Jumatatu tarehe 23 Machi mwaka 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 28 Rajab mwaka 1441 Hijria inayosadifiana na 23 Machi mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita, ilianza safari ya msafara wa Imam Hussein (as) kutoka Madina kwenda mjini Makkah. Hatua hiyo ilijiri baada ya kufariki dunia Muawiyah Bin Abu Sufiyan tarehe 15 ya mwezi wa Rajab na kutwaa madaraka mwanaye, Yazid Bin Muawiyah. Baada ya Yazid kutwaa madaraka, haraka sana alimtaka mtawala wa mji wa Madina amlazimishe Imamu Hussein (as) kutoa baia (kiapo cha utiifu) kwake na kwamba iwapo angekataa kufanya hivyo basi amuuwe. Kwa kuzingatia kwamba Yazid alikuwa mtu muovu na mtenda madhambi, Imamu Hussein alikataa kutoa kiapo hicho na kwa ajili hiyo akaamua kuondoka Madina yeye na watu wa familia ya Mtume Muhammad (saw) kuelekea mjini Makkah. Kabla ya kuanza safari hiyo, Imamu Hussein (as) alimuusia kaka yake Muhammad Ibnil-Hanafiyyah akisema: "Ninatoka kwa ajili ya kurekebisha umma wa babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu saw, ninataka kuamrisha mema na kukataza maovu na kupita njia ya babu yangu Muhammad na baba yangu Ali Ibn Abi Twalib (as)…." Baada ya kufika mjini Makkah, baadaye na kufuatia kukithiri barua za watu wa mji wa Kufa Iraq, waliokuwa wamemtaka aelekee mji huo ili awaongoze, Imamu Hussein (as) aliamua kuelekea mji huo ambapo hata hivyo alizuiliwa na jeshi la Yazid eneo la Karbala na kuuawa shahidi yeye na watu wa familia ya Mtume (saw) katika eneo hilo.
Siku kama ya leo miaka 368 iliyopita, yaani sawa na tarehe 23 Machi mwaka 1652, kulianzishwa shambulizi la manowari za kijeshi za Uingereza dhidi ya majeshi ya Uholanzi. Amri ya shambulizi hilo ilitolewa na Oliver Cromwell aliyekuwa dikteta wa wakati huo wa Uingereza. Akipata uungaji mkono wa Bunge la Uingereza, Cromwell alimpindua mfalme wa Uingereza na kisha kulivunja bunge la nchi hiyo. Inasemekana kuwa, lengo la kutekeleza shambulio hilo lilikuwa ni kulimaliza nguvu jeshi la Uholanzi ambalo lilikuwa na nguvu kubwa ya majini.
Miaka 271 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Pierre-Simon Laplace mwanahisabati mashuhuri wa kifaransa. Alizaliwa mwaka 1749 na baada ya kuhitimu masomo alijishughulisha na kufundisha hisabati. Laplace alitumia sehemu kubwa ya umri wake kutwalii na kufanya uhakiki kuhusiana na elimu za nujumu na hisabati.
Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, liliasisiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (W.M.O). Shirika hilo linafungamana na Umoja wa Mataifa na taasisi zote za hali ya hewa ulimwenguni hushirikiana nalo. Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa shirika hilo ni kutoa msaada wa elimu ya hali ya hewa kwa wataalamu wa anga, mabaharia, wakulima na shughuli nyingine za kibinadamu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana siku ya leo yaani tarehe 23 Machi ikajulikana kuwa Siku ya Hali ya Hewa Duniani.
Miaka 64 iliyopita katika siku kama hii ya leo katiba mpya ya Pakistan ilibuniwa na kwa mujibu wake utawala wa nchi hiyo ulibadlishwa kutoka utawala wa gavana mkuu na kuwa na mfumo wa Jamhuri. Nawabzada Liaquat Ali Khan Waziri Mkuu wa wakati huo wa pakistan alichukua madaraka ya kuiongoza nchi hiyo mwaka 1948 kufuatia kifo cha Muhammad Ali Jinnah aliyekuwa mwasisi na gavana mkuu wa nchi hiyo. Liaquat Ali Khan naye pia aliuawa na raia mmoja wa Afghanistan mwaka 1951.