Oct 05, 2020 02:32 UTC
  • Jumatatu tarehe 5 Oktoba mwaka 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 17 Safar 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Oktoba 2020.

Siku kama ya leo miaka 546 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la  Abus-Su’ud, faqihi na mfasiri wa Qur'ani tukufu katika kijiji cha Mudarris karibu na mji wa Istanbul huko Uturuki. Baada ya kuhitimu masomo, Abus-Su’ud alijishughulisha na ufundishaji na kufanya kazi ya ukadhi mjini Istanbul, kazi aliyoendelea nayo hadi mwisho wa uhai wake. Abus-Su’ud alikuwa hodari katika masuala mbalimbali ya kijamii na aliandaa sheria za kiidara kwa mujibu wa dini ya Kiislamu katika utawala wa Othmania. Mbali na kuzungumza lugha ya Kituruki, alizungumza pia lugha za Kifarsi na Kiarabu. Msomi huyo wa Kiislamu pia ametunga mashairi katika lugha hizo. Miongoni mwa vitabu vya Abus-Su’ud ni ‘Irshadul-Aqlis-Saliim’ ‘Dua Nameh’ ‘Qanun Nameh’ na ‘Mafrudhaat'.

Katika siku kama ya leo miaka 187 iliyopita, kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Sheikh Abdul Rahim Sultanul-Qurrai Tabrizi, qaari mkubwa wa Qur’ani tukufu na mmoja wa walimu mashuhuri wa taaluma ya qiraa, huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kujifunza taaluma hiyo kutoka kwa baba yake, Sultanul-Qurrai Tabrizi alifahamiana na Sheikh Shamil Dagestani na kushirikiana naye. Wakati Sheikh Shamil Dagestani alipoandaa jeshi kwa ajili ya kupambana na Warusi, Sultanul-Qurrai alifanya safari kuelekea Dagestan ili kushiriki katika harakati hiyo. Baadaye alirejea Tabriz na kuanzisha chuo cha Qur’ani na ni wakati huo ndipo alipopewa lakabu ya Sultanul-Qurrai. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na ‘risala katika elimu ya tajwidi’ Sultanul-Qurrai alifariki dunia mwaka 1336 Hijria huko Tabriz.

Katika siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, alizaliwa Louis Jean Lumiere, mwanakemia mashuhuri wa Kifaransa. Mwaka 1895 akiwa pamoja na ndugu yake aliyejulikana kwa jina la Auguste Lumiere, walifanikiwa kutengeneza kifaa ambacho kiliwasaidia kuchukua picha mbalimbali na kusajili harakati. Mwaka huo huo Lumiere alifanikiwa kuonyesha filamu yake ya kwanza au Motion Picture katika majumba ya sinema.

Louis Jean Lumiere

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, Slobodan Milosevic dikteta wa zamani wa Yugoslavia na mhusika mkuu wa vita vya umwagaji damu huko Balkan, alijiuzulu baada ya miezi kadhaa ya malalamiko ya ndani na vikwazo vya kimataifa. Milosevic alikuwa rais wa Serbia tangu mwaka 1990 hadi 1997 na baadaye akawa Rais wa Jamhuri ya Yugoslavia. Katika vita vya Bosnia, na kwa uungaji mkono wa kila upande wa Waserbia, Slobodan Milosevic alishiriki pakubwa katika kutekeleza mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina. Milosevic alikuwa kiongozi wa kwanza mtenda jinai za kivita kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa kwa ajili ya kuhukumiwa. Hata hivyo mhalifu huyo katili alifariki dunia akiwa katika korokoro za mahakama hiyo huko The Hague nchini Uholanzi kutokana na mwendo wa kinyonga wa kushughulikia kesi yake.

Slobodan Milosevic

Na tarehe 5 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu. Siku hii ilitangazwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika tarehe 3 hadi 8 mwezi Septemba mwaka 1994 kwa ajili ya kuenzi mchango wa walimu na nafasi yao kubwa katika jamii ya mwanadamu.