Jumanne tarehe 14 Aprili 2020
Leo ni Jumanne tarehe 20 Shaabani 1441 Hijria sawa na Aprili 14 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1056 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Ibn Nadim mwanahistoria na mtaalamu wa masuala ya vitabu wa Kiislamu alifariki dunia. Umashuhuri wa mtafiti huyo unatokana zaidi na kitabu chake maarufu cha Al-Fahrast. Katika kitabu hicho Ibn Nadim amezitaja takriban elimu zote mashuhuri katika ustaarabu wa Kiislamu na kisha kufafanua maisha na historia ya wanazuoni maarufu katika elimu hizo. Kadhalika Ibn Nadim amevitaja humo vitabu na makala zilizoandikwa kuhusiana na elimu hizo.
Siku kama ya leo miaka 894 iliyopita alizaliwa Ibn Rushd, mwanafalsafa na mwanafikra maarufu wa Waislamu mjini Andalusia (sehemu ya Uhispania ya sasa). Baba na babu wa Ibn Rushd, wote walikuwa makadhi mjini Andalusia. Akiwa kijana alipata kusoma elimu mbalimbali za zama zake, huku akitabahari zaidi katika elimu za hisabati, sayansi ya elimu asilia, nyota, mantiki, falsafa na udaktari. Kufuatia hali hiyo alipewa kipaumbele na watawala wa silsila ya Muwahhidun ambao walikuwa wakiitawala Andalusia wakati huo, kiasi cha kufikia kuteuliwa kuwa kadhi wa mji wa Córdoba, mji mkuu wa Andalusia. Hata hivyo mwishoni mwa umri wake alichukiwa na watawala na hatimaye akabaidishwa. Mielekeo ya Ibn Rushd ilielemea sana kwenye fikra za Aristotle. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na ‘Tahaafut al-Tuhafat’ ‘Kitabul-Kulliyyaat’ na ‘Faslul-Maqaala.’ Ibn Rushd alifariki dunia Disemba, 1198 Miladia sawa na mwezi Swafar 595 Hijiria.
Siku kama ya leo miaka 174 iliyopita alizaliwa Friedrich Carl Andreas, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na Iran huko nchini Ujerumani. Baada ya kufahamiana na mtaalamu mmoja wa masuala ya mashariki wa nchini Denmark, alivutiwa sana na utamaduni wa Iran ambapo alianza kufanya utafiti kwa kipindi cha miaka minne katika uwanja huo. Katika kukamilisha masomo yake aliamua kutembelea nchi za Iran na India sambamba na kujifunza lugha ya Kifarsi. Kwa karibu kipindi cha miaka 30 alikuwa mwalimu wa lugha ya Kifarsi katika Chuo Kikuu cha Göttingen nchini Ujerumani ambapo wanafunzi wake walipata kufahamu tamaduni za thamani za Iran. Mtaalamu huyo wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ujerumani alifariki dunia mwaka 1930.
Siku kama hii ya leo miaka 130 iliyopita muungano wa Pan American ambao baadaye ulibadili jina na kujulikana kama Jumuiya ya Nchi za Amerika uliasisiwa. Nchi wanachama wa jumuiya hiyo zilikuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali hadi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo baada ya vita hivyo kumalizika Jumuiya ya Nchi za Amerika iliundwa kutokana na kuweko haja ya kupanuliwa zaidi mashirikiano kati ya nchi hizo. Pamoja na hayo yote kitu kinachoitia wasiwasi jumuiya hiyo ni satwa na ushawishi mkubwa wa Marekani katika jumuiya hiyo na hatua yake ya kukitumia vibaya chombo hicho kwa maslahi yake ya kisiasa. Kwa sababu hiyo nchi wanachama zinafanya jitihada kubwa za kupunguza ushawishi wa Marekani katika jumuiya hiyo.
Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, serikali ya Umoja wa Kisovieti ilitia saini makubaliano mjini Geneva na kukubali kuondoa majeshi yake katika ardhi ya Afghanistan. Jeshi la Umoja wa Sovieti liliiteka na kuikalia kwa mabavu Afghanistan mwaka 1979. Hata hivyo tangu awali majeshi hayo yalikabiliwa na upinzani mkali wa mujahidina wa Kiafghani. Vilevile Marekani nayo iliyokuwa ikiona maslahi yake yamo hatarini nchini Afghanistan, ilitumia wenzo wa kijeshi, kisiasa na kiuchumi dhidi ya Moscow ili kuilazimisha iondoke nchini Afghanistan.
Miaka 18 iliyopita katika siku kama leo, Hugo Chavez rais wa zamani wa Venezuela alirejea nchini kwake na kushika hatamu za uongozi baada ya kufeli jaribio la mapinduzi ya kumuondoa madarakani. Chavez Aliingia madarakani mwaka 1999 na kufanya mabadiliko makubwa kwa maslahi ya tabaka la chini. Vilevile alichukua hatua za kusimamia mashirika ya mafuta ya Kimarekani yaliyokuwa yakichimba mafuta ya nchi hiyo. Siasa za kujitegemea za Chavez ziliikasirisha sana Washington. Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana Marekani ilipanga na kuratibu mapinduzi mnamo tarehe 12 Machi mwaka 2002. Licha ya mapinduzi hayo kupata mafanikio katika hatua za awali, lakini wananchi wa Venezuela waliokuwa wameridhishwa na mabadiliko ya Chavez, walipinga uingiliaji wa nchi za nje katika masuala ya ndani ya nchi yao. Hugo Chavez alifariki dunia Machi 5 mwaka 2013 kutokana na maradhi ya saratani akiwa na umri wa miaka 58.