Jul 14, 2025 05:45 UTC
  • Jumatatu, 14 Julai, 2025

Leo ni Jumatatu 18 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria mwafaka na 14 Julai 2025.

Siku kama ya leo miaka 236 iliyopita, gereza la kihistoria la Bastille lilitekwa na wakazi wa Paris katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa na sehemu kubwa ya gereza hilo ikaharibiwa.

Jela hiyo ilijengwa mwaka 1369 kwa lengo la matumizi ya kijeshi. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa iligeuka na kuwa gereza la kutisha ambapo ndani yake walizuiliwa wafungwa wengi wa kisiasa hususan watu waliokuwa wakiendesha harakati za kudai jamhuri nchini humo.

Gereza la Bastille lilidhihirisha udikteta wa wafalme wa Ufaransa. 

gereza la kihistoria la Bastille

Katika siku kama ya leo miaka 164 iliyopita ilitengenezwa bunduki ya kwanza ya rashasha.

Bunduki hiyo ilitengenezwa na msomi wa Kimarekani Dr. Richard J. Gatling kwa kutumia uzoefu wa wavumbuzi wa kabla yake wa silaha. Bunduki iliyotengezwa na Gatling haikuwa ya utomatiki lakini baadaye teknolojia ya kutengeneza silaha hiyo ilikamilishwa zaidi na hii leo bunduki ya rashasha inatambuliwa kuwa silaha muhimu sana katika medani za vita. 

Miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Abdul Karim Qassim alifanya mapinduzi nchini Iraq na kuuondoa madarakani utawala wa Kifalme na kisha kuanzisha mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri.

Faisal II mwana wa mfalme na Waziri Mkuu wa Iraq waliuawa katika tukio hilo la mapinduzi. Aidha wafuasi wa utawala wa Kifalme walikandamizwa na kusambaratishwa kabisa. Baada ya mapinduzi hayo, Abdul Karim Qassim aliyekuwa na mirengo ya utaifa alishika hatamu za uongozi nchini Iraq hadi mwaka 1963, wakati alipokuja kuondolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi pia na Abdul Salam Arif aliyekuwa muitifaki wake mkubwa na wa karibu. 

enerali Abdul Karim Qassim

 

Miaka 42 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 23 Tir mwaka 1362 Hijria Shamsia, duru ya kwanza ya Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na Kusimamia Kazi Zake ilianza shughulki zake.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Baraza la Wanazuoni ni moja ya nguzo na asasi muhimu katika mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini. Wawakilishi wa baraza hilo ni lazima wawe mafakihi waliotimiza masharti na huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za wananchi.

Jukumu muhimu la Baraza la Wataalamu ni kumchagua Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusimamia shughuli za utendaji wake. Uchaguzi wa baraza hilo la Iran hufanyika mara moja kila baada ya miaka minane.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, alifariki dunia Mahdi Hamidi Shirazi, malenga, mtafiti na mwandishi mkubwa wa zama hizo.

Mahdi Shirazi alizaliwa mwaka 1293 Hijria katika mji wa Shiraz wa kusini mwa Iran na kutunukiwa shahada ya udaktari katika taaluma ya lugha na fasihi ya Kifarsi.

Dakta Hamidi ameandika vitabu vingi vya mashairi ya Kifarsi, ambapo vingi vinahusiana na elimu ya mitindo, fasihi, historia na fani mbalimbali za mashairi.