Jumatatu tarehe 22 Februari 2021
Leo ni Jumatatu tarehe 10 Rajab 1442 Hijria sawa na tarehe 22 Februari 2021.
Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita alizaliwa Abdullah Bin Hussein maarufu kwa jina la Ali Asghar, mtoto wa Imam Hussein Bin Ali Bin Abi Twalib (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Ali Asghar alizaliwa kipindi ambacho Yazid Bin Muawiya ndio kwanza alikuwa ameshika uongozi na kuanzisha mashinikizo na vitisho dhidi ya baba yake, Imam Hussein (as) akimtaka atoe baia na kiapo cha utiifu kwake. Kwa kuzingatia kuwa mjukuu huyo wa Mtume alimtambua Yazid kuwa mtu muovu na asiyefaa, alikataa kutoa baia kwa mtawala huyo. Ni kwa msingi huo ndio maana siku 18 baada ya kuzaliwa mwanaye huyo (Ali Asghar) akaondoka mjini Madina akiwa pamoja na watu wa familia yake. Nafasi muhimu ya mtoto huyo ilikuwa katika jangwa la Karbala, Iraq wakati wa vita kati ya jeshi la Yazid na Imam Hussein (as). Wakati wafuasi wote wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) walipokuwa wameuawa shahidi, Imam Hussein alimchukua mtoto wake mchanga aliyekuwa na umri wa miezi sita kipindi hicho na kutoka naye nje ya hema kwa lengo la kumuombea maji kutokana na kiu kali iliyokuwa ikimsumbua. Maadui hao wa Uislamu waliokuwa wamewazuilia maji watu wa familia ya Mtume hawakuwa tayari kumpatia maji mtoto huyo mchanga na badala yake Harmalah Bin Kahil al-Asadi, kutoka katika jeshi la Yazid na bila ya huruma alimlenga mtoto huyo kwa mshale wenye ncha tatu ulioikatakata shingo yake na kumuua shahidi Ali Asghar.

Siku kama ya leo miaka 1247 iliyopita sawa na 10 Rajab 195 Hijria, alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina, Imam Muhammad Taqi mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume SAW. Imam Taqi Al-Jawad AS alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ridha AS. Mtukufu huyo alikuwa maarufu kwa lakabu ya 'Jawad' yenye maana ya mtu mkarimu mno, kutokana na ukarimu wake mkubwa. Nyumba ya Imam Jawad ilikuwa kimbilio la wahitaji waliokuwa wamekata tamaa na walitaraji Imam huyo awakidhie shida na mahitaji yao ya dharura. Sambamba na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam mwema huyu, tunakunukulieni maneno ya hekima ya Imam Muhammad Taqi AS ambaye amesema: "Kila mwenye kuwa na imani na Mwenyezi Mungu, basi Allah humuokoa na kila baya na kumhifadhi na kila uadui."

Miaka 63 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 22 Februari mwaka 1958, Abul Kalam Ahmad Azad, msomi, khatibu na mwanasiasa wa India alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 70. Abul Kalam Azad alianza harakati za kisiasa akiwa na umri wa miaka 17 na harakati zake zilikuwa dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza kwa shabaha ya kuwazindua Waislamu wa India. Msomi huyo alifungwa gerezani mara kadhaa na wakoloni wa India, kutokana na hatua zake za kuchapisha na kutoa hotuba zenye kufichua ukandamizaji wa Uingereza. Mara baada ya India kuwa huru, alichaguliwa kuwa mbunge na Waziri wa Elimu na Malezi wa nchi hiyo.

Tarehe Nne mwezi Esfand miaka 41 iliyopita, Ayatullah Dakta Muhammad Husseini Beheshti aliteuliwa kuwa mkuu wa kwanza wa Mahakama Kuu ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hatua hiyo ilichukuliwa na Imam Ruhullah Khomeini baada ya kupasishwa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu na kuundwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge. Dakta Beheshti alikuwa miongoni mwa wanafikra wakubwa na shakhsia mashuhuri wa Mapinduzi ya Kiislamu. Msomi huyo aliuawa kigaidi katika shambulizi la bomu lililotekelezwa na kundi la kigaidi la MKO mwaka 1360 Hijria Shamsia.

Katika siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, Haram mbili takatifu za Maimamu al Hadi na Hassan al Askari katika mji wa Samarra nchini Iraq, ziliharibiwa vibaya kwenye mlipuko wa mabomu kadhaa. Maimamu hao ni wajukuu na watu wa nyumba ya Mtume SAW. Kitendo cha kuharibiwa sehemu kubwa ya haram hizo, kiliwakasirisha mno Waislamu na hasa wafuasi wa Ahlul Bayt wa Mtume SAW. Shambulio hilo lilifanyika kwa lengo la kuzusha vita vya ndani vya kimadhehebu kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni. Hata hivyo kuwa macho wananchi wa Iraq na viongozi wa kidini wa nchi hiyo kulisambaratisha njama hizo.

Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita Abdulmalik Rigi kiongozi wa kundi la kigaidi la Jundullah lenye makao yake huko Pakistan, alitiwa mbaroni katika oparesheni tata ya kiintelijinsia iliyofanywa na maajenti wa Wizara ya Usalama wa Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya kufanya mashambulizi mengi ya kigaidi, gaidi huyo katili alikuwa safarini kuelekea nchini Kyrgyzstan akitokea Dubai, Imarati, kwenda kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani. Hata hivyo wana usalama wa Iran waliokuwa wakifuatilia kwa karibu nyendo zake waliweza kuitambua ndege iliyokuwa imembeba gaidi huyo na kuisubiri iingie katika anga ya Iran na hivyo kuilazimisha kutua katika uwanja wa ndege wa Bandar Abbas wa kusini mwa Iran na baadae wakamtia mbaroni kiongozi huyo wa kundi la kigaidi la Jundullah. Rubani wa ndege hiyo alifanya jitihada kubwa za kutoroka na kutoka nje ya anga ya Iran, lakini alizidiwa nguvu na maafisa usalama wa Iran, na kulazimishwa kuishusha chini ndege hiyo kabla haijaingia kwenye anga ya Imarati. Abdulmalik Rigi alifanya jinai nyingi ikiwa ni pamoja na kutega na kuripua mabomu katika maeneo ya umma nchini Iran, kuwauwa kwa umati raia pamoja na kuwateka nyara. Rigi hakuwa na huruma hata kwa watu wake wa karibu. Abdulmalik Rigi alikiri kwamba alikuwa anapata misaada ya kila namna ikiwemo ya kifedha na kisilaha kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kama njia ya kuliwezesha kundi lake lifanye mauaji ya watu ndani ya Iran hususan katika maeneo ya kusini mashariki mwa Iran na kusababisha mizozo ya kimadhehebu katika maeneo hayo. Gaidi huyo alinyongwa tarehe 30 Khordad mwaka 1389 Hijria Shamsia sawa na tarehe 20 Juni, 2010 Milaadia yaani miezi minne baada ya kutiwa mbaroni. Kukiri huko kwa Rigi kunaonyesha wazi madai ya uwongo ya serikali ya Marekani ya eti inapambana na ugaidi.
