Alkhamisi tarehe 29 Oktoba 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 29 Oktoba mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1495 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Masoudi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW. Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.

Tarehe 12 Rabiul Awwal mwaka wa kwanza Hijria, Mtume Muhammad (saw) aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti wa kwanza kabisa katika Uislamu katika kijiji cha Quba kilichoko pambizoni mwa Madina. Mtume (saw) aliweka jiwe la msingi la msikiti huo wa kihistoria wakati aliposimama kwa siku chache katika eneo la Quba akiwa njiani kutoka Makka na kuelekea Madina. Mtukufu huyo alisimama kwa muda katika kijiji cha Quba akimsubiri Ali bin Abi Twalib na jamaa wa familia ya Mtume.

Katika siku kama ya leo tarehe 12 Rabiul Awwal miaka 1201 iliyopita, alifariki dunia Imam Ahmad bin Hanbal mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Baghdad, Iraq ya leo. Ahmad bin Hanbal alizaliwa mwaka 124 Hijria, katika mji wa Baghdad na kupata elimu ya kidini katika mji huo kutoka kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Shafii. Imam Hanbal alifanya safari katika miji kadhaa kama vile Kufa, Basra, Makka, Madina, Sham na Yemen kwa minajili ya kukusanya hadithi za Bwana Mtume SAW. Ahmad bin Hanbal ndiye mwasisi wa madhehebu ya Kisuni ya Hanbal na mwandishi wa kitabu mashuhuri cha hadithi cha al Musnad.

Katika siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri uliasisiwa nchini Uturuki kwa uongozi wa Rais Mustafa Kemal mashuhuri kwa jina la Ataturk. Kemal Ataturk aliiongoza kidikteta nchi hiyo kwa muda wa miaka 15 na kufanya hujuma za kufuta sheria, nembo pamoja na matukufu ya Kiislamu na wakati huo huo, kueneza utamaduni na nembo za Kimagharibi nchini humo. Hata baada ya kufariki dunia kiongozi huyo aliyekuwa na uadui na Uislamu mnamo mwaka 1938, njama hizo dhidi ya Uislamu nchini Uturuki ziliendelezwa na wafuasi wake.

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, askari jeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia Peninsula ya Sinai iliyoko Misri. Mashambulio hayo yalianza baada ya Rais wa wakati huo wa Misri, Gamal Abdul Nassir kutaifisha mfereji wa Suez. Siku mbili baada ya mashambulio hayo, Uingereza na Ufaransa zilipeleka majeshi yao pembezoni mwa mfereji huo kwa lengo la kuusaidia utawala ghasibu wa Israel. Mnamo mwaka 1957 majeshi vamizi ya Ufaransa, Uingereza na utawala haramu wa Israel yaliondoka katika ardhi ya Misri kufuatia mashinikizo ya fikra za waliowengi, madola mengi ya Magharibi na upatanishi wa Umoja wa Mataifa.

Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, katika jinai yao nyingine, Wazayuni waliwauwa kwa umati wakazi wa kijiji cha Kafr Qasim huko Palestina. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walitangaza utawala wa kijeshi katika kijiji hicho. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni waliwauwa kwa umati wanawaume, wanawake na watoto madhlumu wa Palestina wasiopungua 49 na kujeruhi makumi ya wengine huko Kafr Qasim.

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Aban 1359 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Muhammad Hussein Fahmideh, kijana shujaa wa Kiirani kwenye vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Shahidi Fahmideh alielekea kwenye medani ya vita akiwa na umri wa miaka 13 tu, ikiwa imepita miezi michache tu baada ya kuanza kwa vita hivyo. Shahidi Fahmideh alijitolea mhanga kwa kujifunga kiunoni maguruneti na kujilaza mahala kilipokuwa kikipita kifaru cha adui na kuwatia kiwewe na hatimaye kuwalazimisha wavamizi kukimbia. Hatua hiyo ilipongezwa na Imam Khomeini ambaye alimtaja kijana huyo kuwa ni kiongozi na kigezo cha kuigwa.
