa Iraq wa Baath uliushambulia mji wa Wakurdi wa Halabcha huko kaskazini mashariki mwa Iraq kwa silaha za kemikali. Makumi ya ndege za kivita za utawala wa Saddam zilifanya mashambulizi ya kinyama kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Kikurdi wa mji wa Halabcha. Utawala wa Baath ulianzisha mashambulizi hayo katika hali ambayo kwa upande mmoja ulikuwa umeshindwa kukabiliana na wapiganaji wa Kiislamu wa Iran na wa Kikurdi wa Iraq na kwa upande wa pili wananchi Waislamu wa Halabcha waliwakaribisha na kuwaunga mkono wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na dhulma na ukandamizaji usio na kipimo waliokuwa wakifanyiwa na Saddam. Nchi za Magharibi ambazo ndizo zilizoupatia utawala wa Saddam teknolojia na nyenzo zilizohitajika kwa ajili ya uzalishaji wa silaha hizo za kemikali, hazikuchukua hatua yoyote ya kivitendo mbele ya jinai hizo za Saddam, licha ya karibu watu elfu tano kuuawa katika maafa hayo ya kutisha ya Halabcha.

Jinai ya Saddam dhidi ya Wakurdi wa Halabcha

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita sawa na tarehe 15 Machi 1989, ardhi ya Taba huko kaskazini mashariki mwa Misri ilikombolewa baada ya kukaliwa kwa mabavu kwa miaka mingi na utawala ghasibu wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulilikalia kwa mabavu jangwa la Sinai katika vita vya mwaka 1967, ambalo upande wa mashariki mwake linapatikana eneo la Taba. Utawala wa Tel Aviv ulikubali kuirejeshea Misri jangwa la Sinai baada ya kusaini mkataba wa Camp David mwaka 1987. Israel iliendelea kulikalia kijeshi eneo muhimu la Taba huko kaskazini mwa Ghuba ya Aqaba, licha ya utawala huo wa Kizayuni kuondoka katika baadhi ya sehemu za jangwa hilo.

Ardhi ya Taba huko kaskazini mashariki mwa Misri