Jumanne tarehe 20 Aprili mwaka 2021
Leo ni Jumanne tarehe 7 Ramadhani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 20 Aprili mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1432 iliyopita yaani tarehe 7 Ramadhan mwaka wa 10 tangu kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad (saw), kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, aliaga dunia Abu Talib, ami na mtetezi mkubwa wa Mtume (saw) katika mji wa Makka. Baada ya kufariki dunia Abdul Muttalib, babu mtukufu wa Nabii Muhammad (saw), Abu Talib ndiye aliyebeba jukumu la kumlea Mtume, na akawa bega kwa bega na mwana huyo wa nduguye katika hali zote. Baada ya kupewa Utume Nabii Muhammad (saw), Abu Talib hakumwacha mkono mtukufu huyo na akasimama imara kukabiliana na washirikina wa Kikureishi. Lakini baada ya kufariki dunia Abu Talib washirikina walishadidisha maudhi na manyanyaso dhidi ya Bwana Mtume (saw), kiasi kwamba kutokana na hali ngumu mno iliyomkabili, hatimaye kwa amri ya Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo alihama kutoka Makka kwenda Madina ambako aliasisi utawala wa kwanza wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1239 iliyopita Ma'mun, khalifa wa utawala wa Bani Abbas alimlazimisha Imam Ridha (as) kukubali takwa lake la kuwa mrithi wa kiti cha ufalme baada yake. Ni vyema kuashiria kuwa uadui wa watawala wa kizazi cha Bani Umayyah na Bani Abbas dhidi ya Ahlul-Bayti wa Mutume (saw) ni wa muda mrefu. Vizazi hivyo viwili ni maarufu kwa dhulma, ukandamizaji na utesaji dhidi ya Ahlul-Bayti wa Mtume, ambapo havikusita hata kuwaua maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume wa Allah. Baada ya Ma'mun kutwaa madaraka ya ukhalifa alihofia sana taathira chanya ya Imam Ridha (as) kwa watu na kwa kuwa alikusudia kumuweka mtukufu huyo chini ya uangalizi wake mkali, huku akijionyesha kuwa mwenye mapenzi kwa Watu wa Nyumba ya Mtume, hivyo alitoa amri ya kumuondoa Imam Ridha kutoka mjini Madina na kumpeleka Khorasan (Mash'had ya leo) na kisha akamlazimisha kukubali kuwa mrithi wa kiti cha ufalme. Siku kama ya leo, yaani tarehe 7 Ramadhan mwaka 201 Hijiria, khalifa huyo aliwasilisha mbele ya mtukufu huyo suala hilo ambapo hata hivyo alilipinga. Baada ya kulipinga, mtawala huyo dhalimu alitumia vitisho dhidi ya Imam Ridha (as) ambapo baadaye alikubali tu kwa kutikisa kichwa huku mtukufu huyo akisisitiza kuwa jambo hilo halitofikiwa. Baada ya hapo mtukufu huyo alitumia fursa hiyo kuweza kueneza mafundisho sahihi ya dini ya Uislamu suala ambalo baadaye lilimfanya Ma'mun kuchukizwa na hatua yake ya kumtoa mjini Madina na ni baada ya hapo ndipo akapanga njama ya kumuua, njama ambayo ilitekelezwa sawa na tarehe 30 Swafar mwaka 203 Hijiria.
Siku kama ya leo tarehe 20 Aprili miaka 219 iliyopita Mawahabi wa Hijaz (Saudi Arabia) walishambulia mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq na kuua mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Baada ya mawahabi kushika hatamu za uongozi huko Hijaz mwanzoni mwa karne ya 19 walianzisha mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi hilo lenye misimamo na fikra za kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wengine hususan wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) na miongoni mwa mashambulizi ya mawahabi hao ni yale ya kushambulia miji mitakatifu ya Karbala na Najaf nchini Iraq tarehe 20 Aprili mwaka 1802. Miji hiyo ambayo ni mitakatifu hususan kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia kutokana na kuwa na makaburi ya watu wa kizazi cha Mtume wetu Muhammad (saw) imekuwa ikilengwa na mawahabi. Katika mashambulizi hayo mawahabi walishambulia haram ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein bin Ali mwana wa Bibi Fatima (as) huko Karbala na kuvunja quba na kaburi na mtukufu huyo na kisha wakapora mali iliyokuwa hapo. Waislamu zaidi ya elfu mbili waliuawa katika shambulizi hilo la mawahabi. Mashambulizi hayo yaliwakasirisha sana Waislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia na kuzidisha chuki yao dhidi ya mawahabi na mafundisho ya kundi hilo potofu. Mawahabi walidumisha mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na madhehebu nyinginezo baada ya kuanzishwa dola la watawala wa kizazi cha Aal Saud huko Saudi Arabia na walishambulia na kuharibu Haram ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) na za masahaba zake wakubwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.
Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, Ustadh Muhammad Taqi Shariati, mfasiri wa Qur'ani na mwanafikra wa Kiislamu wa Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. Alizaliwa mwaka 1286 Hijria Shamsia na baada ya kumaliza masomo yake ya awali alielekea katika mji mtakatifu wa Mashad hapa Iran na kuanza kusoma masomo ya dini kwa juhudi na hima kubwa. Baada ya muda mfupi alijiunga na harakati za Kiislamu za kueneza utamaduni na maarifa ya Kiislamu. Aidha akiwa mjini humo Ustadh Shariati alianzisha taasisi ya kueneza maarifa halisi ya Uislamu sambamba na kuandaa vikao vya elimu na kufundisha darsa za tafsiri ya Qur'ani.
Miaka 22 iliyopita inayosadifiana na 20 Aprili 1999, kulitokea maafa makubwa ya mashambulizi yaliyofanywa na wanafunzi wawili wa Kimarekani kwenye shule moja ya sekondari. Wanafunzi hao waliwamiminia risasi na kuwaua wanafunzi wenzao 12 na mwalimu wao na kuwajeruhi wengine 21. Wanafunzi hao waliovamia shule ya Columbine High School iliyoko Denver, jimbo la Colorado, walijiua wenyewe baada ya kufanya mauaji hayo. Mauaji kama hayo ya kutisha yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika maeneo ya umma nchini Marekani. Wataalamu wanasema uhuru wa kununua na kumiliki silaha ni miongoni mwa sababu za maafa hayo yanayotokea kila mwaka nchini Marekani.
Na miaka 11 iliyopita katika siku kama ya leo, mlipuko uliotokea kwenye mtambo wa kuchimba mafuta wa Deepwater Horizon na kuzamisha mtambo huo mali ya Shirika la Mafuta la Uingereza (British Petroleum) kulikosababisha kuvuja mafuta katika Ghuba ya Mexico. Wafanyakazi 11 wa mtambo huo waliuawa na mafuta mengi yaliyokuwa yakivuja kutoka katika kisima hicho yalisababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira kuwahi kutokea katika karne moja ya hivi karibuni huko Marekani.